MASIMULIZI

        

                                            KIBOGOYO KAOTA JINO

Mbele yangu ninaona hema nne,mkabala nazo ni hema nne pia.Hapo ndipo nilipoketi.Kando yetu kuna hema la kijani kiwiti lililotwaliwa na kwaya ya vijana pekee.Wametulia kama wale walio kwenye hema zingine.Katikati ya hema hizi kuna nafasi iliyo na umbo la mraba hivi.Upande wangu wa kushoto ndipo mambo yanatengenea kwani kuna sauti inayohanikiza  kwenye kipaza sauti. Sauti yenyewe ninaifahamu vyema.Ni sauti ya askofu Paulo.Nyuma yake kumejaa safu ya viti vyeupe na mapadri waliovaa nguo nyeupe pe pe pe kasoro askofu aliye na kilemba chekundu.Lau sivyo mtu angedhani ni theluji iliyotwaa hemani walimoketi.

'Yesu Kristo anatuambia kuwa ametuachia upendo',askofu alihubiri.

'Hakuna mapenzi yanayozidi ya mtu kuwafilia rafikize,kwa hivyo tupendane  sisi kwa sisi',alizidisha kuasa askofu Paulo.

Kusema  kweli askofu alitongoa hili na lile almuradi alihakikisha ujumbe umefika au tuseme alitaka mahubiri yatue kisawasawa ndani ya nyoyo zetu vijana.

'Lindeni pia mazingira ili kizazi  hiki na kijacho kisihangaike kwa kukosa rasilimali na pia mpigane na hayawani huyu...ufisadi.Tupigane naye toka nyoyoni mwetu.''

Kufikia hapo  askofu alitua na kunywa mafunda kadhaa ya maji aliyotiliwa na padri mmoja kwenye glasi huku akielekea kuketi

Hii ilikuwa misa ya vijana  wote wa jimbo la Mega.Sherehe hizi huandaliwa kila Jumanne ya kwanza  ya mwezi Agosti.Vigoli kwa vijulanga hutangamana kutoka dikania mbalimbali za jimbo hili ili kumwomba,kutafuta utakaso na kutubu dhambi zao kwa Maulana.Kama ilivyo ada,vijana wa kila dikania huvalia nguo zilizo na rangi au mtindo tofauti na ile nyingine.Sherehe huwa katika dikania mbalimbali kila mwaka     na leo tuko kwetu nyumbani-dekania ya mvumilivu.

Mimi nilikuwa nimevalia suruali nyeusi na fulana ya kijani kibichi,ishara tosha kwa yeyote aliyetaka kujua mimi ni  mwanadikania ya Mvumilivu.Wenzangu pia walivalia vivi hivi ila tofauti ikiwa kwenye suruali kwa wavulana na sketi kwa maghashi.Sherehe zilikuwa zinapamba moto kwani ndio mwanzo mkoko ulikuwa unaalika maua au bora zaidi mwanzo wa ngoma ni lele.

Mara kwaya ikaanza kuimba wimbo uitwao MIMINA.Wimbo huu ulikuwa ndio mwanzo umetokea tu-ulikuwa mbichi haswa! chambilecho vijana-kwani ulichezwa katika kila kituo cha radio.Ghafla utashi ulituzidi.Tukajimwaya ugani.Kila mja alinengua viungo.Raha...raha...raha na raha zaidi.Mara nikahisi nimeguswa begani.Nikaghadhabika mno kama si kubughudhika kwa kuwa nilishangaa kwa kujiuliza  ni nani huyo aliyeshitadi kuninyima starehe ilhali burudani ndio hii kila mtu achukue au ang'ang'anie sehemu yake?

'Hujambo Mraufu?'sauti nyororo ilisikika.

'Ewaaa!Sijambo Suzzy,kumbe  ni wewe?''Kauli ilinitoka baina ya shangwe huku nikijikuta ninamkumbatia kukutu bila kujua.

'Ni mimi',Suzzy alijibu.'Kumbe nawe pia umefika na kujiwasilisha papa hapa,'

'Ndio,mbona nikose ?Sitaki habari za  kusimuliwa mimi.'nilijibu.

'Safi,safi kabisa.Nimeona ukinengua mtindo fulani hapo...wauitaje eti?'Suzzy alichagiza.

'Hahaha... huo ni mtindo uitwao kiduku.Mtindo  mpya kabisa.Kuna mitindo nui lakini huu umeafiki wimbo huu barabara.Uliona nilivyokuwa nimepinda mgongo na kulegeza mikono kama Kangaroo?'

'Afanalek!Mraufu  wewe ni fundi.Itanibidi nije unifunze,nami pia niitwe guru.'Suzzy alisema.

'Bila shaka nitakusaka kokote,nikufunze uive ama uwake kama kaa la moto achia mbali kijinga chake.Ninakiona kifua chako tena dah...'

''Wewe nawe...'Suzzy alinikonyezea jicho na huyo akakimbia kwingine kusakata ngoma hii. Tukio hili la kukonyezewa jicho tena si jicho tu ila lile la kushoto ndilo lilinisisimua hisia.Kiwiliwili kikalegea mno hadi nikashindwa kuendeleza weledi wangu wa kusakata.Nilihisi nimemdondokea huyu mwana wa watu .La nilihisi ameenda na moyo wangu-mishipa ya damu ipige vipi?Niliamua kuondoka ukumbini na kurejea kitini pangu .Nilipokuwa ninaondoka ndipo mfawidhi naye anatangaza kitu fulani.

'Ahsanteni vijana kwa kutumia ujana wenu bila uwoga...Mumedhihirisha damu yenu ingali moto kwelikweli ila msipitilize moto wenyewe zaidi ya hapo.Imetosha.Kwani naona hata mawingu yamelainika,ishara  tosha kuwa Jalali ameyanyoosha ili awatizame.Kama hiki ndicho kigezo cha kuingia mbinguni...basi...ahaaa...bila shaka ninawahakikishieni kuwa mumefuzu asilimia fil mia-ole wetu sisi vijizee.'

watu  waliangua kicheko huku vijana wakifumukana kuelekea hemani pao.

'Subhana  ametulinda siku zote na kutujalia ufanisi.'mfawidhi aliendelea.Huu ndio wasaa wa kumpa zawadi zetu tulizobeba.Ninaomba tujimwaye mwaye tena ugani  lakini safari hii tukiwa na zawadi ili zibarikiwe kama vile ya Abeli na A bra...

Ghafla mtu akatokea sijui  wapi vile na kufululiza hadi katikati ya uwanja na kusimama tisti- kama parafujo za mwili- mahali kila mtu angeweza kumwona.Kila insi pale alituama.Akatokwa na macho pima kwa kuyakodoa kodo.Yumkini kila mja alipigwa na kibuhuti.

Mtu mwenyewe alikuwa na  nguo zilizochanika na kubadili rangi labda kwa kuvaliwa kwa muda wa mwaka mzima bila kuibadili.Kichwani alikuwa amejifunika kwa majani ya mbambakofi,kifuani amevalia gunia na mikononi ameliinua jiwe  kubwa.Mara akaliweka jiwe lake chini.Akaanza kupiga kwata mbele ya askofu. Mara akarejea tena katikati ya uga.Safari hii akajipiga kofi kali kwenye shavu la upande wa kulia,tena baada ya muda mfupi akalipiga shavu la kushoto.Alitekeleza haya kwa ustadi mkubwa.Bado watu walikuwa wamestaajabia kiroja hiki.Hakuna aliyedhubutu kumsogea.Nani atamsogea mtu mwenye akili taahira?

Hadi sasa hivi niandikapo,sijui ni mdudu yupi  kichwani mwake aliachilia mshipa fulani wa akili yake.Mara akainama kama jinsi wanariadha hufanya wanapojiandaa kutimka mbio za masafa mafupi. Hapo ndipo lile gunia  kifuani lilidondoka.

'Msalie mtume!'watu walistaajabia.

Kwani wakati alifanya hivyo ndipo tuling'amua ni mwanamke.Ni   bahati tu kuwa kile kiguo kibovu alichokivalia kiliweza kusitiri vya kusitiriwa kifuani pake ila tumbo lilichomoza.

'Mama yangu weeee!Hebu oneni...jioneeni tu wenyewe.Si eti hilo tumbo lililomfura ni bure.'Suzzy alianzisha dukuduku.

Nilistaajabu kumwona Suzzy nilipokuwa,kumbe alikuwa amekuja nilipokuwa nimeketi bila mimi kuwa na mwao.Labda alitaka kuona kioja hiki,la sinema hii mbashara ya bure apendavyo.

'Labda amekula maharagwe yakamharibikia ama ana uwele wa utapiamlo yule...',sauti ya mvulana aliyezichonga ndevu zake za mashavuni zikampa sura ya kupendeza ilisikika.

'Wewe ndiwe ulimpa maharagwe ama?'Sauti nyingineilisikika ikimjibu .Kicheko kikubwa kilisikika huku kikitikisa mawimbi haya woga.

'La hasha.si hayo jamani,Suzzy alisema.Kuna nunda mla watu ameamua kumlazimishia mfupa kibogoyo,sasa ona gego limeota,'lulu zilimtoka Suzzy.

'Shoga yangu sikia,waume mumetuaibisha mno.Kumbe si bure  mwaelekea mto Kitovu.Hamkomi wala hamkosi kule.Ni nani asiyejua Bi Jamvi huzidishia upunguani huko?Kumbe muliona ni shangwe mumugeuze jamvi la wageni?Haya basi kama ni vitovu mshapimanisha naye,yu wapi mmoja wenu aje hapa tena kadamnasi ya watu atuambie yeye ndiye mrina asali tumpe mzinga wake sasa?'

Bi Majuto alitoa dukuduku lake.kila mtu alishusha kichwa kutoamini na soni tele.

Huyu  alikuwa mama yake Bi Jamvi.Mwanawe aligeuzwa kiruru na jirani yake fulani kwa kutumia nguvu za kishirikina.Inaaminika Jamvi alikuwa hodari masomoni na ufanisi wake ukamwelekeza chuo kikuu akasomee udaktari.Laikini ng'o,hakumaliza hata muhula mmoja ,alirejeshwa kwao huku hata jina lake hakumbuki.Hali haikuwa hali tena.Bi Majuto hakujua be wala te ya hali hii ya mwanawe.Ninakumbuka SUzzy akiniambia usuli wa bi Jamvi baadaye.

Bi majuto alielekea alikokuwa mwanawe akamshika mkono wa kushoto na kuanza kumvuta.Mnamke akajasrika na kuja kumsaidia.Angalau alimsaidia Bi Majuto kuondoa fukuto na kani iliyompata.Bi Jamvi naye alizidiwa mara akaanza kupiga ukemi huku anabwabwaja ovyo na kujimwagia mkojo.Shughuli hii iliendelea baina ya kwikwi zake hadi alipotokomezwa asiwezekuonekana wala kusikika kwa kilio chake tena.

Tulikuwa tumeangaliana huku sauti zikisikika labda watu walihadithiana kuhusun waliyoyaona.Watu hawakujua au wasimame ama waketi.Kila  mtu alikuwa katika fikira mchafukonge.

'Poleni sana kwa yaliyotokea...huyo alikuwa mja wa Mungu ,kiumbe chake haswa!Lakini imebainika na ni wazi-kama mtu aliyepiga mwayo hutambulika kwa machozi machoni-kuwa mpanzi amepanda ila amejificha...'mfawidhu alizidisha tandabelua.Kila mtu alicheka na kuketi ishara tosha kuwa hofu ilikuwa imepungua.

'Haya basi tulete zile zawadi kisha tubarikiwe.'Mshereheshaji ali alishauri.

Kila mja aliamka na kubeba zawadi yake akimpelekea askofu.Askofu alizipokea kwa mawili na matatu huku akiwabariki kwa kuwanyunyizia maji yaliyobarikiwa.Zawadi zilikuwa tele hadi zikatengeneza mlima pale zilipowekwa.Zawadi zilikuwa tumbi nzima si mapakacha ya matunda si jozi za viatu si mavazi si vyakula.Askofu alifurahi zaidi nilipovisha koja iliyonunuliwa na dikania yetu.

Sherehe zilitamatika kwa  kupewa baraka naye askofu Paulo.

'Bwana awe nanyi''

'Awe pia nawe,'waumini walijibu

'Amubariki Mungu baba,mwana na roho mtakatifu'

'Amina,'sote tulijibu.

Kila mtu alifumukana na kuelekea nyumbani huku wakiliacha kundi la vijana likipakia zawadi kwenye gari aina ya toyota cabin. Nilikuwa ninabeta kushoto kutoka lango kuu la kanisa nichukuwe  kichochoro cha kwenda kiamboni petu,niliposikia ninaitwa.

'Mraufu...Mraufu nisubiri,'sauti hii niliifahamu,Ilikuwa ya suzzy.Kidosho niliyekuwa nikisoma naye chuo kikuu cha Mega.Anajuakujiremba ili apendeze kutokana na uzoefu wake wa uanamitindo na mienendo ya kidalji.

'Nipo ninakusubiri,'kauli ilinitoka.

'Nilimsubiri akaja hadi nilipokuwa.'Naomba chuo kikifunguka tena ,nitakuja unifunze kusakata .Sawa?'

'Bila shaka sitakubwaga muhibu,hata ukitaka mtibdo ule wa kupiga chambi,'nilisema

'Hahaha...wewew nawe huwachi stihizai.Maadamu nimeona yaliyomtokea Bi Jamvi.Nimeogopa.Sitaki mtindo huo.'

Tulicheka sote kwa utani huo.

'Nitatimiza miadi.Usihofu,'nilimhakikishia.

Nilimpiga busu la shavuni,hilo ni la kumuaga.Kisha kila mtu akashika hamsini zake,huku akili  ikiwa imeshadidi matukio ya siku,ama lilikuwa igizo jamani? Nisaidieni kwa hilo...........


MTUNZI : BW. OKELLO SETH






                                                   


                                           
        USIKU WA KIZA
      Kibwana yuko pembeni mwa kitanda chake.Anahema kwa sauti  huku jasho likimtoka na kumtiririka mwili mzima.Kutweta kwake kunadhihirisha woga alionao.Anainuka na kuketi kitandani ambamo ni mto pekee uliobaki kwani  shuka na blanketi zinaonekana zikiwa sakafuni.Shuka zinaonyesha mikunjo ya hasira,dhihirisho la vita vilivyokuwepo baina yazo na Kibwana.
    Yule alikuwa Duma au ni  Chui?”Sauti ya Kibwana ilisikika.Mbona mnyama huyo anifuate hivyo?Mwanzo nilipomwona nilidhani  ni paka aliyezoea kuchakura mle jaani lililokuwa mita themanini hivi mbali na nilipokuwa.Hali iligeuka  pale tu nilipochukua jiwe na kumgota nalo ili atokomee.Kwani niliamini kuwa paka yeyote ni pepo,achia mbali huyu wa madoadoa,Kibwana alikumbuka.Mara nikamwona akiruka  akielekea nilikokuwa huku akitoa sauti Grrrr!Grrrr!Woga ulinipanda na ikanibidi kuchana mbuga.Maskini hapo nilipokuwa ningefanya nini na hatari ilikuwa ikinikodolea macho?Ninajua wengi watasema mimi ni mwoga,siwalaumu ila ninawakumbusha kuwa,kwa mwoga huenda kicheko na kwa shujaa mwisho wake ni kilio.
Alikuwa bado yuko kwenye maruweruwe ya usingizi,alipokumbuka kisa alichosimuliwa naye Grace na woga ukamzidi zaidi.Alikumbuka Grace akimwambia kuwa usiku mmoja aligutushwa  na sauti za mbisho mlangoni,mwanzo alisita kuuendea.Alipokuwa bado anatathmini cha kufanya,alisikia sauti ya kiume ikipasua anga kwa kuliita jina lake.Kufikia hapo anakumbuka Grace akisema ilimbidi ajikaze kisabuni licha  ya woga uliomfanya atetemeke na kutetereka mithili ya unyasi kwenye kimbunga. Alipepesuka na kuelekea mlangoni na kuufungua.Salaala!Alistaajabia alichokiona.Alikuwa ana kwa ana na joka kubwa lililokuwa na kichwa cha binadamu.Grace hakujisetiri tena ila aliumwaga mkojo  sakafuni bila kutarajia.Kichwa cha joka lenyewe kilifanana na mumewe aliyeaga dunia miaka miwili iliyopita.Joka lenyewe likamweleza awatunze watoto wao na ahakikishe wamepata elimu ili wajikimu baadaye.
  Kufikia hapo,Kibwana aligutuka na kuiangalia saa yake ya ukutani iliyodhihirisha kuwa zilikuwa saa nane kamili usiku.Alijiambia moyoni kuwa ni heri alale na  kuipuzilia mbali ile ndoto yake ya awali iliyomkosesha raha.Alipiga sala kama kawaida yake baada ya njozi mbovu na ya kutisha kama hio.Aliziokota shuka na blanketi  kutoka pale sakafuni kwa mkumbo mmoja na kuamua kulala tena.Kibwana hakukuwa hata ameyafumba macho yake,aliposikia mshindo mkubwa kwenye jumba lake.Akili ikapiga kuwa sauti hio ilitokea kwenye dirisha la sehemu ya  jikoni kwani ni huko ndiko sauti ya vigae vya vioo ilisikika vilipoanguka. Kwa kweli moyo wake ulisimama kwa sekunde kadhaa huku akipanga cha kutenda.
Aliinuka pale kitandani na kunyapianyapia  kuelekea kwenye sefu yake na kuchukua sime. Baada ya hayo akakata shauri kuelekea jikoni kulikotokea sauti ya purukushani.Akazidi kuusongea ule mlango,moyo ukaanza kupiga kwa sauti.Kusema kweli hali haikuwa hali kwa Kibwana.Pindi tu alipouinua mkono wake kuufungua mlango wa jikoni,aliiona bawaba  ikifunguka taratibu.Akaamua kujibanza kwenye ukuta lakini sehemu ile ambayo mlango ukifunguka utamziba.Mlango ulifunguka wote na akaliona jitu la miraba minne likiwa linasogea aste aste likielekea sebuleni.Kusema kweli binadamu huyu alikuwa anaogofya sana.Kwani alikuwa na kifua kipana kama gazeti lililofunguliwa tayari kusomwa.Nyama za mwili  zimejibanza vibaya vibaya kwenye kiwiliwili chake.Misuli ilijidhihirisha wazi kwani alikuwa amevalia tishati nyeusi tititi iliyombana kwelikweli na yenye maandishi mgongoni”kilicho chini ya jua ni chetu sote”
 Mara jambazi hilo likafinya swichi iliyokuwa upande wa kulia ukitokea jikoni. Mwangaza ukatamalaki mle ndani.Baadaye jambazi likatoa bastola  na kuzunguka kama pia likichunguza mle chumbani. Kwa bahati njema halikumwona,likaiendea meza iliyokuwa mbele yake na kukitwaa kitabu cha kiingereza kilichoitwa “My life in crime,”alichokuwa amekisoma jioni hio.Lilifunua kurasa kadhaa na kisha likang’ata ‘nkt!’Na kusema “Upuzi mtupu,”kisha likakigotesha kitabu  chenyewe ukutani.Wakati huo wote,Kibwana alikuwa analitazama huku hewa ameibana asije akasikika.Ni wakati jambazi lilielekea kwenye jokofu na kuinama ilikuchukua kinywaji aina ya Blue Moon ndipo Kibwana alijikaza kisabuni na kutimka mbio na kulirukia huku akiwa na nia ya kulichoma kwa ile Sime ubavuni.Akalifikia ila kabla hajalidunga,lilimkaba mkono na kumuinua juu juu  na kisha kumrusha juu ya sofa.
 Akiwa sofani,akalisikia likisema ’Unadoo nini sasa buda?Its either you relax or nitabomoa hio kichwa kwa bullet.’Kibwana akatamani kunena,ila mdomo ulikataa kufunguka .Kibwana alihisi uchungu kwenye mbavu zake.Alijaribu kuinuka ili aiokote ile Sime iliyomdondoka mkonono.Ni hapa ndipo jambazi lilimfikia na kumpiga kwa mtutu wa bunduki kwenye utosi.Kibwana aliona kitefutefu na kuhisi kichefuchefu kwa mpigo.Akiwa kwenye hali hii aliuliza ‘Unataka nini?’Kwani alifahamu fika maana ya methali ya ushikwapo shikamana.
  “ Mpumbavu mkubwa wewe,eti unaniuliza nini?Lete chapaa sasa hivi!’Kibwana akamwomba amruhusu amuletee ila asiyakatishe maisha yake ghafla.Aliruhusiwa ila kwa kusindikizwa na kuwekewa mtutu wa bastola kwenye shavu la kushoto huku amemuinua juu juu,vidole tu ndivyo vinavyogusa chini utadhani  aliamua kupumzisha nyayo zisifanye kazi zilizokusudiwa na Mola.Wakaelekea chumbani mwa kulala.wakiwa huko akalipatia bunda la ngwenje.Kisha jambazi likahesabu hela zenyewe na likahamaki na ghafla likampiga ngumi ya usoni.”Hizi ni ngapi mazee?Wewe sonko mkubwa hivi na hata wife huna unanipatia ten thousand only?”Jambazi liliuliza.
    “Hizo ndi…ndi… ndi..zo niko… na …nazo bo…bo..ss.”Kibwana alijitetea japo kwa  kugugumiza.Kibwana aliichukua simu iliyokuwa upande wake na kuidondosha pamoja na blanketi sakafuni ili isivunjike  iangukapo.Yeye binafsi hakujua alikuwa amefanya jambo la busara bali kuinusuru isiibwe.Ghafla aligongwa kwa kifaa butu kichwani.Mara damu  ikaanza kumchururika huku ikimtambaa kichwani pake.Ni hapo ndipo alianguka na kuzimia zii.
    Baada ya  kipindi kirefu cha sintofahamu,Kibwana alipata fahamu na kujaribu kuamka.Maumivu  yalimzidi na akarejea sakafuni na kulala kifudifudi.Akiwa kwenye hali hii ndipo simu ilikiriza.Akajikaza  na kuipokea .Sauti iliyotokea ilikuwa ya mtu aliyemfahamu ila aliisikia kama mwangwi tu.
Sauti ilisema “Hujambo ?Mbona hujafika kazini  leo na masaa ya kuripoti yamepita?”
‘Tafadhali …niko ha…haaali… mahu…tu …ti,’sauti hafifu yake Kibwana ilisikika ikimjibu yule aliyekuwa kule upande wa pili kisha akaidondosha simu.
 Sauti ile ilikuwa ya Grace ,kidosho ambaye alikuwa akifanya kazi naye kwenye kampuni ya kuuza magari ya Chevrolet.Kibwana  akiwa ndiye afisa mkuu mtendaji huku Grace akiwa mhazili.Grace alihaha sana na kuamua kuomba ruhusa kutoka kwa meneja wao bwana Utu Bora ili amusaidie Kibwana.Alimhadithia yaliyomsibu mmoja wao. Bila kupoteza wakati ,Utu Bora aliamua kuchukua gari lake na kumchukua Grace  ndani na kisha kulipiga moto.Walielekea kwa Kibwana kwani Grace alishawahi kumtembelea siku kadhaa za hapo awali na kujihusisha si tu kwa kupiga gumzo ,si kushiriki katika unywaji wa mvinyo na mara nyingine wangejikuta wamegandiana kwenye kumbatio ungedhani ni wapenzi wa siku nyingi.Licha ya hayo kutendeka kila wapatanapo,kuna mengine ambayo Grace hakushiriki wala kukusudia kumpa Kibwana.Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao.
    Walifika kiamboni pake Kibwana na kulikaribia lango kuu ila kulikuwa na kuta zilizokuwa zinajengwa ishara tosha kuwa karibuni lango lingesimikwa pale.Waliingia bomani mle na kupata mlango u wazi.Mle ndani mambo hayakuwa sawa kwani kulikuwa na sehemu tupu ishara kuwa kuna mali iliyoporwa.Chumba kilikuwa kimevurugika,kwani jokofu halikuwepo na chupa za pombe zilizopasuka vigae vigae na kuzagaa kote kote zilionekana.Huku vifaa vya  kielektroniki vikiwemo haswa Televisheni, Redio kaseti na kipakatalishi vikiwa vimeporwa.Grace alifululiza hadi chumba cha kulala.Alipouona mwili wa Kibwana alipiga usiahi.
’woooi!Woooi!Mola mnusuru,’Alimgusa shingoni akahisi kuwa bado alikuwa  na joto.Akapitisha mkono hadi kifuani akaona bado moyo unapiga japo kwa mbali. Bwana Utu Bora akanyanyua  rununu na kuwapigia polisi na kuwajuza kilichojiri.
“Hallo bwana afande,unaongea na Utu Bora…nimepiga kuwaarifu kuwa kuna tukio  la wizi wa kimabavu eneo la Mapozi…Aaaa… kuna vitu vya thamani vimeibwa na mhusika kujeruhiwa,”Utubora alichagiza.Sauti ya askari ilisikika ikisema.
’Twaja sasa hivi eneo hilo na tunashukuru kwa kutuarifu…asante sana mwananchi mzalendo.’kufikia hapo aliamua kuikata simu na kuelekea chumbani mwa kulala mwake Kibwana.Akamwonea huruma maskini huyu wa Maulana.Kulala kwake kulimkumbusha  mnuna wake alivyokuwa amejinyoosha kwenye baraste huko Mandera baada ya kugongwa na gari kwenye kivukio cha binadamu na kisha mhusika akatokomea asipatikane.Ilikuwa bahati tu kuwa alipitia njia hio siku hio na wakati huo akielekea zake dukani kumnunulia mnuna wake Marimba kwani alipania kumtunuku nduguye kwa ala hii baada yake kufuzu masomo ya sekondari na kutaka kusomea usanii na sanaa katika chuo kikuu baadaye.Wasamaria wema ndio walimsaidia kumwokota na kumweka kwenye gari pale barabarani na kasha yeye akampeleka hospitalini  na mwishowe akapona. Alikuwa na matumaini pia huyu atarejelea hali yake ya kawaida.Akiwa kwenye kumbukumbu hizi ndipo alisikia mngurumo wa gari la polisi na mlio wa Ambulansi zikipishana kuingia mle Kiamboni.
Askari walianza uchunguzi moja kwa moja huku matabibu wakimshughulikia mhasiriwa.Kibwana alikuwa hawezi kuongea tena ila alipepesa macho  kwa shida dhihirisho la kuwa alihisi yu taabani.Alibebwa kwenye machela hadi kwenye Ambulansi na Grace akaamua kuandamana nao hadi Royal Hospital palipoagizwa na Utu Bora apelekwe.Askari walifanya uchunguzi wao kikamilifu na baada ya masaa kadhaa wakagundua kitu kilichokuwa chini ya kiti.Kumbe ilikuwa  ni bastola iliyoachwa na jambazi baada ya kubugia mvinyo na kumfanya aisahau.Mambo mengine yalikamilishwa na wakang’oa naga kuelekea stesheni na huku Utu Bora akiachwa kwa hakikisho kuwa mshukiwa atatafutwa.
Baada ya masaa tisa hivi kupita baada ya polisi kurudi pahala pao pa kazi,Utu Bora alimwandikia Grace ujumbe kuwa  ahakikishe anampa habari zozote zitakazotokea huko na atakuja baadaye kushughulikia ada ya hospitali.Mwisho alimjuza kuwa Inspeka wa polisi amemweleza kuwa wametumia alama za vidole kwenye bastola iliyopatikana na kugundua mshukiwa kwa jina la Msudia Kilimbu mwenye jina la kupanga Mejandiye mumiliki wa bastola hio na alistakimu eneo la Mabondeni.Walikuwa wametuma askari kadhaa huko anakoishi na walifanikiwa kumfumania na kumtia mbaroni akiwa chumbani mwake akikoroma na kumwaga udenda ovyo labda ni kutokana na mvinyo aliobugia kwa wingi .Kwa hivyo kilichobaki ni mgonjwa apone na kuweza kumtambua mshukiwa ili  baadaye afikishwe kortini.

    Huko Royal Hospital,Kibwana alipelekwa hadi chumba cha wagonjwa mahututi. Kwani daktari alisema ‘He is in a critical situation and we need to speed up our actions.’Grace hakuruhusiwa kuingia mle ndani basi aliketi kwenye benchi iliyokuwa pale pahali pa mapokezi.Alipoachwa hapo akawa  anatembea na kuketi baada ya muda mfupi.Alipoketi,alikuwa mara anauweka mguu mmoja juu ya mwingine.Mara anatenganisha miguu yenyewe,mara uso anauzika ndani ya viganja vyake.Haya yote anayafanya huku macho yake yakiwa ameyagandisha kwenye mlango alimoingizwa Kibwana.Alisubiri utafunguliwa saa ngapi na cha muhimu zaidi aongee na daktari ampashe habari yoyote,iwe mbaya au nzuri zote ni habari.
MTUNZI : BW. OKELLO SETH










Maoni 2 :