Uundaji
wa maneno ni mabadiliko ya istilahi na muundo unaosababishwa na mabadiliko
ya sayansi na tekinolojia katika Nyanja mbalimbali za jamii ili kukidhi dhima
ya lugha kama chombo kinachojitosheleza katika mawasiliano. Ili kukidhi haja hii
kuna mbinu mbalimbali zinazotumika katika uundaji na ukuzaji wa istilahi ya
maneno katika lugha. (Matinde 2012:110).
Hivyo basi uundaji wa
maneno ni ujenzi au uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa
maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya
mawasiliano. Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi,
kisiasa, kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa
mfano tunayo maneno mapya kama vile ufisadi, uwekezaji, ujasiriamali, ukeketaji
na mengine mengi kutokana na mabadiliko ya kijamii.
Zifuatazo
ni mojawapo ya njia za uundajia wa maneno katika lugha ya Kiswahili:-
I.
UTOHOZI:
Ni mbinu ambayo maneno
kutoka lugha chanzi hutoholewa toka lugha chanzi na hatimaye hufanyiwa
marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha
pokezi kabla ya kutumiwa. Neno linapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa
utaratibu wa lugha pokezi, hata hivyo maana ya neno lililotoholewa
hubakia ileile ya awali. Matinde, (2012 :114).
Mifano:
KIINGEREZA
|
KISWAHILI
|
Switch
|
Swichi
|
Lorry
|
Lori
|
Budget
|
Bajeti
|
Agenda
|
Ajenda
|
Biology
|
Baolojia
|
Dollar
|
Dola
|
Oxygen
|
Oksijeni
|
Ubora
wa mbinu hii:
i)
Mbinu hii ya utohozi ni mbinu rahisi ya kutumiwa katika uundaji wa msamiati.
Mzungumzaji yeyote anaweza kutumia mbinu hii hata bila kuhudhuria kozi
yoyote ya isimu au kufundishwa.
ii)
Maneno mengi huweza kuundwa kwa kutumia mbinu hii ili kukidhi mahitaji ya
matumizi katika lugha mbalimbali.
Udhaifu
wa mbinu hii.
i)
Mbinu hii hulemaza ubunifu wa wanajamii katika kuunda msamiati mpya wenye
kuakisi utamaduni wa jamii husika.
ii)
Lugha tohoaji huonekana kukosa uasilia yaani lugha huonekana kuwa chotara.
iii)
Baadhi ya maneno katika Kiswahili ambayo yametoholewa kutoka lugha ya
kiingereza katika lugha ya
Kiswahili hutamkwa kwa namna tofauti kabisa.
Mifano;
KIINGEREZA
|
KISWAHILI
|
Data
|
Data,
deta
|
Dance
|
Densi,
dansi
|
Bank
|
Bank,
benki
|
Radio
|
Redio,
radio
|
Hivyo
basi, kutohoa maneno toka lugha nyingine ni ile hali ya lugha fulani kuchukua
maneno toka lugha nyingine yaani kila lugha ina tabia ya kuchukua maneno toka
lugha nyingine ili kukidhi mahitaji ya msamiati.
Maneno kutoka lugha
nyingine yanapotoholewa hubadilishwa kimatamshi ili yafuate kanuni za lugha
husika.
Katika lugha ya Kiswahili
maneno yanayotoholewa hayana budi kusanifishwa na baraza la Kiswahili la Taifa
ndipo yaruhusiwe kutumiwa rasmi.
Mifano mingine ya maneno
yaliyotoholewa kutoka lugha nyingine ni kama ifuatayo:-
Dukani
kihindi
Salamu
kiarabu
Kitivo
(kipare)
Ikulu
(kigogo/kisukuma).
Bunge
(kigogo).
II. TAFSIRI.
Matinde, (2012) anadai
tafsiri ni mbinu ya kuunda maneno ambapo maneno au vifungu katika lugha chanzi
hufasiriwa katika lugha lengwa. Ufasiri huu huzingatia muundo wa lugha pokezi.
Mifano,
KIINGEREZA
|
KISWAHILI
|
Free
market
|
Soko
huria
|
Ruling
part
|
Chama
tawala
|
Ubora
wa mbinu hii.
Mbinu hii huzingatia
kigezo cha maana zaidi kuliko muundo wa maneno yaliyochukuliwa toka lugha
chanzi na kutafsiriwa huafiki utamaduni wa lugha lengwa. Hali hii husaidia
katika kuunda maneno yenye maana iliyo wazi na inayokubalika katika lugha
lengwa.
Udhaifu
wa mbinu hii.
Mara nyingi huwa vigumu
kutafsiri baadhi ya manenotoka lugha chanzi kwa kufuata kigezo maana.
Kuna uwezekano wa kupata
tafsiri ambazo hazina maana wala mantiki katika lugha lengwa.
Mfano.
Kitchen party
- sherehe ya jikoni.
Things fall apart
- vitu vilivyoanguka na kutapakaa.
III.
UFUPISHAJI:
Rubanza (1996) anaeleza
kuwa baadhi ya majina ya maneno katika lugha nyingine za dunia hutokana na
ufupishaji wa maneno yanavyotumiwa kwa pamoja kwa kutumia herufi au silabi za mwanzo
tu za maneno hayo. Njia hii ameita Akronimu.
Matinde (2012) anaeleza
kuwa ufupishaji ni mbinu ambayo hutokana na kitenzi ‘fupisha’ chenye maana ya
kufanya kitu kiwe kifupi au kupunguza urefu wa kitu.
Kwa mujibu wa Rubanza
(1996) njia ya ufupishaji imegawanyika katika sehemu kuu mbili kama ifuatavyo:-
a. Akronomi.
Kwa mfano katika Kiswahili
tuna maneno ambayo yametokana na herufi au silabi za mwanzo za maneno kama
vile:-
UKIMWI
-
Ukosefu wa Kinga Mwilini.
TUKI
- Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
BAKITA
- Baraza la
Kiswahili Tanzania.
TAKUKURU
- Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa.
KKKT
- Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania.
b.
Uhurutishaji.
Uhurutishaji ni tendo
jingine linalokaribiana na tendo la akronimi, katika tendo hili vijisehemu vya
maneno huwekwa pamoja kuunda neno jipya. Mfano katika lugha ya Kiswahili
tunaweza kupata maneno kama vile:-
Chakula cha
jioni -
Chajio.
Hati za
kukataza -
Hataza.
Mama mdogo
-
Mamdo.
Chakula cha mchana -
Chamcha.
Vijisehemu vilivyowekwa
pamoja si lazima viwe vyanzo vya maneno.
c.
Ufupishaji Mkato (clipping).
Matinde, (2012)
anatofautiana na Rubanza (1996) kwa kuongeza mbinu nyingine ya ufupishaji
ambayo ni ufupisho mkato (clipping). Katika mbinu hii baadhi ya vipashio au
silabi hudondoshwa na kuacha sehemu tu ya neno asilia.
Mifano.
NENO
ASILIA
|
KIFUPISHO
|
Dar
es salaam
|
Dar
|
Shemeji
|
Shem
|
Morogoro
|
Moro
|
Dada
|
Da
|
Binamu
|
Bina
|
IV.
KUINGIZA MANENO YA LAHAJA NA LUGHA ZA KIBANTU.
Hiki ni chanzo kingine cha
upatikanaji wa istilahi za Kiswahili.
Dhana
ya Lahaja.
Lahaja ni namna
tofautitofauti za kuzungumza lugha moja. Aina hizi tofauti za kuzungumza
lugha moja haziwazuii wazungumzaji kuelewana. Mgulu, (1999:17).
a.
Kuingiza maneno kutoka lahaja za Kiswahili.
Mifano.
Wawe
- kipate au kiamu
Mbolezi
- kimvita.
Tungomsele
- kiamu
b.
Kuchukua kutoka lugha nyingine za kibantu.
Njia ya kuchukua istilahi
kutoka lugha ya kibantu imekuwa ikitumika kuongeza istilahi za Kiswahili.
Mifano.
Ngeli
- Kihaya
Bunge
- kigogo
Ikulu
- kisukuma
V. KUBUNI.
Matinde (2012) anasema
ubunifu ni mbinu ya kubuni msamiati katika lugha husika na kurejelea dhana au
vitu vipya ambavyo hapo awali havikuwepo katika jamii husika. Ni mbinu ambayo
hutumiwa badala ya kuchukua maneno kutoka lugha nyingine. Mfano kubuni kwa kuongozwa
na vigezo maalum kama ifuatavyo:-
Uakisi
wa umbo la kirejelewa.
Kuna leksia za Kiswahili
ambazo huakisi umbo la kiashiriwa.
Mifano ya maneno.
Neno ̔ Nyoka’
huibua taswira ya kitu kilichonyooka.
Neno ‘pembe kali’
hurejerea umbo lenye pembe iliyo na digrii pungufu ya 90.
Neno ‘kidole tumbo’
(appendix) huakisi umbo la sehemu ya mwili inayorejelewa ambayo ni kifuko
kama kidole ambacho kipo sehemu ya chini ya utumbo mkubwa.
Uakisi
wa sauti au mlio.
Uakisi huu hubainika pale
ambapo leksia huhusika kudhihirisha mfanano wa kisauti au mlio baina yake na
kirejerewa.
Mifano.
Pikipiki
mlio, pik… pik… pik…
Kuku
mlio, ku… ku… ku…ku…
Cherehani
mlio, cherr…cherr…cherr…cherrr…
Uakisi
wa tabia.
Baadhi ya leksia katika
lugha huakisi tabia za kirejelewa, kwa mfano neno ‘Kifaurongo’ ambalo
limeundwa kutokana na maneno mawili ‘kufa’ na ‘urongo’. Huyu ni mdudu
apatiakanaye kwenye kokwa la embe ambaye akiguswa hujikunja na kukaa kimya kama
amekufa. Hivyo basi neno kifaurongo huakisi tabia ya mdudu huyo.
Mfano mwingine ni ‘kinukamito’
ambayo imeundwa na maneno mawili ‘nuka’ na ‘mto’ hurejelea mtu anayeoa na
kuacha mara kwa mara (asiye na msimamo).
Uundaji
wa Maneno
Katika sehemu zilizotangulia, tumeangalia kwa ujumla dhaha za
msingi na kanuni zinazotumika katika taaluma ya mofolojia, na kutoa mifano
kutoka lugha mbali mbali. Katika sehemu hii tutaangalia jinsi lugha
zinavyotumia kanuni za namna hiyo katika kuunda maneno. Kwa kuanza mjadala,
tuangalie maneno ya orodha mbili zifuatazo:
A
a) mtu
b) mti
c) kisu
d) ndizi
e) sema
f) imba
g) ona
b) mti
c) kisu
d) ndizi
e) sema
f) imba
g) ona
B
a) somo
b) ushindi
c) kiongozi
d) mwanafunzi
e) semesha
f) imbia
g) onana
b) ushindi
c) kiongozi
d) mwanafunzi
e) semesha
f) imbia
g) onana
Maneno ya kundi (A) tunaweza kuyaita maneno-asili, kwa
sababu hayakutokana na mashina au mizizi ya maneno mengine, yaani hakuna
kipashio kilichoongezewa katika mzizi ili kuunda neno jipya. Lakini maneno ya
kundi (B), tutakubaliana, yameongezewa vipashio vya ziada na vipashio hivyo
vimesababisha kutokea kwa maneno mapya. Maneno ya kundi (B) tuyaite maneno-unde,
kuyatofautisha na yale ya kundi (A). Ni muhimu kuona tofauti iliyopo kati ya
maneno ya makundi haya mawili. Maneno yote ya hapo juu tunaweza kuyakatakata
katika mizizi na viambishi, na kupata mofimu tofauti kwa kila neno. Jambo
muhimu hapa ni kazi za vipashio vinavyounda maneno ya kundi (A) na vile
vinavyounda maneno ya kundi (B). Baadhi ya wana-sarufi wanaweka tofauti kati ya
uchambuzi wa maneno ya makundi haya kwa kuuita ule wa maneno ya kundi (A)
MOFOLOJIA-AMBISHI, na ule wa kundi (B) MOFOLOJIA-UNDAJI. Tunaweza kusema kuwa
kilichofanyika katika maneno ya kundi (A) ni kuweka viambishi katika mizizi ya
manenu hayo, ili kuonyesha ngeli katika (a-d), na kuweka irabu /a/ kuonyesha
udhihirisho wa kitenzi katika (e-g).
Maneno ya kundi (B) ni changamano zaidi. Maneno haya yamewekewa
“viundaji”, yaani vipashio ambavyo kazi yake ni kuunda maneno mengine kutokana
na mizizi hiyo hiyo. Hivyo neno {somo} ni nomino-unde, kwa sababu
limetokana na kitenzi {soma}, na kipashio /-o-/ kilichowekwa baada ya
mzizi {sem-} ni mofimu-undaji, na kikazi ni kiundaji-nomino. Neno
“jipya” {somo} linaingia katika ngeli ya 5 na wingi wake ni {masomo}
ambalo linaingia katika ngeli ya 6. Katika (B) neno {ushindi} linatokana
na mzizi {shind-} ambao umeongezewa kiundaji nomino /-i-/ na kuwekewa kiambishi
ngeli /u-/, na hivyo kuliingiza neno hilo katika ngeli ya “nomino dhahinia”
iliyo na maneno mengine kama {uuri, ukubwa} n.k. Neno la (c) {kiongozi}
tumekwisha lijadili katika 4.0 hapo juu, nalo linatokana na mzizi wa kitenzi
{ongoz-} ambao umewekewa kiundaji-nomino /-i/ kama neno lililotangulia, lakini
limepewa kiambishi ngeli /ki-/. Neno linalofuata, {mwanafunzi} ni
changamano zaidi kwa sababu linatokana na mizizi ya maneno mawili {-ana} na
{funz-}. Mzizi wa neno la kwanza ndio umechukua kiambishi-ngeli /mu-/, ambapo
lile la pili ndilo linachukua kiundaji /-i/. Maneno kama haya yanaitwa ambatano,
kwa vile kimsingi ni maneno mawili yaliyowekwa pamoja ({mwana} na {mfunzi}).
Mifano hii michache inaonyesha njia tofauti zinazotumiwa kuunda
nomino za Kiswahili kutokana na maneno ya makundi mengine. Kanuni za uundaji wa
maneno ni tofauti katika kila lugha, lakini uundaji wa maneno ni jambo la
kawaida sana. Kwa mfano, maneno yafuatayo ya Kiingereza ni maneno-unde: {childhood,
cleanllness, helpful} n.k. (Kutokana na maneno {child, clean, help}).
Kwa wana-sarufi wengi, mofolojia-undaji hasa inashughulikia kanuni za namna hii
katika lugha tofauti, yaani kanuni za uundaji wa maneno ya kundi moja kutokana
na mizizi ya makundi mengine tofauti.
Uingizaji wa maneno (22.B:e-g) hapo juu katika mofblojia-undaji
unaleta utata kwa sababu maneno haya yanabaki katika kundi la vitenzi na hivyo
si “tofauti” na vitenzi-sahili kama {sema, imba, ona} (lakini angalia
mjadala katika 4.4). Hata hivyo, kinadharia, hakuna tofauti kati ya kanuni za
uundaji zinazotumika katika maneno haya na zile zinazotumika katika maneno ya
(B: a-d). Kama vile ambavyo tumeweza kuainisha viundaji nomino -/i/ na /-o/,
tunaweza kuainisha viundaji-vitenzi /-esh-/, /-i-/, na /-an-/ ambavyo
vimeongezwa katika mizizi ya vitenzi-sahili {sem-a, imb-a, on-a}.
Viundaji hivi pia vinatumika katika kuunda vitenzi vya Kiswahili kutoka makundi
mengine ya maneno, kama sifa na nomino: {safi: safisha; fupi: fupisha;
neema: neemesha}, n.k. Katika msingi huo basi, {sema} na {semesha}
ni maneno mawili tofauti kama yalivyo {ongoza} na {kiongozi}.
Hivyo tunaweza kusema kuwa neno {semesha} ni kitenzi-unde kinachotokana
na mzizi {sem-} ambao umeongezewa kiundaji {-esh-}; na maneno mengine tunaweza
kuyaelezea kwa njia kama hiyo.
Maneno-unde katika lugha kama ya Kiswahili ni mengi sana, na jambo
hili ni muhimu kwa sababu linasaidia kurahisisha mawasiliano. Mzungumzaji
anaweza kuhusisha mara moja maana ya neno-unde kutokana na maana anayoijua ya
neno-sahili lililokuwa msingi. Vile vile, viundaji katika lugha, kila
vinapotokea, vinabakia na maana karibu ile ile, hivyo hata kama mzungumzaji
hajalisikia neno-unde kabla, anaweza kubuni maana yake ikiwa anajua maana ya
shina la msingi. Kwa mfano, si vigumu kwa mjua-Kiswahili kuona mshikamano
uliopo kati ya maneno yafuatayo: {imba: imbia: imbisha: imbika: wimbo:
mwimbaji: uimbaji}, kwa sababu anajua maana ya shina {imba} na
anajua “maana” ya viundaji vilivyotumika.
Katika utangulizi tulisema kuwa mojawapo ya maswali ambayo taaluma
ya mofolojia inapaswa kuyajibu ni uhusiano uliopo kati ya maana ya
neno-changamano na maana za vipashio vinavyolijenga. Katika kuangalia neno moja
moja, tunasisitiza zaidi taarifa za kisarufi zinazobebwa na vipashio
vinavyolijenga neno hilo. Kwa mfano, neno {masomo} limejengwa na mofimu
tatu: /ma-/ ambayo ni kiambishi ngeli, ngeli ya sita; /som-/ mzizi; na /-o/
kiundaji-nomino. Vipashio hivi ndivyo vinavyolipa neno hili maana maalumu na
hivyo kulitofautisha na maneno mengine yanayochangia visehemu vinavyoliunda
kama : {somo} (umoja wa {masomo}); {maneno} (linachangia
/ma-/ na /o/); {somea} (linachangia mzizi /som/) n.k.
Kuna swali lingine ambalo tulisema wana-sarufi wanapaswa kulishughulikiakatika
taaluma ya mofolojia, nalo ni uhusiano uliopo kati ya maneno ya lugha moja. Ni
dhahiri kuwa kuna uhusiano wa ndani kati ya maneno hayo ambao unatawaliwa na
kanuni maalumu. Uhusiano wa aina ya kwanza ni ule wa kundi. Kwa mfano,
tukisema kuwa neno mtu ni nomino, ni kwamba tumekwishaliingiza
katika kundi la NOMINO, na hivyo kukiri kuwa linaingia katika uhusiano maalumu
na maneno mengine ya kundi hilo, yaani linashiriki katika sifa zile
zinazotofautisha maneno ya kundi hilo na maneno ya makundi mengine katika lugha
hiyo moja. Huu ni uhusiano wa msingi katika lugha zote, kwa sababu kushiriki
kwa neno fulani katika kundi kunatawala matumizi ya neno hilo katika sarufi
nzima ya lugha.
Uhusiano wa aina nyingine ni kama tuliouona katika sehemu hii, kwa
mfano, uhusiano kati ya maneno-sahili na maneno-unde yanayochangia mzizi mmoja.
Mpaka sasa, mahusiano haya tumeyaangalia kwa ujumla tu, lakini itakuwa
imedhihirika kuwa kuna kanuni nyingi tofauti ambazo zinatumika katika uundaji
wa maneno na ni muhimu kuweza kuzielezea kwa uwazi ili kuona jinsi
zinavyohusiana na kanuni zinazotawala katika lugha nyingine. Kwa kufanya hivyo,
huenda tukaweza kuunda kanuni za mofolojia ya lugha-jumla. Tutazijadili
kanuni hizo katika sehemu inayofuata.
|
HITIMISHO:
Kwa ujumla uundaji wa
maneno hupanua mipaka yake ya matumizi kwa kuongeza msamiati. Lugha nyingi
ikiwemo lugha ya Kiswahili hutohoa baadhi ya msamiati kutoka lugha nyingine za
dunia kutokana na mwingiliano wa watu. Lakini hata bila kutohoa maneno kutoka lugha
nyinginezo kila lugha ikiwa pamoja na lugha ya Kiswahili kuna njia mbalimbali
zzitumikazo katika kukuza msamiati wake.
MAREJELEO.
Masebo, J. A. (2010). Nadhari
ya Lugha Kiswahili 1.Dar-Es Salaam: Nyambari Nyangwine
Publisher.
Matinde, R. S. (2012). Dafina
ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na
Vyuo
Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa
wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi
Kenya:
Longhorn Publishers.
Rubanza,Y. I.(1996). Mofolojia
ya Kiswahili. Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
Matumizi 5 ya kiambajengo
JibuFutaNimefarijika sana na utajiri huu wa lugha nzuri na adhimu ya Kiswahili
JibuFutaNaioenda mada hii kiukweli jmn
FutaNimefarijika sana maana nimepata nilichokuwa nakihitaji
JibuFutaAsante sana kwa uchambuzi na ufafanuzi aula, kongole.
JibuFutaMifano ya misimu katika uundaji wa maneno ni nini
JibuFutaNaombeni msaada sasa hivi
Safi sana
JibuFutaNimefarijika sana. Asanteni
JibuFutaVizuri
JibuFutaKazi kuntu ✌️✌️
JibuFutaNashukuru sana
JibuFutaMatatizo yepi yanapatikana katika uundaji wa maneno?
JibuFutaUkoseaji wa matamshi
Futaeleza sababu za uundaji wa isitilahinza lugha ya kiswahili?
JibuFutaBora sana👍
JibuFutaNzuri sana
JibuFutaNzuri sana
JibuFutaJe munaweza kufafanua urudufishaji hasa katika undajiwake
JibuFutaBora zaidi
JibuFutaHoja tano za uundaji wa maneno naombeni msaada
JibuFuta