Ijumaa, 22 Februari 2019

MOFOLOJIA


1.2 Mofolojia Dhana ya mofolojia imeshughulikiwa na wanaisimu wengi kama vile Matthews (1974), Hartman (1972), Richard et.al. (1985) miongoni mwa wengine. Neno hili limetoholewa kutoka kwa neno la Kiingereza morphology. Neno hili limetumika katika taaluma zingine kama vile:
Utabibu (human morphology and anatomy) Sayansi ya mimea (plant morphology) Jiografia (geomorphology)
Katika taaluma ya isimu neno hili limekuwa likitumika kwa zaidi ya karne moja na linatumiwa kwa maana ya somo au tawi la isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno na aina zake. Tawi hili la isimu hushughulikia hasa kipashio cha neno. Wanaisimu mbali mbali wameeleza maana ya dhana ya mofolojia.
Mathews (1974) anaeleza mofolojia kama tawi la taaluma ya isimu ambalo linachunguza maumbo ya neno hususan maumbo ya mofimu.
Hartman (1972) anaeleza mofolojia kama tawi la sarufi ambalo hushughulikia kuchunguza na kuchambua maumbo, fani, na aina za maneno yalivyo sasa pamoja na historia yake.
Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) inaeleza mofolojia kama tawi la isimu ambalo huchunguza maneno na aina za maneno.
Kwa ujumla, wanaisimu wanakubaliana kwamba mofolojia inaweza kugawanywa katika makundi mawili makuu:
Mofolojia ambishaji
Mofolojia nominishaji
(i) Mofolojia Ambishaji Hii ni mofolojia ya mnyambuliko wa maneno. Hapa vipashio hupachikwa na kuongezewa kwenye mizizi ya maneno na kuzalisha maneno ya ziada yenye maana tofauti. Mzizi wa neno haubadiliki kamwe. Matokeo ya minyambuliko si kupata neno jipya bali ni kuongezea maana fulani ya kisarufi katika neno hilo. Kila lugha ina taratibu zake zinazoongoza minyambuliko.
mzizi maneno yaliyonyambuliwa mtu jitu, watu cheza chezwa, chezea, chezacheza, chezeana nk. ruka rukia, rukiana, rukiwa, rukaruka, rukwa nk.
(ii) Mofolojia Nominishaji Aina hii ya mofolojia pia hujulikana kama mofolojia ya uundaji. Katika aina hii ya mofolojia, viambishi mbali mbali huongezwa kwenye mzizi wa neno tukapata neno jipya kabisa. Neno linalozalishwa huenda likawa si la aina moja na neno asilia. Kwa mfano, katika Kiswahili nomino huundwa kutokana na vitenzi.
vitenzi nomino imba wimbo, mwimbaji, kuimba, mwimbishaji
kivumishi kitenzi refu refusha
1.3 Uainishaji wa Lugha Kimofolojia Somo la mofolojia linatokana na hamu ya wanaisimu kutaka kujua maumbo ya lugha tofauti tofauti. Katika kutekeleza jambo hili mofolojia imewawezesha wanalugha kuziainisha hizo lugha katika makundi mbali mbali kwa kuzingatia yale maumbo yake ya ndani. Uainishaji lugha kimuundo ndio umetumika zaidi kuliko aina zingine za uainishaji kwa kuzingatia miundo ya lugha mbalimbali. Jamii zifuatazo za lugha zimebainishwa.
(i) Lugha Tenganishi Katika lugha hizi maneno huundwa kwa mofimu moja moja ambayo huwa ni neno zima. Maneno katika lugha hizi hayaambishwi wala kutenganishwa katika vijisehemu vidogo vidogo. Mfano mzuri wa lugha kama hii ni Kichina ambapo tutapata sentensi kama hii:
Kichina Maana Wô mâi jûzî chî I buy orange eat Kiingereza kina sifa hii pia lakini si sana. Tazama:
She will go He will come
(ii) Lugha Ambishi Bainishi Katika lugha kama hii maneno yana viambishi mbali mbali. Viambishi vinajidhihirisha moja kwa moja na mizizi ya maneno inajitokeza kwa uwazi. Mizizi haichanganyishwi na
viambishi. Lugha kama hii ina viambishi vya awali, kati na mwisho. Kila kiambishi hudhihirisha maana fulani. Mfano wa lugha kama hizi ni pamoja na Kiswahili, Kijapani, Kifini na Kituruki. Tazama mifano ifuatayo kutoka kwa lugha ya Kiswahili.
{m} {kulim} {a} {a} {ta} {kuj} {a} {vy}{eti} {n}{zuri} {m}[toto]
(iii) Lugha Ambishi Mchanganyo Lugha ambayo huchanganya viambisho na mizizi ya maneno kiasi kwamba mtu hawezi kutenganisha viambishi na mzizi kwa urahisi. Mifano ya lugha kama hizi ni pamoja na Kigiriki, Kilatini na Kiarabu. Katika lugha hizi maneno mengi huwa changamano na husitiri zaidi ya mofimu moja. Kiingereza kina sifa hii kwa kiasi. Tazama;
mouse mice come came go went
Mifano hii ya Kiingereza inadhihirisha mchanganyiko wa viambishi vya wingi kwa mfano (mice) na wakati uliopita (came, went) na mizizi ya maneno.
Zoezi la 1.1 ?Je, somo la Mofolojia lina umuhimu gani?
Kufikia hapa, tumeangazia somo la mofolojia na matawi yake. Hebu sasa tuchunguze na kueleza dhana zinazotumika sana katika somo hili ili kuliangazia zaidi.
1.4 Dhana Mbalimbali Katika Somo la Mofolojia (a) Dhana ya Mofu Dhana hii ni gumu kufafanua hata hivyo mofu ni udhihirishaji wa mofimu kama ilivyo foni kwa fonimu. Mofu ni yale maumbo halisi yanayozua mofimu. Kwa mfano katika Kiingereza tuna neno cat kwa umoja na cats kwa wingi. Neno cat ni mofu moja inayozua mofimu ya kileksika. Neno cats ni mofu mbili inayozua mofimu ya kileksika (cat) na mofimu ya kiambishi cha wingi (s).
(b) Dhana ya Mofimu Mofimu ni kipashio kidogo cha kisarufi kilicho na maana (Hockett, 1988). Ni tamko ndogo lenye maana. Mofimu ina sifa zifuatazo. (a) Mofimu ina umbo halisi (b) Ina umbo la kifonetiki (c) Huwa na maana (d) Ina nafasi ya kisintaksia katika kuunda vipashio vikubwa vya kisarufi.
kmf. neno mtoto lina mofimu {m} + {toto} {m }- mofimu ya ngeli ya /1/ {toto} - mzizi
Ilhali neno anasoma lina mofimu zifuatazo: {a } - {na } - {som } - {a}
nafsi - wakati - mzizi - kiishio
Kuna aina kadha za mofimu.
(i) Mofimu Huru Ni mofimu zinazojisimamia kimaana na ambazo haziambatanishwi na viambishi vingine. Zinakaa peke yake na zina maana kamili. Zinajitosheleza kimaana bila kuunganishwa na viziada vyovyote kmf. kalamu, paka, taa. Aina hii ya mofimu hujitokeza kama mofimu za kileksia na mofimu za kiwamilifu (Yule, 1985).
Mofimu za Kileksia Kundi hili huwa na maneno ya kawaida pamoja na vivumishi. Mofimu hizi ndizo hubeba ujumbe au maana ya ujumbe katika sentensi kmf. Sungura, Nairobi, Kenya, kaka, kalamu, simba nk.
Mofimu za Kiwamilifu Haya ni maneno yanayotenda kazi fulani katika lugha nayo huwa ni viunganishi, vihusishi au vielezi. Tazama:
Viunganishi: lakini, aidha, bila, ilhali, lakini nk. Vihusishi: nje, ndani, juu, pekee, kwa nk. Vielezi : sana, leo, saa tatu nk.
Mofimu huru ni maneno halisi.
(ii) Mofimu Funge Mofimu funge haijitoshelezi kimaana bila viziada. Huambatanishwa na viambishi vingine kuleta maana kamili. Hazikai peke yake na lazima ziunganishwe na mofimu zingine ili zikamilike. kmf. kiambishi cha ngeli ya kwanza /m/ katika neno m-kora ni mofimu funge. Hali ya mofimu hizi kukosa kujisimamia imepelekea wanaisimu kuziita mofimu tegemezi. Zimegawanyika katika makundi mawili.
Mofimu Ambishi Mofimu hizi ni viambishi ambavyo haviwezi kujisimamia na mara nyingi havibadilishi mzizi wa neno. Kuna viambishi vifuatavyo:
mwanzo m-kulima kati a-li-tumbukiz-a mwisho som-ek-a (ek ni mofimu mwisho kabla ya kiishio cha kibantu -a)
Mofimu Nominishaji Hizi ni mofimu ambazo hutumiwa kuunda maneno mapya. Maneno yaliyoundwa mara nyingi huwa katika kikundi tofauti na maneno asilia.kmf.
kitenzi nomino pika mpishi, mapishi, upishi ongoza kiongozi, mwongozo, uongozaji
(iii) Mofimu Tata Mofimu tata huwa na maana zaidi ya moja. kmf. panda, paa, tunda, mbuzi nk.
(iv) Mofimu Changamano Huelezwa katika mkabala wa muundo. Mofimu changamano ni mofimu ambazo huundwa kwa kuweka pamoja angalau mashina au mizizi miwili ya maneno ambayo kwa kawaida huwa huru kmf. mwanahabari, mwanasiasa, kiinuamgongo.
(v) Mofimu Kapa Hizi ni aina za mofimu ambazo hazidhihiriki kwani ni za kidhahania. Mofimu kapa hazionekani katika neno. Mofimu hizi hatuzioni, hatuziandiki wala kuzitamka ijapokuwa athari zake zinahisika na kueleweka kmf. Nomino za ngeli ya 9/10 katika lugha ya Kiswahili huwa na mofimu kapa. Tazama: nguo nguo (neno hili lina mofimu kapa kwani halibadiliki katika wingi. Pia maneno kama vile samaki au maji ambayo yanapatikana katika ngeli ya 9/10. Maneno mengine katika ngeli ya tano na sita (Ji/Ma) pia huwa na mofimu kapa katika umoja na wingi; kmf. debe, kasha nk.
(vi) Mofimu Mzizi Mofimu mzizi ni ile sehemu ya mofimu ambayo haibadiliki na ambayo hubeba maana ya kimsingi ya neno. Hii ni mofimu ambayo inatufafanulia maana ya neno na mara nyingi mofimu za ziada huambatanishwa nayo katika unyambuaji. Tazama mfano ufuatao; kutokana na mofimu mzizi pik (pik-a) tunapata pikapika , pikwa, kupika, pikiwa, pikiana nk.
Zoezi la 1.2 ? 1. Bainisha dhana zifuatazo: mofu, mofimu na alomofu. 2. Huku ukitoa mifano kutoka kwa lugha ya Kiswahili, bainisha aina mbali mbali za
mofimu
Hapa juu tumeeleza aina mbali mbali za mofimu. Hebu sasa tuangalia jinsi ya kutambulisha mofimu na kuzitenga.
1.5 Uainishaji wa Mofimu Nida (1948) anaeleza mofimu kama kipashio cha kiisimu ambacho hakifanani kifonetiki na kisemantiki na kipashio kinginecho. Mofimu basi itatambulika kwa urahisi. Tazama mifano ifuatayo katika lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiingereza;
{m}{chez}{o} {ha}{ta}{end}{a} {paka} {taa} {boy} {boy}{ish} {mad} {mad}{den}{ing}
Ili kutambua mofimu kwa njia hii utalinganisha maneno yenye muundo karibu sawa kisha uyalinganishe na utenganishe mofimu za maneno. Tazama;
{pik}{a}
{pik}{i}{a} {pik}{ik}{a} {pik}{ian}{a}
1.5.1 Kanuni za Kutambua Mofimu Nida(1949) amependekeza kanuni sita za kutambua mofimu. Hizi kanuni zinategemeana na hakuna ile inayojitosheleza.
Kanuni ya kwanza inasema kwamba maumbo ambayo yanafanana kifonetiki na kisemantiki yanabainishwa kama mofimu moja. Maumbo haya yanapojitokeza huwa yanasimamia mofimu moja. Kmf. katika Kiingereza kipashio {-er} kinapounganishwa na baadhi ya vitenzi kinaleta maana ya mtu anayetekeleza kitendo fulani, na ni mofimu moja.
run runn-er dance danc-er sing sing-er
Hata hivyo wakati mwingine, kipashio hiki kinapojitokeza katika maneno mengine, kinaleta maana tofauti. Tazama; broad-er, furth-er, clean-er na smart-er
Kanuni ya pili ya kutambua mofimu ni kuangalia maumbo yenye maana moja lakini yanayotofautiana katika umbo la kifonetiki ambalo linaweza kuelezeka kifonolojia ( tunaweza pengine kueleza athari zinazotokana na sauti zinazofuata). Maumbo haya huwa ni mofimu moja ijapokuwa yanatofautiana kifonetiki lakini kisemantiki yana maana moja. Katika Kiingereza kipashio cha kinyume hujitokeza kifonetiki kwa namna tofauti tofauti ijapokuwa maana ni moja. Tazama;
{il} {il}legal
{il}literate
{im} {im}possible
{im}practical}
{in} {in}complete
{in}capable
{un} {un}necessary
{un}healthy
{ir} {ir}reversible
{ir}rational
Wakati mwingine maana hubadilika kama inavyodhihirika katika mifano hii: invaluable, incredible, infamous, ingenious, indispensable nk.
Maumbo ambayo yana maana sawa lakini yanatofautiana katika umbo la kifonetiki huwa ni mofimu moja. Mara nyingi tofauti hizi za kifonetiki haziwezi kuelezeka kwa urahisi kifonolojia na tena hazidhihirishi utaratibu maalum. Tazama mofimu ya wingi katika lugha ya Kiingereza.
boy boys {-iz} pie pies {-s) issue issues {-z}
ox oxen {-en} sheep sheep {φ}
Hatuwezi kueleza mabadiliko ya mofimu hii kwa urahisi.
Katika ngeli ya Ji/ma katika lugha ya Kiswahili tunaona sifa hii kwa kiasi ambapo sura ya umoja na wingi katika baadhi ya maneno inabadilika. Si rahisi kutambua mara moja majina katika ngeli hii. Viambishi vya wingi ( na wakati mwingine vya umoja) kwa mfano katika ngeli ya 6 vina maana moja lakini vina maumbo tofauti ya kifonetiki (wingi: ma, me na φ; umoja ji, φ ) na haviwezi kuelezeka kifonolojia.
mofimu za umoja/wingi umoja wingi (ji) (me) jino meno jiko meko ( φ ) (ma) karatasi makaratasi
umbo maumbo ( φ ) ( φ ) jambazi jambazi
debe debe
Kanuni ya nne ni kutazama maumbile ya neno. Kama maneno yanatofautiana kimaumbile tu huweza kuwa mofimu moja. Ikiwa katika maumbo tofauti inayojitokeza ni ya kimaumbile tu basi maneno haya huwa ni mofimu moja. Tazama:
foot feet
Homofoni hutambulikana kuwa mofimu moja au mofimu tofauti kwa misingi ifuatayo. Homofoni ni maneno yanayotamkika kwa njia sawa lakini yana maana tofauti. Tazama jozi za maneno yafuatayo ya Kiingereza:
meat meet flour flower pail pale threw through
bare bear tare tear sew so Kumbuka
-homofoni zenye maana tofauti huwa ni mofimu tofauti kabisa -homofoni zenye maana moja huwa ni mofimu moja
Kanuni ya sita ni kuangalia mofimu katika mikabala tofauti. Mofimu inaweza kutambulikana kama: (i) Inaweza kujitenga (kmf. mofimu huru {paka}) (ii) Inaambatishwa kwenye kipashio kinachoweza kujitenga (kmf. mofimu tegemezi
{dance} +{er} ,{pig}+{an}+{a} (iii) Hujitokeza kama kiambishi pekee kama kitengo kinachoweza kujitegemea kmf.
mwanajeshi mwana + jeshi mwana hewa mwana + hewa askarijeshi askari + jeshi mitishamba miti + shamba
Katika mifano ya (iii) hapo juu, sehemu mbili za neno zinajitegemea nazo ni mofimu tofauti.
Zoezi la 1.3 ? 1. Tumia kanuni zilizopendekezwa na Nida (1949) kuainisha mofimu katika maneno
yafuatayo; Kuangaliana, ng’oa, tembeleanatembeleana, ua, kula, choo, mwanafunzi, mwanaharamu.
1.6 Alomofu Alomofu ni maumbo tofauti ya mofimu. Alomofu ina sifa mbalimbali. (a) Umbo halisi ambalo ni sehemu ya neno. (b) Ni mofu mojawapo ya mofu za mofimu moja.
Alomofu basi ni sura tofauti za mofimu moja.
Kwa mfano alomofu za wakati ni pamoja na /li/, /na/, /ta/, /po/, /ka/ nk. Alomofu za umoja katika ngeli ya kwanza ni /m/ , /mu/ na /mw/. Tazama:
mtu watu mwalimu walimu muumba waumba
Kauli ya kutendeka ina alomofu zifuatazo:
/ek/ shoneka pondeka /ik/ pikika limika /lek/ toleka leleka /lik/ valika vulika /ikan/ takikana patikana /ekan/ onekana ezekana /likan/ julikana
tambulikana /lekan/ ?
Jinsi ya kufanyiza ina alomofu kadha wa kadha:
/iz/ fanyiza /ez/ pendeza /ish/ pigisha /esh/ endesha /liz/ tuliza /lez/ koleza /lish/ zalisha /lesh/ tolesha
Alomofu huonyeshwa kwa alama za msharazi / /.
Kufikia hapo tumeeleza somo la mofolojia, dhana zinazotumika katika somo hili pamoja na mbinu/kanuni za kutambua mofimu. Unaweza kutazama marejeleo yafuatayo kwa maelezo zaidi.
1.7 Maswali 1. Bainisha aina tofauti tofauti za mofimu kwa kutoa mifano kutoka kwa lugha mbali
mbali za Kiafrika. 2. Tumia kanuni zilizopendekezwa na Nida (1949) kuainisha mofimu katika lugha yako
ya kwanza.
Marejeleo ya Lazima Hartman, R. 1972: Dictionary of Language and Linguistics. London: Applied Science Publisher.
Hockett, C. F. 1958: A Course in Modern Linguistics. Newyork: Macmillan.
Matthews, P. 1974: Morphology: An Introduction to the Theory of Word Structure.
Cambridge: Cambridge University Press.
Nida, E. A. 1949: Morphology: The Descriptive Analysis of Words. Michigan: Michigan University Press.
Yule, G. 1985: The Study of Language. Cambridge: Cambridge University Press.
SOMO LA 2 Uundaji wa Maneno
1.0 Utangulizi Mbali na kutuwezesha kuziainisha aina za lugha, somo la mofolojia linahusisha uundaji wa maneno, istilahi na utoaji wa maana ya maneno haya katika lugha husika (Nida, 1956). (Tutapitia haya katika somo la 2)
Katika somo hili la pili tutachunguza mbinu mbalimbali za uundaji wa maneno ambazo hutumika katika lugha kwa ujumla. Pili tutaangazia kwa jinsi ambavyo mbinu hizi hutumika kuunda maneno na istilahi katika lugha ya Kiswahili na pia tutazitathmini kwa kuangalia matatizo yanayotinga uundaji wa msamiati na istilahi katika lugha ya Kiswahili.
2.1 Shabaha Baada ya kulipitia somo hili, ninatarajia kwamba utaweza: 1. Kubainisha mbinu mbali mbali za kuunda maneno katika lugha. 2. Kutathmini mbinu hizi kwa kuonyesha ni ipi zalishi zaidi. 3. Kutoa mifano kutoka kwa lugha ya Kiswahili katika mkabala wa mbinu hizi.
2.2 Uundaji wa maneno Katika jamii, dhana, matukio na vifaa mpya huzuka ambazo huhitaji kuzungumziwa. Basi panakuwa na haja ya kuzua msamiati mpya kuzungumzia juu ya matukio haya mapya katika jamii. Baadhi ya sababu zinazofanya watu wazue msamiati na istilahi mpya ni pamoja na: 1. Kuelezea dhana mpya zinazobuniwa. 2. Kwa sababu ya maendeleo ya haraka katika nyanja mbalimbali za maarifa ya
binadamu kmf. sayansi, uchumi, teknolojia, sheria, siasa, uchumi nk. 3. Uchakavu wa maneno ya awali kmf. neno la zamani la damu katika Kiswahili ni ngeu
ambalo halitumiki tena. 4. Sababu za mila, aibu au wasifu ambazo watu hukwepa kutumia. 5. Maingiliano ya kijamii yanasababisha haja ya kuunda maneno mapya kuwakilisha
maingiliano ya jamii hizi. 6. Kufanikisha mawasiliano baina ya taasisi, matabaka na mashirika mbali mbali
Mbinu tofauti hutumika ili kuunda msamiati mpya.
Zoezi 2.1 ? 1. Kwa nini maneno katika lugha yaundwe?
2. Toa sababu ambazo zimepeleka lugha ya Kiswahili kuunda istilahi
mbalimbali.
2.3 Mbinu za Kuunda Msamiati na Istilahi (a) Mwambatano Mbinu hii inahusu kule kuunganishwa kwa maneno mawili kuzua neno moja lenye maana mpya tofauti na maneno yaliyoiunda.
N + N mwana + jeshi mwanajeshi
duara + dufu duaradufu mbata +mzinga mbatamziga mlango +mfuto mlangomfuto
N + Kt nukta + tulia nuktatuli
mwamba + dukiza mwambadukiza
N + KV ng’ombe + jike ng’ombejike
kiini + tete kiinitete mja + mzito mjamzito fundi + sanifu fundisanifu pembe + nne pembenne chungu + -zima chungunzima
Kt + N pima + mvua kipimamvua changa + moto changamoto saga + gego sagagego chemsha + bongo chemshabongo fungua + kinywa kifunguakinywa
Kt + Kt yeyusha + ungana myeyungano
Kt + KL ona + mbali kionambali
Upungufu wa mbinu hii ni kwamba: Maneno mawili yenye maana tofauti uambatanishwa pamoja kuzua neno moja, jambo ambalo lina uzito wa kisemantiki. Lakini yafaa maneno yatumike mpaka yazoeleke.
(b)Unyambuaji Katika mbinu hii viambishi vinaongezwa katika mizizi mwafaka kuizua neno mpya. Aina tofauti za unyambuaji hutokea.
(1) Unyambuaji kwa kutumia viambishi. Hapa maana mpya la neno hupanuka kupitia viambishi. kmf. Kutokana na mzizi piga - tutapata
kupiga pigo pigana mapigano
Kutokana na mizizi mingine tutapata; mzizi neno lililoundwa zuri uzuri jamaa ujamaa ulevi mlevi, vileo
Kupitia unyambuaji wa viambishi nomino huundwa kutokana na vitenzi. Kitenzi nomino tafiti utafiti chuma uchumi tawala utawala weza uwezo, mweza
(c) Kukopa Kukopa ni mbinu inayotumiwa na lugha zote za ulimwengu kurutubisha msamiati wake. Kukopa kunatokana na mambo fulani;
Huenda neno linalokopwa linasimamia kitu ambacho hakipo katika utamaduni kopaji.
Kasumba ya uzungumzaji hivi kwamba wazungumzaji hupendelea kutumia maneno fulani kuliko mengine kmf.
neno asili- neno la kukopa kuanguka-kufeli kupita-kupasi pinde- kona mungu-mola
maingiliano marefu ya kitamaduni na kijamii
Utabaka: Lugha inayohisiwa kuwa ni ya tabaka la chini hukopa kutoka kwa lugha ya tabaka la chini
Kiswahili huunda msamiati, maneno na istilahi mpya kupitia mbinu ya kuazima maneno kutoka kwa lugha zingine. Kiswahili kimeazima maneno kutoka kwa lugha za Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kihindi, Kireno, Kituruki, Kishirazi, na Kijerumani nk. Maneno yakiazimwa hubadilishwa kuchukua muundo wa KV ambao ndio asili kwa lugha ya Kiswahili. Kiswahili kimeazima maneno kutoka kwa lugha za Kiafrika pia. (Mifano tuliyotoa hapa chini imechanganyisha mbinu zote za ukopaji hata hivyo baadaye tutazungumzia juu ya mbinu tofauti za ukopaji). Lugha Kopeshaji mfano wa maneno Kishirazi mnara, nanga, kiwida Kihindi pesa, bima, laki, godoro Kituruki baruti, bahasha, korokoroni
Kireno karata, pera, bendera, mvinyo Kijerumani hela, barawani, shule Kiingereza Mei, daktari, kampuni, eropleni Kiarabu Rehema, faraja, alhamisi
Kutoka lugha zingine za Kiafrika tunapata ukopaji wa maneno kama yafuatayo;
Kinyamwezi ikulu, kabwela, bunge Kikuyu matatu Kipare kitivo Kihaya lweya Kimasai mbuti, ngalemu
Ukopaji unakuwa ni wa njia nyingi:
(i) Kukopa kwa Tafsiri Katika mbinu hii vifungu katika lugha asilia hutafsiriwa katika lugha kopaji. Kiswahili kimetumia mbinu hii kujenga msamiati na istilahi zake. Tazama mifano ifuatayo:
Commissioner General Kamishena mkuu District Officer Mkuu wa Wilaya Opposition Party Chama cha Upinzani Rainbow Alliance Muungano wa Upinde wa mvua Basic principle Kanuni Msingi Publicity Section Sehemu ya Uenezaji Electoral Commission Tume ya Uchaguzi
Upungufu wa mbinu hii ni kwamba unaweza kupata tafsri ambazo hazileti maana inayokusudiwa kmf.
mobile phone - simu za kurandaranda (simu za mikono) sick leave - likizo ya ugonjwa dictatorship - uongozi wa imla (uongozi wa kimabavu yafaa zaidi)
(ii) Utohoaji Kupitia kwa mbinu hii wanalugha wanachukua maneno kutoka kwa lugha asilia na kunukuu kwa kuangalia fonolojia ya lugha pokezi . Neno linatamkika kwa utaratibu wa lugha pokezi. Maneno yaliyotoholewa hupata maana kutokana na lugha asilia kmf.
atom - atomi virus - virusi office -ofisi
doctor -daktari
mbinu hii ina upungufu mkubwa hasa pale ambapo utaratibu maalum haufuatwi tunaweza kuzalisha zaidi ya neno moja. Tazama
dance- dansi, densi bank- banki, benki officer- afisa, ofisa
Utohozi wafaa kutilia maanani utamkaji katika lugha pokezi ili tuzue maneno yasiyo tatanishi.
(iv) Kukopa sisisi Huu ni ukopaji wa moja kwa moja. Hapa maneno yanachukuliwa yalivyo katika lugha changizi na kutumiwa katika lugha kopaji.
Neno Lugha Changizi Kitivo Kipare Ikulu Kinyamwezi Kasri Kihindi mbunge Kisukuma matatu Kikuyu
(d) Ufupishaji
Kuna mbinu kadhaa zinazotumika katika kufupisha maneno ukapata mengine mapya.
(i) Ufupishaji mkato Katika mbinu hii, neno hufupishwa kabisa na vifungu vichache hutumika. Tazama mifano ifuatayo kutoka katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Kiswahili Kifupisho
bibi bi baba ba Kiingereza Kifupisho jumbojet jumbo television teli examination exam
memorandum memo refrigerator fridge photograph photo fanatic fan papa pa
(ii) Akronimu
Kutumia silabi za mwanzo za maneno fulani katika kirai kuunda neno kmf.
Ukosefu wa Kinga Mwilini UKIMWI
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili TUKI Chama Cha Kiswahili cha Taifa CHAKITA
(iii) Uhulutishaji Ni mbinu ambayo hutumika kwa kufupisha virai kupata maneno. Mara nyingi sehemu ya mwanzo ya kirai cha kwanza huunganishwa na sehemu ya kwanza ya neno la pili kuunda neno jipya. kmf.
msikwao mtu + asiye + kwao
chajio chakula + jioni mwambayavu mwamba + kama yavuyavu mala maziwa +lala
Udhaifu wa mbinu hii ni kwamba visehemu ambavyo si vya mwanzo hutumika pia. Tazama:
huhaba huduma hadi bandarini
runinga rununu + maninga
Wakati mwingine shina nzima hutumika katika kuunda neno jipya. Tazama:
Kiua + dudu kiuadudu ute + mayai uteyai (egg yolk)
Ukosefu wa mantiki wa kutekeleza mbinu hii kwa ujumla. Hasa kwa kuamua ni kirai kipi kitakachotumika kmf. fupaja kutoka kwa mfupa wa paja, je kwa nini si mfupaja kama ilivyo mkono, mguu nk.
(e) Kubuni Hii ni mbinu ya kuunda maneno isiyo ilihamu ya kifonolojia, kimofolojia au kiothografia. Kuna njia mbali mbali za kubuni msamiati kwa kubuni. (i) kubuni kwa kinasibu (ii) kubuni kwa kuongozwa na vigezo maalumu.
Kubuni kwa kinasibu
Huku ni kuzipanga fonimu za lugha kulingana na utaratibu wa ujenzi wa lugha inayohusika iili kuunda neno ambalo halipo katika lugha . Kwa njia hii maneno mapya ya lugha huundwa kwa kuzingatia kanuni za isimu za lugha husika kisha yakapatikana dhana mbali mbali. Njia hii hutatua tatizo la kuchukua maneno ambayo tayari yapo katika lugha ya kushindiria mzigo mwingine.
ndege - kisopo golo - bureau de change
Mara nyingi neno linaloundwa halina uhusiano na dhana linalosimamiwa au kitu kinachotajwa. Tunakosa uhusiano wa kitajo na kitajwa. Pana tatizo kama watumiaji neno hilo hawakuhusishwa na uundaji wake.
Kubuni kwa kuongozwa na vigezo maalumu Vigezo kama maumbile, tabia au matumizi ya kitu vinaweza kutumiwa kuongoza kubuniwa kwa neno. Hapa tunapata ubunifu ukifuata misingi ya kionomatopea kupata majina kama vile;
pikipiki tingatinga
kengele firimbi gari la moshi kifauwongo ndege msumeno nyeleo barua pepe mtandao
Upungufu wa mbinu hii ni kwamba inamfunga mwundaji istilahi kuambatanisha neno na kitajwa, jambo ambalo haliwezekani kila mara.
(f) Uwawilishaji/ Uhamishaji Mbinu hii inahusu kuhamisha vipashio vya neno kuchukua nafasi tofauti katika neno jipya linaloundwa. Pia uhamishaji maana wa neno la awali likapata maana mpya. Tazama; -Vyaa (kwa maana ya zaa ) tunaunda avya ( kuhamisha sauti).
-Kupe (mnyama anayenyonya ng’ombe damu) linatumika kwa mtu anayetegemea mwingine -Kifaru (mnyama) linapata maana ya gari la vita
(g) Kuradidi Hii ni mbinu ya kurudia neno au sehemu ya neno ili kuleta maana mpya. Kwa mfano;
kizunguzungu pilkapilka wayowayo pikipiki polepole
(h) Ugeuzaji Hapa neno linageuzwa kutoka kikundi kimoja kisarufi na kuingizwa katika kikundi kingine. Kmf.
mchezo mchezaji okoa mwokozi, wokovu
2.4 Kumbuka!
Matatizo katika Uundaji wa Maneno (a) Maneno kubeba uzito kimaana. Tatizo hili linaweza kutatuliwa iwapo
maneno yatatumika mara nyingi yazoeleke (hasa maneno ya kisayansi na teknolojia). (b) Kuwepo kwa istilahi/maneno mbalimbali kwa neno moja kmf.
nomino, jina, nauni runinga, televisheni mavi, kinyesi, mlima, kimba (c) Kutokuwa na utaratibu maalum. Ukosefu wa ruwaza moja. Tazama mifano ifuatayo
kutoka somo la Biolojia; Plasmagene - utoroji Plasmalema - ugoziuwili Plasmadesta - kiuzichembe
Tazama pia mifano ifuatayo kutoka somo la Isimu;
base - msingi, kiini cha neno baseform - umbo msingi basecompound - neno ambatano (neno msingi lapotea katika maana ya tatu) (d) Maneno mengine yanakosa “ukubalifu wa kimataifa”. Katika biolojia kwa mfano, maneno fulani yametungwa lakini inaonekana kwamba yanakosa ukubalifu wa kimataifa na ingekuwa mwafaka zaidi kama yangekopwa na kuswahilishwa moja kwa moja.
Neno Neno lililopendekezwa Neno ambalo lina umataifa mirage mazigazi miraji hydrophte yungiyungi hidrofite hydrotropism ubadilihali hidrotropisimu
(e) Kuwepo kwa istilahi chungu nzima kwa dhana moja. Ukosefu wa kutosanifisha istilahi ni pigo kubwa. Katika somo la isimu kwa mfano, sauti za /m, n, ng' na ny/ huitwa sauti za nasali /nazali / ving’ong’o au vipua. (f) Dhana zilizotoholewa hasa katika lugha za Kiafrika ni gumu kufasiri kama mtu
hajui lugha asilia: kmf. neno lugha asilia maana Kiangata Kisiu hob Chonyo Kipemba oedima Mlulu Kipare Peata (g) Kutafsiri istilahi katika lugha za kigeni mara nyingine kunapotosha dhana ya msingi liyokuwa katika istilahi za lugha chasili kmf.
lugha msingi tafsiri Ofisi ya vipimo vya Taifa National Bureau of Standards Mapokeoni Reception
Zoezi la 2.2
?1. Jadili kwa kutoa mifano njia mbali mbali ambazo Kiswahili kimetumia kujenga msamiati na istilahi zake.
2. Onyesha kasoro za mbinu hizi. 3. Toa maoni yako kuhusu njia za kuboresha uundaji wa msamiati katika lugha ya Kiswahili.
Kufikia hapa tumeona mbinu mbali mbali za kuunda maneno na matatizo yanayotinga uundaji wa istilahi katika lugha ya Kiswahili. Hata hivyo lugha ya Kiswahili imeendelea kujitahidi katika uundaji wa istilahi na msamiati ili kufikia uasiriaji.
Marejeleo ya lazima Temu, W.C. 1984: ''Kiswahili Terminology: Principles Adopted for the Enrichment of the Kiswahili Language'' katika Kiswahili Volume 51/1 na 51/2
uk. 112 –126. Dar es Salaam: TUKI.
Mdee, J.S. 1986: ''Matatizo ya Kuunda Istilahi kama Yanavyojitokeza katika Kiswahili'' Katika Mulika uk. 47 – 69. Dar es Salaam: TUKI.
Tumbo-Masabo, Z.M. 1982: ''Towards a Systematic Terminology Development in
Kiswahili'' katika Kiswahili Juzuu 48/1 Dar es Salaam: TUKI.
SOMO LA 3 Nadharia ya Sarufi
3.0 Utangulizi Katika mada hii, nitajadili nadharia ya sarufi mapokeo kama mkondo wa sarufi. Nitaeleza pia aina mbalimbali za dhana ambazo hutumika katika mkondo huu wa sarufi. Aidha, nitaeleza aina za maneno mbalimbali yanayofungamana na nadharia hii. Mwishowe nitaitathmini nadharia hii kama mkabala mojawapo wa sarufi.
3.1Shabaha Baada ya kulipitia somo hili ninatarajia ya kwamba wanafunzi wataweza: 1. Kubainisha mikondo mbali mbali ya sarufi. 2.Kufafanua dhana mbalimbali za sarufi mapokeo. 3.Kufafanua aina mbalimbali za maneno. 4.Kutathmini nadharia ya sarufi mapokeo kama mkondo wa sarufi.
3.2 Utangulizi Uchambuzi wa lugha ambao umekuwa ukiwashughulisha wanaisimu kwa muda mrefu sasa umepita katika mikondo mitatu mikuu. Misimano hii imesababisha kuzuka kwa nadharia tofauti za sarufi ya lugha kwa kila mkondo. Nadharia hizi ni:
Sarufi Mapokeo ( pia huitwa jadi) Sarufi Miundo ( pia hujulikana kama muundo/maumbo) Sarufi Zalishi
3.3 Sarufi Mapokeo
Historia Yake Mtazamo wa awali zaidi ambao ulishughulikia lugha ulikuwa wa kifalsafa. Sarufi mapokeo iliasisiwa na wanafalsafa wa ulaya hasa Ugiriki. Hawa walishughulikia lugha tangu karne ya kumi na tatu. Wakati huu, lugha iliangaliwa kama kipengele kimoja cha uchunguzi wa taaluma nyingine (za falsafa) kama historia, fasihi, dini, mantiki na baalagha. Kule Ugiriki, kipengele cha lugha kilishughulikiwa katika taaluma ya falsafa. Wachunguzi hodari wa falsafa ya kigiriki walikuwa Aristole na Plato.
Sarufi ya awali zaidi ilitungwa na Myunani aliyeitwa Dionysus Thrax na iliitwa Techne Grammatike (The Art of Grammar). Baadaye warumi walitumia mfumo wa kisarufi wa Wayunani katika lugha ya Kilatini bila mabadiliko mengi.
Kati ya karne ya 12 hadi ya 14 kikundi cha wasomi kilichoitwa Modistae kilitoa kazi mbalimbali zilizojikita katika sarufi ya makisio. Mtazamo wao wa kisarufi ulikuwa
ukiitwa grammatica speculativa. Waliamini kwamba kuna sarufi bia moja inayohimiliwa na uhalisia na urazini wa binadamu. Kufikia karne 17, maoni tofauti ya kisarufi yaliendelezwa. Kufikia mwaka wa 1700, sarufi za lugha 61 zilikuwa zimeandikwa zikiwemo zile za Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kiitaliano.
Sarufi nyingi za mwanzo ziliandikiwa kwa makusudi ya kufundishia. Pia walitaka kuzisanifisha kupitia maandishi.
Katika kipindi hiki cha maendeleo ya sarufi, wataalamu waligawanyika kimaoni wengine wakipendekeza sarufi fafanuzi au elezi na wengine sarufi elekezi.
3.4 Misingi Ya Nadharia ya Sarufi Mapokeo Mkabala wa Sarufi Mapokeo una misingi yake katika sifa maalum ambazo zinaibainisha sarufi hii. Nadharia ya sarufi mapokeo basi inajikita katika misingi ifuatayo:
Lugha iliyochukuliwa kuwa msingi wa sarufi ilikuwa Kilatini. Hii ni kwa sababu mambo mengi ya kitaalamu wakati huo yalichunguzwa na kuandikwa kwa Kilatini. Lugha ya Kilatini ilikuwa mojawapo ya lugha awali sana kuwa na maandishi. Lugha zote zilichunguzwa kwa misingi ya Kilatini. Lugha zote ulimwenguni zilichukuliwa kuwa na sarufi moja. Kwa muda mrefu lugha ya Kilatini ilichukuliwa kama kielelezo cha matumizi ya kiwango cha juu kabisa cha lugha. Kwa hivyo wanamapokeo, walichunguza na kuishilia na kanuni na sheria zilizoeleza matumizi yake. Kanuni hizi zilichukuliwa kama kigezo cha kuchambulia lugha nyingine za ulimwengu – hata Kiingereza. Kmf. Kilatini kina sifa ya kunyambulika kwa maneno. Kwa kutumia kigezo hiki wanamapokeo walikiona Kiingereza kuwa na chembe za sarufi kwani hakina sifa hii sana kikilinganishwa na Kilatini ilhali Kichina ambacho hakina tabia hii kilisemekana kuwa hakina sarufi.
Kutumia Kilatini kama kigezo cha kupimia lugha zingine ni makosa kwani kila lugha ina sauti, mitindo, mbinu na sarufi ya kipekee. Isitoshe maoni kwamba lugha zote zinafanana kimuundo na kiumbo ni dhaifu. Lugha zinatofautiana kwa njia mbalimbali. kmf.. Kwa upande wa msamiati tutapata maneno kama haya; Kiingereza Kiswahili Kitharaka Gikuyu Kikamba water maji ruji mai kiw'u
Mawazo kama haya yalizusha maoni kwamba hadhi ya Kilatini ilikuwa ya juu zaidi. Hata hivyo lugha zote ni sawa kihadhi. Kila lugha inatimiza mahitaji ya wazungumzaji wake kijamii. Tazama jamii nyingi za Kiafrika ambazo hazina maneno asili ya dhana kama condom, computer, missile na rocket. Lakini zina maneno yanayoshughulikia maisha ya kawaida ya jamii.
Sarufi mapokeo ilipendekeza kanuni za lugha Sarufi mapokeo ilieleza kwa jinsi ambavyo mtu anatakiwa kuongea na kuandika. Kulikuwa na kanuni ambazo zilipasa kufuatwa katika kutumia lugha kwa njia sahihi. Wanamapokeo walitoa sheria zilizoelekeza namna ya kutumia lugha. Udhaifu wa kufanya hivi ni kwamba sarufi haipaswi kuwa ya kulazimishwa inapaswa kuwa ya
kueleza. Walisahau kwamba sarufi yapaswa kuangalia lugha kama ilivyo na kuieleza sio kulazimisha sheria. Wazungumzaji hawatungiwi kanuni za jinsi ya kuongea lugha yao. Kila mzungumzaji wa lugha fulani anazifahamu sheria za lugha yake bila sheria hizo kutolewa wala kuandikwa. Sheria za lugha ni za kiasilia. Kwa kutumia umilisi wake, mzungumzaji asilia anafahamu sheria zinazoongoza kwa mfano; wingi/uchache, ukubwa nk.
Kazi za kisanaa zilihusishwa na falsafa. Kazi mbalimbali za wasomi mashuhuri wakati huo zilichukuliwa kuwa ndizo zilizotumia lugha kwa njia sahihi zaidi. Matumizi ya lugha nje ya ilivyotumika katika kazi hizi yalichukuliwa kuwa ni makosa. Hivyo mtazamo wa lugha ukawa kuwa mabadiliko ya lugha yalikuwa ya kuharibu na kuwa hatua ya awali ya lugha fulani ilikuwa bora na sahihi zaidi kuliko hatua ya baadaye. Udhaifu wa mawazo haya ni kwamba walichukulia kwamba lugha haikui. Kutokana na maoni haya vitabu vya sarufi vilivyoonyesha kanuni za utumiaji sahili wa lugha vilitungwa.
Walionelea lugha kuwa ni ya kionomatopea Wanamapokeo walionelea kwamba kulikuwa na uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno na kile kinachorejelewa na neno hilo. Maneno kama kengele, tingatinga na pikipiki – yanatokana na sauti inayotolewa na vyombo hivi. Katika lugha nyingi za ulimwengu sio maneno yote ambayo yanaweza kuhusishwa moja kwa moja na vyombo/vifaa vinavyozungumziwa. Maneno mengi hayachukui utaratibu huu. Katika Kiswahili kwa mfano, maneno kama meza, kiti, ua na mengine mengi hayana uhusiano na vifaa hivi.
Walijishughulisha na kueleza kategoria za sarufi kmf. nomino na vitenzi. Wanamapokeo walihakiki sentensi kwa kutambua vipashio vyake mbalimbali. Waliangalia jinsi vipengele hivi vilivyotumiwa – vizuri au kimakosa katika sentensi, pia walijaribu kuvieleza vijisehemu hivi na kuvitolea maana. Walipanga vipashio vya lugha katika makundi pia.
Walionelea kwamba lugha ya maandishi ilikuwa bora kuliko lugha ya mazungumzo. Kwa wanamapokeo, lugha ilikuwa ile iliyoandikwa. Maoni haya yalishikiliwa sana na Wagiriki. Maoni yao yanafungamana na neno la Kigiriki grammar yaani sarufi linalotokana na neno la Kigiriki grammatike linalotumiwa kwa maana ya 'kuandikwa'. Kutokana na neno hili basi wanamapokeo wakachukulia kwamba lugha yoyote ambayo haikuwa imeandikwa au kuandikiwa sarufi haikuwa lugha kamwe. Lugha ya Kilatini ndiyo iliyokuwa imeandikwa wakati huo. Sarufi za lugha zote za ulimwengu ziliegemezwa kwa lugha ya Kilatini ambayo ilikuwa lugha ya wasomi wakati huu na tena iliyoandikwa. Udhaifu wa mawazo haya ni kwamba lugha ya kuongea ndiyo kongwe zaidi kuliko lugha ya kuandikwa, kabla maandishi yavumbuliwe, watu walikuwa wakitumia lugha kwa kuwasiliana. Maandishi ni mbinu ya kuhifadhi lugha. Lugha si maandishi wala maandishi si lugha. Kuna lugha nyingi za ulimwengu ambazo hazijaandikwa kmf. Kidorobo na Kiogiek. Je hizi si lugha? Lugha ya kuongea ndiyo yenye msamiati kamili. Maandishi yanawakilisha lugha ya kuongea. Isitoshe sio rahisi kuandika maneno yote ya lugha au sentensi zake kwani mzungumzaji asilia wa lugha fulani ana uwezo wa kuzua maneno na sentensi kochokocho.
Lugha ya mazungumzo ndiyo yenye nguvu zaidi kwani inabadilika kutegemea historia. Lugha iliyoandikwa haibadiliki. Mazungumzo yanazidi kubadilika kila mara kutegemea wakati. Tazama Kiingereza cha wakati wa Shakespeare na cha sasa. Lugha ya mazungumzo ni hai/tamu. Kupitia kwa mazungumzo mtu anatoa hisi zake (kukasirika, furaha nk.). Isitoshe ishara hutumiwa katika mazungumzo. Kiimbo katika lugha nyingi kinajidhihirisha zaidi katika lugha ya mazungumzo. Mara nyingi maneno yanayotofautishwa na kiimbo hayaonyeshwi katika maandishi.
ZOEZI LA 3.1 ? 1.Toa historia fupi ya lugha yako ya kwanza. 2. Unaweza kueleza baadhi ya sheria za sarufi za lugha yako? 3. Eleza sifa bainifu za sarufi mapokeo 4. Je, nadharia hii inadhihirisha kasoro gani? Zijadili
3.5 Dhana za Sarufi Mapokeo Katika sehemu hii nitaeleza dhana mbalimbali zinazotumika katika nadharia ya sarufi mapokeo kama vile sentensi, kishazi, kirai na neno.
Neno Bloomfield (1933) katika Language anaeleza neno kama kipengele cha lugha ambacho ni kidogo na ni huru. Kipengele hiki huweza kutamkika peke yake. Katika sarufi mapokeo, neno hutazamwa kama kipengele cha kimsingi. Neno lilitumiwa na wanasarufi mapokeo lakini hawakutoa maelezo au ufafanuzi unaotosheleza. Tatizo hili lilitokana na matumizi yao ya lugha andishi peke yake. Waliegemeza maana ya ''neno'' na sarufi andishi.
Katika maandishi, neno linatambulikana kwa urahisi. Tunaweza kutambua maneno katika sentensi kwa kuangalia nafasi inayoyagawa na kuyatenganisha. Ikiwa kuna nafasi kati ya vipashio viwili, basi kila kipashio kinachukuliwa kuwa neno. Katika lugha ya mazungumzo, nafasi hizi zinafikiriwa kuwa zinasimamiwa na kituo au mtuo. Lakini ukweli ni kwamba hatutui baada ya kutamka kila neno. Labda baada ya kila sentensi, au kishazi au kifungu cha maneno. Tunaposikia lugha tusiyoielewa, hatuwezi kusema ni wapi maneno yanapoishia. Hili linatufafanulia wazi kuwa mazungumzo/au lugha ya kuongewa hujitokeza katika mkondo au mfululizo bila kutua kwokwote. Ijapokuwa wanasarufi mapokeo walitumia neno bila kutia maelezo yanayotosheleza, bado tunahisi kwamba dhana hii ipo. Tunaweza kuifafanua kupitia kwa mitazamo mitatu.
Mtazamo wa kwanza ni kufafanua neno kama kipashio cha kisemantiki au maana. Hiki ni kipashio cha kiisimu chenye maana moja. Hivyo basi, kila neno linasimamia maana moja. Tatizo kuu hapa linatokea kwa sababu ni vigumu kueleza maana moja ni gani. Hili hudhihirika zaidi tunapoangalia lugha ambazo si tenganishi yaani lugha za uambishaji na lugha za unyambuaji (uainishaji huu ni wa Wihelm von Humboldt, 1836 aliyetajwa katika John Lyons, 1968). Lugha za uambishaji kama vile lugha ya Kiswahili hutumia vipashio aghlabu vidogo vidogo na kuviongeza kwenye vipashio vingine ili kupanua/kuongeza maana. Lugha za unyambuaji kama vile Kilatini huongeza viungo
kwenye vipashio ili kuonyesha uhusiano wa kisarufi huku viungo hivyo vikiongeza maana ya kisarufi.
Ikiwa kipashio kina mofimu zaidi ya moja, inakuwa vigumu kushikilia kwamba kina maana moja kmf. mtoto. Asilimia kubwa ya maneno ya Kiswahili yanayoonyesha idadi pamoja na ngeli kmf. mtu au katika Kiingereza singer – sing + er. Kuna pia vipashio vyenye maana moja lakini vikiungana, maana nyingine tofauti inajitokeza kmf. kula rushwa; put up with. Ikiwa tunaeleza neno katika mkabala wa lugha tenganishi, basi mtazamo huu unafaa. Lakini ikiwa tutakumbana na vipashio vyenye maumbo tata, basi dhana ya maana moja inatatanisha.
Namna ya pili ya kufafanua neno ni kuliangalia kama kipashio cha kifonolojia au kifonetiki. Katika mtazamo huu, neno hutambuliwa kwa kutazama sifa za kisauti. Katika baadhi ya lugha, neno linaweza kuwa na ulinganifu wa vokali – yaani vokali zote zinahusiana/zinashirikiana kisifa. Sifa hizi ni kama vile kuviringa, ambapo vokali zote zina mviringo, kuwa juu, au chini na mbele au nyuma. Maneno ya lugha ya Kiswahili huwa na tabia hii kmf. piga – pigia; choma – chomoa; tia – tilia
Hata hivyo si lugha zote ambazo zinazodhihirisha ulinganifu huu wa kifonetiki katika maneno yake. Mkazo pia huweza kutumika ikiwa unapatikana katika mazingira maalum ya neno. Katika Kiswahili, mkazo hupatikana katika silabi ya pili kutoka mwisho. Hivyo tunaweza kutambua kipashio fulani kama neno tunapotia mkazo katika silabi hii. Katika neno mwana + hewa = mwanahewa (tutaweka mkazo katika silabi-ha).
(mkazo: utamkaji wa nguvu zaidi katika sehemu fulani ya neno)
Neno linaweza kufafanuliwa kwa kufuata mbinu mbalimbali za kiisimu. Mtazamo huu hulenga kwenye wazo kwamba neno linaweza kutengwa ili lijisimamie. Vile vile haliwezi kuchanganuliwa na ndani yake mkapatikana maneno mengine. Namna moja ya kufafanua neno katika mtazamo huu ni kulichukua kama kipashio chenye uwezo wa kufuatwa na mtuo. Kwa hivyo, hata kama katika matamshi mtuo haupatikani, bado (tunatarajiwa/tunajua kwamba uwezo huo upo. Kutogawanyika kwake kunamaanisha kwamba hatuwezi kuingiza viungo vyo vyote ndani yake. Namna hii inaweza kutumika tu pale ambapo umbo la neno halina utata. Maelezo haya yanaonyesha kwamba ni vigumu kufafanua dhana ya neno. Hata hivyo, tunaweza kulitambua katika uchambuzi.
Sentensi Wanasarufi mapokeo walifafanua sentensi kama tamko lenye fikra iliyokamilika. Dhana hii ya fikra iliyokamilika inatatiza kwa vile ni vigumu kuieleza. Je, neno halisimamii fikra? Je, fikra ni nini? Je, fikra iliyokamilika ni gani, na ni gani ambayo haijakamilika? Hata kama tutachukua sentensi kama fikra, bado itakuwa vigumu kueleza dhana ya sentensi changamano au sentensi ambatano. Namna mwafaka zaidi ya kufafanua sentensi ni kuangalia muundo wake. Kila sentensi imeundwa kwa vipashio maalum vilivyopangwa kwa mpangilio maalum. Ikiwa tunaweza kueleza muundo huu, basi tutakuwa tumeonyesha kipashio kinachoweza kuitika sentensi kmf. S N+Kt Juma amefika
S N+KV+Kt
Jua kali limemchoma S N+Kt+N
mbwa amemuuma mtoto
Kila kipashio katika sentensi kina nafasi yake ambayo kinachukua. Hakiwezi kuchukua nafasi ya kingine bila kutatiza maana. Tunapochukua muundo kama kigezo cha kufafanulia sentensi, basi sentensi inakuwa kipashio kikubwa zaidi ambacho kinaweza kuwa na muundo wa kisarufi. Uainishaji wa sentensi katika makundi matatu – yaani sentensi sahili, changamano na ambatano unajikita kwenye vipashio vilivyoiunda
Kirai Katika sentensi, mnapatikana maneno ambayo yana kazi moja. Maneno haya yanaweza kuchukuliwa kama kipashio kmf. mti mrefu/umeanguka. Vipashio vya aina hii huitwa virai ( Pia huitwa vifungu au vikundi) navyo hupatikana kama sehemu moja ya sentensi. Virai haviwezi kujisimamia. Kila sentensi ina virai viwili vikuu vinavyoiunda –Kirai Nomino (KN) na Kirai Tenzi (KT). Virai hivi huchukua nafasi maalum katika sentensi. Lazima kila kirai kiwe na neno kuu linaloongoza mengine kmf. KN lazima kiwe na nomino au kikundi cha maneno chenye nomino inayoyaongoza au kiwakilishi kinachosimamia nomino. KN huchukua miundo tofauti. Muundo wa KN Kiswahili KN N – mtoto ( amelala) KN N + KV – mtoto mchanga (amelala) KN N + KV1 + KV2 – mtoto mchanga mnyamavu (amelala) KN Kiw – Yeye (amelala) KNKV +N Yule mtoto (amelala) KNN1 +N2+ Kt (kishirikishi) + KV Juma na Ali ni wakora KNØ Lete mpira
Inadhihirika hapa kwamba KN kinaweza kuwakilishwa na neno moja ambalo lazima liwe ama nomino au kiwakilishi. Kila lugha ina muundo wa kirai ambao unaweza kuwa tofauti na miundo ya lugha nyingine kmf. KN cha Kiswahili huanzia kwa nomino, kisha kivumishi, kikafuata ihali KN cha Kiingereza huanzia kwa kibainishi (KB, yaani; the, a, an) kisha kivumishi halafu nomino
kmf. Kiswahili KN N + KV KT
mtu mrefu aliingia Kiingereza KN KB + KV + N + KT
A tall man arrived
Muundo wa KT cha Kiswahili ni tata. Kila KT huwa na mofimu tegemezi zinazopachikwa kwenye mzizi pamoja na maneno mengine kama vile vielezi.
kmf. Mzee alikula jana S KN + KT + KL
Mtoto alikula jana
(Tutaangalia kwa undani mambo haya tutakavyoendelea). Lakini kwa sasa tutazame kirai tenzi kwa kifupi. KT cha Kiswahili huchukua miundo tofauti pia.
KTKt+ KL Alianguka vibaya KTKt(kisaidizi)+ Kt (kikuu) Mtoto angali analala KTKt+ N+ KL1+ KL2 Alipiga mkewe vibaya sana KTKt + KKH (Juma) Alilala juu ya kitanda KTKt + KN (Juma) Alikimbilia Mkate
KTKt(kishirikishi) + KL (Juma) ni hodari
Kishazi Virai huungana na kuunda vipashio vikubwa zaidi vinavyoitwa vishazi. Hivi huwa na uzito wa sentensi. Sentensi sahihi ni kishazi kimoja (kina kiima na kiarifu kimoja).
kmf. Kamau alilala jana Kuna aina mbili za vishazi. Kishazi huru kinaweza kujisimamia kama sentensi ilhali kile tegemezi hakiwezi. Sentensi huainishwa kutegemea vishazi vilivyotumiwa kuiunda.
Kmf. Kamau alifariki jana ( hiki ni kishazi huru)
Kamau (ambaye ni mwalimu mkuu wa shule yetu) alifariki jana (kishazi tegemezi kimepigiliwa mstari)
ZOEZI LA 3.1
? Tofautisha vipashio mbali mbali vya Kisarufi kwa kuvitumia katika sentensi.
3.6 Aina za Maneno Wanasarufi mapokeo waliainisha maneno katika makundi manane. Haya ni: Nomino/jina/nauni Kitenzi/kitendo/kiarifu(a) Kiwakilishi/pronouni/kijina Kivumishi/sifa Kihusishi/preposisheni Kiunganishi Kielezi/kisifa Kihisishi/kiigizi/maneno ya mshangao
Je, maneno haya yapo katika lugha yako ya kwanza? Yatambue!
1. Nomino/Majina Nomino pia huitwa majina na ni neno linalotumiwa kusimamia kitu. Kitu hiki kinaweza kuwa mtu, mahali nk. Jina ni neno linalotaja kitu, hali au jambo lolote hata kama ni la kufikiriwa tu (Nkwera, 1978:8). Kutokana na sifa zao mbalimbali nomino zimegawanyika katika aina zifuatazo.
a. Majina ya pekee
Haya ni majina yanayotaja vitu maalum kama vile watu, miji nchi nk. kmf.. Maria, Nairobi, Tanzania, Jamatatu, Februari nk. Yote huanza kwa herufi kubwa.
b. Majina ya kawaida
Haya ni majina yanayotaja vitu au mambo yote ambayo si maalum au ya pekee kwa mfano: kiti, gazeti, samaki, jembe nk. Katika majina ya kawaida kuna ya wingi, jamii na dhahania
(i)Majina ya dhahania
Haya ni majina yanayotaja vitu vinavyoweza kufikirika au kudhaniwa tu, vitu visivyoweza kuonekana au kushikika kwa mfano: usingizi, upole, uzalendo.
(ii)Majina ya wingi
Haya hutaja vitu vinavyopatikana katika hali ya wingi tu. kmf.. maji, mafuta na mchanga.
(iii) Majina ya jamii
Haya hutaja vitu ambavyo asili yake ni mkusanyiko au jamii ya vitu vingine, kmf. timu, batalioni, baraza, kikosi na familia.
2. Vivumishi
Ni maneno yanayotoa sifa zaidi za jina – yanavumisha majina. Hutoa habari zaidi za mtu/kitu/mahali – alivyo au jinsi kilivyo, jinsi kinavyoonekana au jinsi kinavyofikiriwa kwamba kina tabia fulani au kipo katika idadi fulani/hali fulani.
Aina ya Vivumishi (i)Vivumishi vya sifa Maneno yanayotaja tabia, yaani namna watu walivyo au jinsi kitu kilivyo: mfano – dogo, -ema, -chafu, -geni, safi, stadi nk.
(ii)Vivumishi vya idadi Ni maneno yanayoonyesha idadi ya watu, vitu, au mambo kmf. moja, mbili, chache,-ingi nk.
(iii)Vivumishi vimilikishi Hujulisha mali ni ya nani kmf. –angu, -ake, -ao, -enu na -etu .
(iv)Vivumishi vionyeshi Maneno yanayoonyesha ujirani wa kitu au umbali wa kitu kwa uhusiano wa kingine kmf. huu, hiki, hizi, hili, mle, kule, zile pale nk.
(v)Vivumishi viulizi Kama vile: -Ipi, -ngapi na gani.
(vi)Vivumishi vya pekee Navyo ni: –enye, -enyewe, -ingine, -ote na o–ote
(vii)Vivumishi vya a –unganifu kmf. katika sentensi zifuatazo
jeshi la mgambo Jeshi la mzee mtu wa watu lugha ya wazee Viatu vya shule
3. Viwakilishi/ pronomino au pronauni Haya ni maneno yanayosimama badala ya majina. Viwakilishi ni vya namna tano:
(i)Viwakilishi Vionyeshi Huyu analala Ile naipenda Huku hakukaliki Humo hamkaliki/mnapendeza
(ii)Viwakilishi Viulizi Matumizi yake yanaonyeshwa katika sentensi zifuatazo. Yupi unayemtaka ? (kuku) Ngapi zimeshonwa ? (nguo) Wangapi wamebaki ? (kondoo)
(iii)Viwakilishi vimilikishi Hivi ni kama -angu,- etu, -ake na -ao . Kwake kuna mbwa (nyumbani kwake ...) Pako pachafu (mahali)
Yake imepotea (nguo)
(iv)Viwakilishi vibainishi Hivi vinatumika kwa njia hii katika sentensi ili kutoa maelezo zaidi. Kmf. Kazi ambayo haukuifanya jana utaifanya leo
(vi)Viwakilishi nafsi Vinatumika hivi katika sentensi. Nilisema (mimi) ulisema (wewe) Alisema (yeye)
Viwakilishi nafsi huru ni pamoja na mimi, wewe, yeye, sisi, wao, ninyi Viwakilishi nafsi viambata vimepigiliwa mstari; nilisema, ulisema, alisema
4. Vitenzi Ni neno linaloeleza kufanyika kwa jambo. Ni maneno yanayoonyesha kitendo kinachotendeka. Kuna aina mbalimbali.
(i)Vitenzi Vikuu Ambavyo hutaja matukio mbalimbali kmf. taarifa, hali ya kitendo na kauli/jinsi ya kitendo kmf. Maria anaandika barua, Musa anaruka, Joel anateta, Moi anatawala
(ii)Vitenzi Vishirikishi Hufanya kazi ya kushirikisha au kuleta uhusiano baina ya jina, kiwakilishi, kivumishi au kielezi na jina, kiwakilishi, kivumishi au kielezi kingine
kmf. Baba ni mwenyekiti wa kijiji, Mama ni hodari, Ali atakuwa baharia, Yeye ni mrembo, Yeye ni hatari, Tausi alikuwa mwalimu.
(iii)Vitenzi Visaidizi Hutumika sambamba na vitenzi vikuu katika sentensi ili kukamilisha maana. kmf. Juma angali analima Wanajeshi walikuwa wanapanda mlima
5.Vielezi Kielezi ni neno au maneno yanayoelezea kuhusu tendo linavyofanyika
(i)Vielezi vya mahali Hueleza zaidi matendo kuhusu mahali yanapofanyika Anapanda juu Ametokea kusini Ameingia ndani Ameenda Nairobi
(ii)Vielezi vya wakati Hufafanua wakati matendo yanapotokea Alifika jana Gari litawasili asubuhi Mtihani utaanza saa tatu
(iii)Vielezi vya idadi Hutujulisha tendo limetokea mara ngapi Nimekuja mara tatu Mponda hufika shuleni mara chache Hii ndiyo mara yake ya kwanza kupaona
(iv)Vielezi vya namna/jinsi Hueleza jinsi tendo linavyofanyika Anatembea polepole Walianguka chubwi Alilala fofofo Alivaa kizungu
6.Viunganishi Huunganisha neno kwa neno, neno kwa kikundi au sentensi kwa sentensi. Watoto wanacheza na wazee wanapumzika Mtoto hakulia wala hakufanya matata Viunganishi vingine ni lakini, au, ila, kwa sababu, hata, kama, ilhali, halafu, na kwa kuwa nk.
7.Vihisishi Ni maneno yanayodokezea hisia, mguso au vionja vya ndani vya mzungumzaji. Maneno haya hudhihirisha iwapo mzungumzaji ana kebehi, uchungu, furaha, shangwe, mshangao au utambuzi kmf. Ala, ebo, aka, masalaale, kumbe na lo.
8.Kihusishi Hili ni neno linaloonyesha uhusiano uliopo baina ya maneno, fungu la maneno au sentensi kmf. wa, ya, cha, kwa na za
Mifano ya sentensi: Nguo za Juma zimepotea Alisafiri kwa gari Aliwekelea kitabu juu ya meza
3.7 Udhaifu wa kutenga maneno katika aina nane Kama tutakavyoonyesha, ufafanuzi wa aina za maneno una upungufu mkubwa ambao unadhihirisha tatizo kubwa la nadharia ya sarufi mapokeo.
Kuna maneno ambayo yanapatikana katika makundi tofauti. Baadhi ya vivumishi hutumika kama vielezi au nomino. kmf. Vitabu vizuri (kivumishi)
Ametembea vizuri (kielezi) Uzuri ni utu.(nomino) Tazama pia;
Uzuri wake unababaisha (nomino) Mtu mzuri anababaisha (kivumishi) Mtu yule anacheze vizuri (kielezi)
Ni vigumu kuainisha mzizi kama –zuri katika mkabala huu kwa kuwa unapatikana kama nomino, kivumishi na kielezi. Ingekuwa rahisi kama maneno yangeainishwa kutegemea utendakazi wake katika sentensi.
Maelezo na maana ya aina hizi za maneno si dhahiri. Hayatokani na utafiti wowote, hayaeleweki, hayatenganishwi vilivyo na iwapo mtu hayajui hapo awali/kutoka mwanzoni hawezi kusema ni aina gani la neno linalozungumziwa. Wanamapokeo ueleza nomino/jina kama neno litumiwalo kutaja mtu, mahali au kitu nk. Kutokana na maelezo haya basi jina halipewi ufafanuzi wa kutosha.
Isitoshe maelezo yenyewe yalijitokeza kama kilinge. Wangeanza kutoka mahali fulani na kuishilia palepale! Kmf. nomino ni jina la kitu. Kitu ni nomino.
Kiwakilishi (pronauni) kilielezwa kama neno litumiwalo badala ya nomino. Maelezo haya hayaridhishi kwani neno lolote lile linaweza kutumika badala ya nomino.
Mbona pia tuwe na aina nane tu. Huenda lugha zingine zikawa na zaidi ya aina nane za maneno. Isitoshe kikundi cha vielezi kinaonekana kuwa kina maneno ambayo hayana uhusiano wowote kmf. haraka, sana nk. maneno haya hayana uhusiano. Tazama pia tofauti za vielezi 1. alikimbia sana (kielezi 1) 2. Alikimbia haraka sana (kielezi 2) 3. Mtoto mzuri sana (kivumishi)
Maneno kama sana, mno na kabisa yanaonekana kuwa na utendakazi maradufu licha ya kuwa vielezi
Kumbuka
Licha ya udhaifu huu wa kutenga maneno katika aina nane bado tunahitaji kategoria hizi ili kuweza kuandika sarufi na kuitumia. Hii ni kwa sababu sarufi huelezwa kwa njia ya kategoria na aina za maneno. Jambo muhimu basi ni kuweza kueleza kila kategoria ya neno kulingana na matumizi yake au utendakazi wake katika sentensi.
3.8 Umuhimu wa Nadharia ya Sarufi Mapokeo. Ijapokuwa kazi yao inadhihirisha kasoro nyingi wanamapokeo walichangia katika kuendeleza sarufi.
Isimu iliibuka kwa sababu ya/au kutokana na mwamko wa wayunani wa kuihakiki lugha. Mwamko huu ulifanya watafiti wengine kutoka sehemu zingine za ulimwengu kuishughulikia lugha. Utangulizi uliofanywa na wanamapokeo basi ulikuwa kitangulizi na kichocheo cha kuanzishwa kwa nadharia zingine za kutazama sarufi.
Walitoa dhana za kisarufi zinazotumika mpaka wa leo. Istilahi na dhana nyingi zinazotumika katika isimu leo kama vile nomino, vitenzi, sentensi na vishazi zilitokana na kazi ya wanasarufi mapokeo.
Istilahi zilizozuliwa na wanamapokeo zinaendelea kutumiwa na kupanuliwa huku zikipewa mtazamo mpya ili ziweze kutumika katika lugha nyingi iwezekanavyo.
Wayunani ndio waliokuwa watu wa kwanza kutumia kategoria za kisarufi zinazotumiwa leo kama jinsia, unyambulishaji, idadi, wakati na hali.
3.9 Dhana zaidi za Sarufi Usarufi Sentensi inaelezwa kuwa na usarufi endapo haijavunja sheria yoyote ya uundaji wake, yaani imefuata mpangilio wa maneno unaokubalika kuwa ni sahihi. Sentensi itakosa usarufi ikiwa maneno, vifungu/vikundi au hata vishazi ambavyo havikubaliwi kufuatana vimefanya hivyo. Hapa sentensi itakosa kukubalika katika kiwango cha sintaksia kmf. *Mzuri mtoto sana alimpiga Juma **Sana alimpiga mzuri mtoto Juma
Usarufi hasa unahusu kule kuundwa kwa njia nzuri kwa sentensi kisarufi na kisintaksia. Sentensi ya pili hapo juu imekosa usarufi kwa sababu kisintaksia muundo wake haulingani na sheria za lugha ya Kiswahili. Sentensi ya kwanza imeundwa kufuatia sheria za kisarufi za Kiswahili. Imefuata mpangilio wa maneno ambao ni sahihi katika sarufi ya Kiswahili.
Ukubalifu Sentensi zenye ukubalifu ni zile ambazo zina uwezekano wa kuzalishwa, zinaeleweka, hazina utata mwingi na zina uasilia. Ukubalifu ni dhana pana zaidi kuliko usarufi. Ikiwa sentensi inafasirika, basi inaweza kukubalika katika kiwango cha maana kmf. Msichana hii imekuja jana. Sentensi imekosa ukubaliano wa kisarufi lakini tunaweza kuifasiri sentensi hii kwanza kwa kuisahihisha. Mara nyingi tunaweza kuwasiliana kwa kiwango fulani bila kutumia sentensi zenye usarufi. Sentensi inaweza kuwa imeundika barabara kufuatia sheria za lugha lakini isikubalike katika kiwango cha maana:
kmf. Mtoto mzee alinyonya kwa funjo/Fisi analia/chai ni kavu Sentensi hizi zina usarufi lakini hazikubaliki kwa sababu zina utata mwingi, hazina uasilia na hazionyeshi uwezekano wa kuzalishwa na mzawa wa lugha. Ukubalifu unaenda sambamba na uwezo. Mzungumzaji asilia ana uwezo wa lugha yake ya kiasilia.
Wakati mwingine wazungumzaji hutoa sentensi za kisarufi ambazo kwa kiwango cha maana hazikubaliki
kmf. Mtoto mzee alinyonya kwa fujo. Mtoto hawezi kuwa mzee. Nyonya ni kitendo cha mtoto. Fujo inahusu kulewa hasa sio kunyonya Mfano maarufu wa Chomsky ni: Colourless green ideas sleep furiously ( ** Colourless cannot be green. Ideas cannot sleep). Sleeping is a passive experience and so it cannot be furious.
Ukubalifu unapatikana katika viwango vyote vya udhibiti wa lugha. kmf. katika kiwango cha fonolojia tutapata sentensi kama hizi.
Unasema gama nani? (Unasema kama nani?) Gutoga haba trive-in nitaenda mara mocha (Kutoka hapa Drive-In nitaenda mara moja)
Kumbuka
Washairi wanaweza kufasiri semi kama hizi na basi kuzikubali.
Kiswahili kina sheria za ukubalifu
1. N (-kawaida)(-Ashiria) Nomino ambayo si ya kawaida haifuatwi na viashiria au haiambatanishwi na viashiria Kmf. Hatusemi Nairobi hii ni chafu au Wamalwa huyu ni kiongozi mzuri
2. Kt (kishirikishi) (+KN/KV) Kitenzi kishirikishi hufuatwa na nomino au kivumishi Ali ni mwalimu Mtoto ni mfupi
3. Kt(Shamirishi) (+KN) Kitenzi shamirishi hufuatwa /huambatanishwa na nomino Alijenga nyumba Alinunua gari
4. Kt(sishamirishi)(-KN/KV) Kitenzi kisichoshamirishi hakifuatwi na nomino wala kivumishi. Maria anacheka vibaya Maria anasoma sana
Shamirishi=elekezi Sishamirishi=kisoelekezi
Kufikia hapo nimeeleza nadharia ya sarufi mapokeo, dhana zake, udhaifu na nguvu zake. Nimeeleza kwamba licha ya matatizo yanayojitokeza katika mkabala huu wa sarufi, bado ni muhimu katika kufasiri sarufi za lugha za ulimwengu.
Marejeleo ya Lazima Bornstein, P. D. 1984: An Introduction to Transfomational Grammar. Lanham: University Press of America.
Liles, B. I. 1971: An Introductory Transformational Grammar. Eaglewood Cliffs: Prentice Hall Inc.
Yule, G. 1985: The Study of Language. Cambridge: Cambridge University Press.
SOMO LA 4 Sarufi Miundo
4.0 Utangulizi Katika somo hili nitajadili mkondo wa pili wa nadharia ya sarufi ambao ni sarufi miundo. Sarufi miundo pia inaitwa sarufi fafanuzi au sarufi elezi. Mkondo huu aidha unajulikana kama sarufi muundo au sarufi maumbo. Katika somo hili nitaeleza misingi ya sarufi miundo, dhana na mambo muhimu yanayojitokeza katika nadharia hii pamoja na baadhi ya vitengo vya nadharia hii. 4.1Shabaha Baada ya somo hili ninatarajia kwamba wanafunzi wataweza: 1. Kueleza misingi ya nadharia ya sarufi miundo. 2. Kufafanua dhana mbali mbali za sarufi miundo 3. Kubainisha vitengo mahususi vya sarufi miundo 4. Kutathmini nadharia ya sarufi miundo kama mkondo wa sarufi.
4.2 Maana ya Muundo Sarufi mapokeo hutumia mtazamo wa uelekezaji kwa kuelezea matumizi ya lugha katika mkabala wa matumizi bora. Uchanganuzi wake wa lugha unajikita kwenye kanuni zinazopaswa kufuatwa ili usemi usiwe na makosa. Baada ya muda mrefu baadhi ya wanasarufi walianza kuhisi kwamba mtazamo huu una upungufu mkubwa. Walihisi kuwa kanuni zilizoainishwa na wanamapokeo hazikuwa na uwezo wowote wa kupimia matumizi ya lugha, yaani hazingeweza kutumika kama kigezo cha kuainishia matumizi bora na yasiyo bora. Henry Sweet, katika A new English Grammar (1891, Vol.I:5) anapinga kanuni za sarufi mapokeo kwa kusema; “Kanuni za kisarufi hazina thamani yoyote kwani zinaarifu kuhusu hali maalum. Matumizi yoyote ya lugha yana usarufi endapo yanatumika kwa ujumla na watu”
Sweet alidhamiria kuchambua lugha kwa mtazamo wa kisayansi. Sarufi ilichukuliwa kama sayansi kwa kufuata mbinu au njia za kisayansi za kuchunguza mambo. Sarufi miundo inachukuliwa kama chanzo cha uchambuzi wa kisayansi wa lugha. Lugha hapa inachukuliwa kama mfumo uliojengeka kwa mpangilio maalum. Mfumo huu una miundo inayodhihirisha ruwaza maalum zinazorudiwarudiwa. Uchambuzi wa lugha basi unajikita katika uelezaji wa ruwaza hizi.
Ili kuweza kuielewa nadharia ya sarufi miundo yafaa kwanza tufasiri dhana ya muundo kwa ujumla wake.
Kwa mujibu wa Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) muundo ni mpangilio wa vipashio mbalimbali katika lugha.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1982) inaeleza muundo kama umbo la kitu kutokana na jinsi kilivyoundwa au kutengenezwa. Aidha ni namna ya utengenezaji wa kitu.
4.3 Misingi ya Nadharia ya Sarufi Miundo
Sarufi hii imejikita katika misingi ifuatayo.
Hujaribu kueleza lugha na kuifafanua
Wanamiundo wanaeleza matumizi yote ya lugha yaani kueleza jinsi lugha ilivyo bila kujikita kwenye matumizi bora, safi au ufuataji wa sheria/kanuni zilizowekwa.
Wao walitegemea miundo au maumbo ya lugha yanayoonekana yaani maumbo ya nje yaliyo dhahiri. Haya ni maumbo tunayoyaona katika maandishi au tunayoyasikia katika mazungumzo.
Wanamiundo walishikilia kwamba maumbo ya lugha yanaweza kuelezeka kwa urahisi kwa vile yanaweza kufikika au kuonekana wakati wa uchanganuzi.
Kiini cha uchanganuzi wao ni muundo au umbo la lugha sio maana. Walipanga vipengele vya isimu kulingana na data sio maana.
Walieleza muundo kama mpangilio wa ruwaza zinazojirudiarudia ambazo zina nafasi zilizojazwa na vipengele vya kisarufi. Kmf.
N Kt KL Mtoto analia sana Kiatu kilipotea jana Vyumba vimesafishwa leo
Kwao, miundo ya vipashio ni kitu cha kidhahania ambacho huonyesha kazi ya kipashio iliyobuniwa ili kusaidia kutoa maelezo ya kile kiwezacho kusemwa au kuandikwa katika hadhi ya kipashio.
Kwao, lugha imejengwa kwa mofimu, mofimu ikiwa ndicho kipashio kidogo chenye maana katika neno.
Wanamiundo walichunguza jinsi vipashio vinavyojenga tungo kwa kutumia mtindo wa kugawa sentensi ili kuweza kuzichanganua.
Wanasarufi mapokeo walifafanua dhana zao katika mkabala wa maana – wanamiundo nao waliazima istilahi/dhana hizi za wanamapokeo na kuzieleza upya. Walizichukulia kama vipashio vya lugha vinavyotenda kazi kwa namna maalum. Kwa mujibu wa wanamiundo, basi utendakazi au uamilifu ukawa ndicho kigezo cha kwanza cha kueleza dhana na istilahi mbalimbali.
Wanamiundo walieleza maumbo ya vipashio hivi pamoja na uhusiano wake na vipashio vingine katika sentensi. Walishirikisha kigezo cha maana kwa kuangalia uhusiano wa vipashio na vingine kmf. Wanamapokeo walieleza nomino kama jina la mtu, mahali au kitu. Wanamuundo wanaangalia nomino kama neno linalofanya kazi fulani/au kwa namna fulani (yaani wanaangalia utendakazi wa vipengele) Wanaangalia nomino kwa uhusiano wa vipashio vingine – kama neno linalolazimisha au kutumiwa kuleta ukubaliano wa kisarufi katika maneno mengine ya sentensi.
Wanamiundo walithamini zaidi uhusiano wa vipashio au maneno katika sentensi zaidi ya maana ya vipashio vyenyewe.
Uhusiano wa vipashio ndio unaounda msingi wa uchanganuzi wa wanamiundo. Kwao maana ya sentensi inatokana na muundo wake.
Kwa ujumla mtindo wa wanamiundo wa kugawa sentensi kwa kuangalia vipashio vyake uliitwa mtindo au mbinu ya uchanganuzi wa viambajengo (immediate constituent analysis) or IC Analysis.
Zoezi 4 .1 ? 1.Linganisha misingi ya nadharia ya sarufi mapokeo na ya sarufi miundo.
2.Wanamiundo walikuwa na msukumo upi?.
4.4 Uchanganuzi Kiuambajengo Uchanganuzi kiuambajengo ni mojawapo ya vitengo vya nadharia ya sarufi miundo. Uchanganuzi kiuambajengo ulitumiwa mwanzo katika mofolojia. Katika mofolojia, mofimu hufuatana kwa namna au ruwaza maalum katika uundaji wa maneno. Ruwaza hii huitwa muundoambajengo. Neno lenye umbo tata linaweza kugawanywa katika viambajengo vifuasi yaani linaweza kugawanywa katika viambajengo viwili ambavyo vinaweza pia kugawanywa kila kimoja katika viambajengo viwili hadi kufikia mofimu au viambajengo ambavyo haviwezi kugawanywa tena. Hivi huitwa viambajengo tamati. kmf. neno kupigana lina viambajengo vifuasi ku+pigana, vya pigana ni pig+ ana, viambajengo tamati ni ku + pig + an + a Uchanganuzi kiuambajengo ulitumiwa katika sintaksia kama mbinu ya kugawanya maneno au makundi ya maneno.
Wazo kuu hapa ni kuwa katika sentensi yoyote, baadhi ya maneno yana uhusiano zaidi ya mengine. Sentensi huchukuliwa kama muundo ulioundika kwa viambajengo ambavyo vinaweza kugawanywa katika sehemu mbili hadi kufikia sehemu ambazo haziwezi kugawanyika tena. Kila sehemu inadhihirisha maneno au makundi ya maneno yaliyokaribiana au kuhusiana zaidi. Sehemu ambayo haiwezi kugawanywa tena huitwa kiambajengo tamati.
Msingi wa uchanganuzi kiuambajengo unajikita kwenye swala la ubadilishaji yaani kila kiambajengo kilichochanganuliwa kinaweza kubadilishwa na kingine katika nafasi au mazingira yale yale. Hivi tunaweza kuelewa ni vipi aina za maneno zimetawanyika katika sentensi. Swala la ubadilishaji ni la kimsingi katika sarufi miundo.
Uchanganuzi kiuambajengo ni mbinu ya uchanganuzi iliyodhihirisha uhusiano hasa wa kikundi nomino na kikundi tenzi pamoja na viambajengo vyao. Hivyo aina za maneno kutambulika kutegemea jinsi zilivyotawanyika na kuhusiana katika sentensi.
Uhusiano wa karibu Sentensi sio mfululizo wa maneno. Kwa mujibu wa wanamiundo sentensi inaelezwa kama viwango vya viambajengo. Hivyo basi ule uwezekano wa kuigawa hadi vipashio vya chini zaidi. Kwa mujibu wa wanamiundo, kwa wazungumzaji asilia wa lugha fulani, ni dhahiri kwamba maneno fulani ya lugha yana uhusiano wa karibu kuliko yalivyo na mengine katika sentensi – kwa mujibu wa wanamiundo basi, sentensi ingegawanywa kutegemea uhusiano huu wa karibu kmf.. paka waliwakamata panya.
Paka / waliwakamata panya (mgao wa kwanza) paka / waliwakamata // panya (mgao wa pili)
paka / wa /// li /// wa /// kamat /// a //panya (mgao wa tatu)
paka + wa li + kamata + panya N1 + wingi wakati + kitenzi + N2 Kwa mujibu wa wanamiundo dhana ya wingi (wa) katika mfano huu ina uhusiano wa karibu na nomino paka kuliko ilivyo nao na viambajengo vingine. Dhana ya wakati uhusiana mno zaidi na kitenzi. Katika sentensi za Kiswahili ni dhahiri kwamba wingi/uchache unahusiana na nomino ilhali nyakati/hali uhusiana na kitenzi.
Maneno mengine yanayohusiana na nomino ni kama vionyeshi [yule, huyu, wale]; au vivumishi kama vile [mzuri, kirefu, mnene ]. Vielezi [ kmf. polepole, haraka, hodari]
navyo vina uhusiano wa karibu na kitenzi. kmf. mtoto huyu anacheza vizuri sana. Sentensi hii itachanganuliwa hivi; mtoto huyu/ anacheza vizuri sana mtoto huyu/ anacheza// vizuri sana mtoto huyu/ anacheza// vizuri ///sana
m////toto huyu/ a////na////chez////a vi////zuri ///sana
Zoezi 4.2 ?1.Changanua sentensi hizi ukifuata mtindo wa wanakiuambajengo (a) kiatu chake kimepotea (b) mtoto alilia usiku kucha (c) simba mkali aliwavamia mbuzi wake (d) vioo vyote vimevunjika
Kwa ujumla upanuzi wa sentensi katika nadharia ya sarufi miundo ulifanywa bila kuzipa sehemu/vipengele tofauti majina na kuendelea kuzipanua na kuzipanga mradi zinaonyesha uwiano katika ruwaza yake. kmf.. Juma anaenda Juma anaenda sokoni Juma anaenda sokoni kununua matunda Juma anaenda sokoni kununua matunda aliyotumwa na shangazi yake ..... anayeitwa Asha ..... ambaye ni mgonjwa sana
Je, walijuaje watakatia wapi sentensi kwa kuangalia ruwaza kama hizi?.
Ruwaza za aina hii pia ziliwezekana. Juma anaenda/Mary anakula/Rose anasoma Jethro ni mpole/Auma ni mrefu/Mti ni mfupi
Ijapokuwa vipashio hivi havikupewa majina, hadhi ya vipashio ilionekana kuchukua orodha hii. Sentensi ambacho ndicho kipashio kikuu, kishazi, kirai, neno, mofimu na fonimu (sauti)
Njia nzuri ya kuonyesha mtindo huu ni kwa kutumia kielelezo cha aina ya mti. Matawi mbalimbali ya mti hudhihirisha migao mbalimbali.
Paka // mweusi a /// li /// m /// fuata // panya Kwa kutumia mtindo huu sentensi za aina nyingi [kmf. sentensi sahili, ambatano, changamano] zinaweza kugawanywa na kuchanganuliwa. Kmf. Panya mweusi ambaye alikuwa akiwasumbua kina Juma alifuatwa na paka mweupe
Paka mkubwa mweusi alimfuata panya mweupe
paka mkubwa mweusi a li m fuat a panya mweupe
Mchoro huu wa mti unaonyesha wazi hadhi ya vipashio. Vipashio vidogo zaidi huunda kwa kuunganishwa pamoja kuleta vipashio vikubwa zaidi kutoka chini hadi juu. Dhana ya upanuaji ndiyo hutumika zaidi. Vipashio husemekana kuwa vimepanuliwa kutoka vingine iwapo vipashio hivyo vinaweza kuchukua nafasi yake kmf. a, b ni upanuaji wa A iwapo a,b vinaweza kuchukua nafasi ya A. kmf.
a b paka mweusi alimfuata panya mweupe
A Mtindo wa upanuaji ni dhana kuu katika uchanganuzi wa wanamiundo. Pia, wazo la vipashio kuchukua nafasi ya vingine ni mahususi.
Kmf. paka mweusi alimfuata panya mweupe
Mbwa mkali................................. Kuku mwekundu........................... Mnyama mwingine.......................
Zoezi 4.3 ? Je, huchukuaji nafasi ni upi? Ueleze kwa kutoa mifano ya sentensi
Hapo juu tumegusia dhana ya upanuaji. Hebu tuieleze zaidi. Katika sentensi hii: Mti mrefu ulikiangukia kiti cheusi (A). Sentensi hii inaweza kupanuliwa ikawa Mti mrefu aina ya mchungwa ulikiangukia kiti cheusi cha mzee Juma (B) inaweza pia kufupishwa ikawa mti ulikiangukia kiti.
B ni upanuaji wa A Upanuaji hapa ni mbinu inayotumiwa kuonyesha huchukuaji nafasi wa viambajengo fulani na vingine. Pia upanuaji huleta maana ya kule kuongezea vipengele fulani kwa sentensi hivi kwamba tunaanza na neno moja hatimaye kuwa na maneno mengi. Tazama; Chungwa limeiva Chungwa lililoiva lilitundwa na Eva Jana chungwa lililoiva lilitundwa na Eva na Adam Inasemekana kwamba chungwa lililoiva lilitundwa na Eva na Adam shambani mwa Eden.
Njia nyingine ya kuwasilisha mgao wa viambajengo inaonyeshwa hapa chini:
Mtoto huyu anasoma polepole
(mkato 1) Mtoto huyu anasoma polepole
(2) mtoto huyu anasoma polepole
(3) m toto huyu a na som a polepole
Zoezi 4.4 ? Changanua sentensi zifuatazo kwa kutumia uchanganuzi kiuambajengo. (a) Mtoto wake amepona (b) Wezi walikamatwa jana (c) Rehema aliamka mapema sana
4.5 Faida za Uchanganuzi Kiuambajengo
Viambajengo huonyesha mpangilio wa kimstari au mfuatano wa maneno na vijengo vingine katika sentensi.
Mtindo huu huonyesha hadhi ya viambajengo hadi kufikia kile chenye hadhi ya chini kabisa.
Uambajengo kwa kiasi fulani huweza kupambana na shida ya utata wa kimuundo katika umbo la sentensi. kmf. Baba Juma amefika
Baba Juma / amefika Baba / Juma amefika
Ni njia ya kimsingi au njia ya kuendelea kuchanganua sentensi katika kujenga viwango vya vipashio. Mbinu hii ilipisha njia zingine zilizofana zaidi yake.
4.6 Udhaifu wa Uchanganuzi Kiuambajengo
Mtindo wa viambajengo mwanzo ulichukulia kwamba sentensi imeundwa na mfululizo wa maneno yaliyopangwa kwa mstari. Kwa hivyo mtindo huu hauwezi kugawa vizuri sentensi ambazo zina maneno ambayo hayajitokeza katika mfululizo (ruwaza ya mfuatano). kmf. (a) Unataka kuondoka je! hawangeeleza kipashio je.
(b) She made the whole story up
‘up’ inahusiana zaidi na ‘made’ (made + up)
Mtindo huu haungeeleza baadhi ya utata katika sentensi, jambo ambalo linawezekana iwapo viambajengo tofauti vitapewa majina. kmf. baba Juma amefika
S S
KN KT KN KT
N1 N2 nafsi wkt mzizi N1 N2 Kt
nafsi wkt mzizi kiishio
Baba Juma a me fika Baba juma a me fik a
Baba Juma amefika Baba Juma amefika
KN KT KN KT
Mtindo huu haukuonyesha jinsi ya kuunda na kuzalisha sentensi mpya na zaidi isipokuwa zile zinazopatikana katika data.
Kigezo cha kugawa hakikuonyeshwa vilivyo.
Hawakuonyesha majina ya viambajengo.
Uchanganuzi kiuambajengo ulishindwa kutumika kwa baadhi ya sentensi ambapo viambajengo vikuu havikudhihirika kwa urahisi. Kmf.
Je, mzazi wangu aliitwa na mwalimu mkuu? Mtoto hakulia wala hakuleta matata Mwalimu alipigwa na mzazi
Uchanganuzi kiuambajengo ulishindwa kudhihirisha mahusiano maalum kati ya sentensi kama vile sentensi msingi na sentensi zalishwa kmf. uhusiano wa kauli tendi na kauli tendwa katika sentensi kama vile
(a) Juma alipiga mtoto.
(b) mtoto alipigwa na Juma.
Uchanganuzi huu ulijikita kwenye semi maalum yaani semi zilizorekodiwa ambazo huitwa kongoo. Uchanganuzi kama huu unaofuata mtazamo elezi huishilia kuorodhesha data. Sarufi iliyokamilika sharti iweze kueleza sentensi au semi zilizotolewa na mzungumzaji pamoja na zile ambazo bado hazijatolewa yaani lazima ueleze umilisi/uwezo wa mzungumzaji asilia unaomwezesha kuzalisha sentensi zisizokuwa na kikomo au sentensi kochokocho. Lazima sarufi iweze kutilia maanani sentensi zilizorekodiwa na zile ambazo hazijarekodiwa. Sarufi miundo ambayo ni mfano mzuri wa sarufi elezi inashindwa kutekeleza jambo hili.
Zoezi 4.5 ? Tathmini mbinu ya uchanganuzi kiuambajengo kama njia ya kuchanganua lugha?
Marejeleo ya Lazima Bornstein, P. D. 1984: An Introduction to Transfomational Grammar. Lanham: University Press of America.
Liles, B. I. 1971: An Introductory Transformational Grammar. Eaglewood Cliffs: Prentice Hall Inc.
Yule, G. 1985: The Study of Language. Cambridge: Cambridge University Press.
SOMO LA 5
Sarufi Miundo Virai 5.0 Utangulizi Kufikia hapo tumepitia mikondo ya awali ya sarufi. Katika somo hili, tutabainisha kitengo kingine cha nadharia ya sarufi miundo kinachojulikana kama Sarufi Miundo Virai. 5.1 Shabaha Baada ya somo hili wanafunzi wataweza: 1. Kueleza misingi ya nadharia ya sarufi miundo virai. 2. Kufafanua dhana mbali mbali za sarufi miundo virai. 3. Kufafanua sentensi kwa kutumia vielelezo tungo. 5. Kuchanganua sentensi kwa kutumia kanuni miundo virai. 6. Kutathmini nadharia ya sarufi miundo virai kama mkondo wa sarufi.
5.2 Alama za Sarufi Miundo Virai Zifuatazo ni alama tutakazotumia katika kufafanua nadharia ya sarufi miundo virai. S Sentensi N Nomino Kt Kitenzi KL Kielezi KV Kivumishi KW Kiwakilishi KU Kiunganishi KH Kihusishi KI Kihisishi
KN Kirai Nomino KT Kirai Kitenzi KKH Kirai Kihusishi KKL Kirai Kielezi KKV Kirai Kivumishi
5.3 Misingi ya Kinadharia Uchanganuzi kiuambajengo hushughulikia sentensi ambazo tayari zimetamkwa au zimetolewa. Ala yenye nguvu zaidi ingekuwa ile inayotambua viambajengo kisarufi (umuhimu wa sarufi) pamoja na kudhihirisha sentensi zinazoweza kuundika katika lugha. Ala kama hii sharti iwe zalishi ili iweze kuzalisha sentensi zote za lugha zenye usarufi. Sarufi miundo virai ina sifa hii kwa kiasi. Sarufi miundo virai ni kitengo cha Sarufi Geuza umbo na hujihusisha tu na uambajengo.
Sarufi miundo virai hushabihiana na uchanganuzi kiuambajengo katika matumizi yake ya ubanaji na matumizi ya mikato/migao. Viambajengo katika sentensi hutambuliwa kwa kubanwa. Alama hutumiwa kusimamia viambajengo mbalimbali kmf.: KN; KT; KKH.
Kila mabano yaliyokamilika (bano la kufungua na kufunga) hudhihirisha kiambajengo kifuasi kmf. viambajengo vifuasi vya sentensi ifuatayo vinaweza kubanwa hivi
[[[mtoto] [mtukutu]] [[aliitwa] [[na] [[mwalimu] [mkuu]]]]]
Ubanaji/mkato katika sarufi miundo virai huwakilisha/husimamia muundo kirai wa sentensi ambao pia huweza kuwakilishwa katika mchoro matawi/kielelezo matawi.
S
KN KT
N KV Kt KKH
KH KN
N KV
Mtoto mtukutu aliitwa na mwalimu mkuu (mkufu tamati)
Mchoro matawi au ubanaji kama kielelezo cha muundo kirai wa sentensi huitwa kielelezo tungo. Hatima yake ni kudhihirisha viambajengo vifuasi vilivyoiunda sentensi.
Mahali matawi mawili yanapokutana huitwa kifundo. Isipokuwa vistari vya mwisho, kila kifundo kinawakilisha kiambajengo ambacho husimamiwa na alama kmf. KN, KT, N, K nk. na ambacho ni kipashio cha kisarufi. Ikiwa kifundo kinapatikana juu ya kingine, basi kinasemekana kuwa kinakiongoza au kinakimiliki. Uongozi huu unadhihirisha vile kiambajengo kikubwa kinaweza kuundwa kwa viambajengo vidogo vidogo. Mchoro matawi vilevile huonyesha ni kiambajengo kipi hutangulia kipi na ni kipi hufuata.
Kmf. KN cha kwanza hufuatwa na KT. Kt hufuatwa na KN cha pili nk.
Michoro matawi ya miundo virai hutupa maelezo kuhusu muundo wa sentensi lakini haituelezi ni vipi sentensi mpya zinaweza kuzalishwa. Hili hufanyika kupitia kwa kanuni miundo virai .
Zoezi la 5.1
?Fafanua dhana zifuatazo: (i) kifundo (ii) kielelezo tungo (iii) ubanaji
5.4 Kanuni Miundo Virai Kanuni miundo virai hutumiwa katika kuonyesha na kueleza viambajengo vya sentensi. Kanuni hizi zinaonyesha maana ya sentensi. Kanuni hizi ndizo huunda sarufi miundo virai. Kwa kutumia kanuni hizi, sarufi hii inaweza kuzalisha sentensi nyingi. Kupitia kwa kanuni hizi vijisehemu tofauti vya tungo vinaweza kupewa majina na pia kuelezwa kisarufi. Jambo hili halingewezekana kupitia uchanganuzi wa viambajengo. Kanuni miundo virai ni sheria za kuandika upya. Sheria hizi huandika upya sehemu zote za tungo hadi kufikia kiwango cha mofimu.
Jinsi ya kueleza kanuni hizi kmf. Mti mrefu uliangukia nyumba nzuri Sentensi hii inaweza kuzalishwa kwa kupitia kanuni sita. 1. S KN + KT 2. KN N + KV 3. KT Kt + KN 4. N m-ti, nyumba 5. KV m-refu, n-zuri 6. Kt u-li-anguk-i-a
Tunaweza kutumia kanuni hizi na kuunda sentensi nyingine kwa kutumia maneno yale yale lakini katika nafasi tofauti (ni muhimu tutilie maanani upatanisho wa kisarufi. Kmf: Nyumba nzuri iliangukia mti mrefu. Nyumba ndefu iliangukia mti mzuri. Mti mzuri uliangukia nyumba ndefu.
Sentensi zaidi zinaweza kuundwa kwa kubadilisha maneno yaliyotumiwa katika sentensi hii na mengine ya aina moja. kmf. kuku mtoto mbwa
mweusi mrefu mchoyo fukuza piga meza Kanuni hizi zinaweza kufasiriwa kwa namna mbalimbali. Kanuni ya KT Kt + KN haimaanishi kwamba ni lazima kila KT kiweze kupanuliwa hivi. KT kinaweza kupanuliwa na kuwa kitenzi pekee kmf. Mtoto amekuja. Kanuni mwafaka zaidi ingekuwa
KT Kt (-KN). Ikiwa hivi basi, kiambajengo cha KN katika KT si cha lazima. KT kinaweza kupanuliwa kwa namna nyingine pia kmf. KT Kt + KL Asha alikimbia haraka KT Kt + KV Kamau ni mzuri KT Kt + KKH Mtoto alipanda juu ya meza KT Kt + KN + KN Mwalimu alimpatia mtoto kitabu KT Kt (kisaidizi) + Kt (kikuu)
Mtoto angali analala Mtu alikuwa amepotea Walimu wamewahi kumtembelea Ng'ombe wamekwisha kukamuliwa KT Kt + N + KKL
Alipiga mkewe vibaya sana KT Kt + N + KU + KL
Alishona nguo kwa kasi KT Kiw + Kt
Amelala KT Kiw1 + Kiw2 + Kt + N + KL
Yeye (a)lifika Nairobi jana
Kanuni hizi hupanua kategoria za kisarufi katika kategoria nyingine za kisarufi kama vile S KN + KT; KT Kt + KN; KN N + KV kmf. kanuni 1-3. Hizi huitwa kanuni kategoria
Kanuni zingine 4 – 6 hupanua kategoria za kisarufi na kuzifanya maneno maalum kmf. Kt uliangukia; N mti, nyumba KV mrefu, nzuri nk. Ili kanuni hizi (4-6) ziweze kuzalisha sentensi zinazokubalika katika lugha ni lazima zionyeshe kwa mfano vitenzi vinavyoweza kupanuliwa na kuwa na Kt na KN na vile ambavyo haviwezi. Hii ndiyo sababu vitenzi hugawanywa katika makundi mawili kitenzielekezi/kitenzi shamirishi na kitenzi kisoelekezi/kitenzi sishamirishi. Tunahitaji kanuni za uchopekaji wa maneno/leksika ambazo zitatuonyesha kwamba kitenzi piga lazima kifuatwe na KN ilhali kitenzi lala si lazima kifuatwe. Uchopekaji wa maneno humaanisha hali ya kuweka maneno katika nafasi zilizochukuliwa na alama, yaani kupanua kategoria za kisarufi katika maneno.
Kanuni zinazotuonyesha neno ambalo likitumika lazima lifuatwe na kategoria ya kisarufi huitwa kanuni za kategoria tegemezi. Jambo muhimu la kutilia maanani kuhusu kanuni hizi ni kuwa zinaongoza maneno kwa kuonyesha ni yapi yanayoweza kufuatwa na kategoria zingine za kisarufi.
Kuna kanuni zingine zinazoongoza matumizi ya maneno ili yasitumike/yasiwekwe katika sentensi moja na mengine hivi tunajiuliza ni kitenzi kipi kinaweza kutumika na nomino ipi; ni nomino ipi inaweza kutumika na kivumishi kipi nk. kmf. kitenzi kunywa kinaweza kutumiwa pamoja na nomino ambayo haina sifa ya kimaana ya kunywa kmf. ugali? Bila kanuni hizi, mzungumzaji ataishilia kuunda sentensi zisizokubalika kimaana kwa
kutumia kanuni za kategoria za kisarufi pamoja na zile za kanuni za kategoria za sarufi tegemezi. Kanuni hizi ndizo hutuwezesha kuzalisha sentensi ambazo zinaweza kufasirika kimaana kmf. tazama: - Ouma anakula ugali - Ouma anakula maji - Ouma analala motoni
Colourless green ideas sleep furiously Kanuni zinazoongoza matumizi ya maneno ili kitenzi kmf.– kula kisifuatwe na maji kwa mfano huitwa kanuni teuzi. Kanuni hizi ni za kimaana na wala si za kisarufi. Zisipofuatwa, sentensi zenye usarufi zinaweza kuzalishwa lakini zikakosa maana. Kanuni hizi hujikita kwenye lugha maalum kmf. Kiingereza drink – (+N liquids) Kiswahili kunywa – (+N majimaji) Kikamba kunywa – (+N majimaji + sigara + bangi + moshi+ tobako Kanuni teuzi huwa maalum katika kila lugha.
5.5 Kanuni Miundo Virai na Unyambuaji Kwa kutumia kanuni miundo virai, tunaweza kunyambua sentensi. Unyambuaji ni tendo la kupachika vipashio kwenye kiini ili kujenga maneno. Hapa unyambuaji utachukuliwa kama mkufu wa alama zilizopangwa. Mkufu huu wa alama unajenga sentensi. kmf. 1. S KN + KT Juma amefika 2. KN N Juma 3. KT Kt amefika 4. Kt Kiw + wkt uliopo + mzizi (kit)
Kwa kutumia unyambuaji: 1. # S # 2. # KN + KT # 3. # N + Kt # 4. # N + Kiw. + wkt + mzizi wa kitenzi # 5. # N + Kiw. nafsi ya kwanza + wakati uliopo + mzizi wa kitenzi #
N Juma Kt amefika (# ni mipaka ya sentensi )
Unyambuaji hufuata utaratibu maalum. Alama hunyambuliwa moja baada ya nyingine mpaka (hadi) tunafikia wakati alama haziwezi kunyambuliwa tena. Unyambuaji unaweza kugeuzwa hadi kielelezo tungo
-1- S
-2- KN KT
-3- N Kt
-4- Kiw wkt mzizi kiishio
Uliopo
-5&6- Juma a me fik a
mf. 2 Mwalimu mkuu alifukuza watoto wote (unyambuaji) 1. S KN + KT 2. KT Kt + KN 3. KN N + KV 4. Kt Kiw + wkt + mzizi
Uliopita 5. N mwalimu, watoto 6. KV mkuu, wote 7. Kt alifukuza
mwalimu mkuu alifukuza watoto wote
S
KN KT
N KV Kt KN
N KV
M-walimu m-kuu a-li-fuk-uz-a wa-toto w-ote
Viatu vyangu vyote viliibiwa jana usiku
S
KN KT
N KKV Kt KKL
KV1 KV2 KL1 KL2 (wakati) (wakati)
Viatu vyangu vyote vilibiwa Jana usiku
Rhoda na Monica wangali wanaugua
S
KN KT
N KU N Kt (kikuu)
Kt Kisaidizi
Rhoda na Monica wangali wa na ugu a
Juma ni mzuri ( mkali, mnene, hodari)
S
KN KT
N Kt(kishirikishi) KV
Juma ni mkali (mwalimu, mnene, hodari)
S
KN KT
N KV Kt KN
Kiw wkt kiini kiishio
N KV
idadi
Mwalimu mkuu a li fukuz a watoto wote
Yeye angali mgonjwa
S
KN KT
N Kt KV
Kiw. Kionyeshi kisaidizi
Yeye angali mgonjwa
Juma ni mkali
S
KN KT
N Kt KV
(kishirikishi)
Juma ni mkali
Zoezi la 5.2 ?Fafanua sentensi zifuatazo huku ukitumia ama unyambuaji au vielezo tungo
1. Chakula kile ni kitamu 2. Cha mlevi huliwa na mgema 3. Tutakapofika kwake tutafurahia 4. Leo mvua nyingi imenyesha 5. Twawaombea Mola awape nguvu
5.6 Umuhimu wa Kanuni Miundo Virai
Kanuni miundo virai huongoza viambajengo katika sentensi na kutaja muundo wa viambajengo vinavyopatikana katika sentensi fulani. Pia hutaja vipashio vinavyounda sentensi kmf..
S KN + KT Hutaja kwamba vipashio vingine vya sentensi vimeundwa kwa maneno kadha wa kadha kmf.
KKH K + KL + Kl
Kwa haraka sana
Ilhali vipashio vingine vimeundwa kwa neno moja N mti
Kanuni miundo hujenga msingi wa sarufi miundo virai wa lugha na sarufi inayotumia kanuni hizi huitwa sarufi miundo virai.
Sheria/kanuni miundo virai zinaweza kuzalisha sentensi zote ambazo ni za kisarufi katika lugha husika.
Zinaonyesha mpangilio wa viambajengo katika sentensi. Huonyesha jinsi viambajengo vinavyoambatana kwa utaratibu. Kmf.. S KN + KT sio
S KT + KN hata katika sentensi Kama
(1) Alienda itakuwa S KN + KT na pia (2) Lete itakuwa S KN + KT
Sio S KT (pekee).
Sheria hizi zinaonyesha baadhi ya vipashio hadi kufikia kiambajengo cha chini kabisa.
S KN + KT KN N Juma KT Kt analima Kt Kw + wkt + mzizi + kiishio (A-na-lim-a)
Huonyesha majina ya vipashio na uhusiano wake.
5.7 Vielelezo Tungo
Jukumu la sarufi ni kutoa maelezo ya sentensi. Sarufi hueleza ishara S KN + KT na kuziambatanisha na sentensi halisi. Haya huwezekana kwa mujibu wa sheria za sarufi hiyo (ya lugha husika) S KN + KT inatuagiza tuandike sentensi kama kirai nomino (KN) na kirai kitenzi (KT). Haya kwa kutumia kielelezo tungo huonyeshwa kama:
S
KN KT
Asha amelala
Sheria za kielelezo tungo hufuatwa kutoka kushoto hadi kulia. KT huweza kupanuliwa pia kama
KT
K KN
N
Alimwaga Chai
Ni vizuri itambulikane ya kwamba mara nyingi pana uwezekano wa kuwa na KN mbili kmf.
S
KN1 KT
N Kt KN2
N
Mtoto a li tema mate
KN ambayo inamilikiwa na S moja kwa moja ndiyo kiima cha sentensi hiyo. KN2 inayomilikiwa na KT ndiyo yambwa ya sentensi hiyo.
5.7. Dhana Za Ziada
5.7.1 Dhana za Kielelezo Tungo (a) Kifundo
Katika kielelezo cha matawi, kifundo huwakilisha mahali ambapo viambajengo sisisi hutengana kmf.
- V - Vifundo
Jina la kategoria la kisarufi linalojitokeza katika kifundo huitwa jina la kifundo. Kuna vifundo ambavyo huwa na matawi na vile ambavyo havina matawi. Tukichukua mfano wa sheria hii X YZ tunaweza kuwa na mti huu:
X
Y Z
Katika mfano huu X humiliki Y na Z. Y na Z ni ‘watoto’ ‘mazao’ ya X ilhali Y na Z ni vifundo dada. Y na Z ni vifundo watoto wa X. Majina haya hutumiwa katika sarufi miundo virai ili kufafanua utaratibu wa kupanga vipashio katika muundo wa ndani wa sentensi.
Dhana ya njia hutumiwa kueleza mstari wa moja kwa moja kutoka kifundo kimoja hadi kingine kmf.
X YZ ni vifundo watoto wa X
YZ ni vifundo dada Y Z ZB ni njia
A B
Kutokana na mchoro huu, tunaweza kueleza kwamba X inamiliki Y na Z ilhali Z inamiliki A na B.
Kifundo kilicho juu zaidi ndicho kinachomiliki vifundo vya chini au vilivyo chini yake.
Kifundo ambacho hakimiliki vingine huitwa kifundo tamati kmf. B. Kile ambacho humiliki vingine sio kifundo tamati kwani kinaweza kupanuliwa kmf. Z. Kifungu cha sentensi ambacho hujitokeza chini ya vifundo mwisho, yaani mwisho wa kielelezo tungo huitwa mkufu tamati.
X
Y Z
A B
Alienda sokoni mkufu mwisho/tamati
5.7.2 Dhana za Sarufi Miundo (a) Kifundo tamati na kifundo ambacho si tamati Aina ya vifundo hivi hupatikana katika kielelezo tungo. Vifundo tamati ni aina ya vifundo ambavyo havimiliki vingine au haviongozi vingine. Vifundo ambavyo si tamati vinaweza kunyambuliwa kwa kutumia sheria za kuandika upya. Vifundo ambavyo si tamati humiliki vingine. Vifundo tamati hujenga mkufu tamati. Mfano wa vifungo tamati ni (Juma amefika) mkufu tamati N + Kt. Vifundo ambavyo si tamati mf. KN + KT
Tutaonyesha haya kwa njia ya unyambuaji: S KN + KT (Vifundo ambavyo si tamati) KN N Juma (kifundo tamati) KT Kt amefika (kifundo tamati)
(Kt Kw + wkt + mzizi + kiishio)
A- me- fik -a Juma amefika (mkufu tamati) Maelezo haya yanaweza kuonyeshwa katika kielelezo tungo.
-1- S
-2- KN KT
-3- N K
-4- Kiw wkt mzizi
-5- Juma a me fik a
1,2,3 vifundo ambavyo si tamati 4 kifundo tamati 5 mkufu tamati
(b) Jina amilifu Jina amilifu huonyesha kazi/jukumu la kiambajengo fulani katika kielelezo tungo kmf. kiambajengo kinachotekeleza kazi ya;
KN kama vile (mwalimu mkuu) KT kwa mfano (alifukuza wanafunzi wote)
(c) Jina kategoria