Jumatatu, 12 Februari 2018

SARUFI

Matumizi ya maneno na viambishi maalum
  1. Kwa
Hutumiwa ili kuleta au kuonyesha maana zifuatazo:
  • Mahali – ili kuonyesha mahali ni lazima kwa ifuatwe na jina la binadamu. Mf.
Tafadhali nionyeshe kwa Namwaya.
Hii ni njia ya kwenda kwa mwalimu mkuu.
Kesho nitaenda kwa nyanyangu.
  • Umilikaji wa mahali- hupachikwa kwenye mizizi ya viambishi vimilikishi nafsi (-angu, -ako, -enu, -ao) mifano
Ninaenda kwao.
Unacheza kwako.
Analima kwake.
Wanalima kwao.
  • Kivumishi cha A- Unganifu kuvumisha nomino za kitenzi jina. Mfano
Kucheza kwa Pele kunakumbukwa mpaka leo.
Kuimba kwa Mercy Masika kunavutia.
  • Kifananishi. Mfano.
Vitu hivyo vinafanana kama shilingi kwa ya pili.
  • Kilinganishi- hasa matokeo katika mashindano fulani.
Mfano:
Manchester United iliishinda Arsenal mabao nane kwa moja.
Kenya Pipeline iliishinda Kenya prisons seti tatu kwa mbili.
  • Pamoja na au jumuiko- kuonyesha mchanganyiko wa vitu au watu.
Watu warefu kwa wafuupi wataingia ukumbini.
Walikuweko vijana kwa wazee.
Alibeba vitabu vyote, vikubwa kwa vidogo.
Tulikula chapati kwa mandondo jana.
Nilienda katika hoteli hiyo nikaagiza ugali kwa sukuma.
  • Maswali (hutumika pamoja na viulizi kuwa swali).
Mfano:
Kwa nini ulichelewa kufika darasani?
Walichelewa kufika kwa sababu gani?
  • Muda / kipindi cha kitendo kutendeka.
Chakula kililiwa kwa saa nzima.
Amekuwa akiugua ukimwi kwa miaka tisa sasa.
  • Kuonyesha sehemu ya kitu kizima/ kutaja akisami.
3/8  -tatu kwa nane
Moja kwa sita huitwa sudusi.
Mwalimu alitupa tamrihi nikapata alama arobaini na tatu kwa hamsini.
  • Kitu kikitumika kama kifaa |chombo cha kutenda kitendo.
Nitasonga sima kwa mwiko.
Tulikula vibanzi kwa nyuma.
  • Sababu / kusudi / nia ya kutenda kitendo.
Mfano:
Timu yetu ilishindwa kwa kukosa maandalizi mazuri.
Vita vilizuka kwa ukabila.
Aliteswa kwa ujeuri wake.
Alinichapa rungu kwa nia ya kuniua.
  • Jinsi au namna kitendo kilivyotendwa.
Mfano:
Kijana mlafi alikula kwa ulafi.
Farai alikimbia kwa  mwendo wa kakaka.
Kwa nini unatembea kwa maringo?
  • Katika misemo au nahau na hasa kuunganisha maneno mawili sawa au yanayohusiana katika usemi Fulani.
Mfano:
Kushirikiana bega kwa bega- kushirikiana pamoja au kwa karibu.
Kuandamana moja kwa moja – kufululiza bila kusimama.
Kuonana ana kwa ana – kuonana uso kwa uso.
  • Kiunganishi hasa kikichukuana na hivyo kuleta maana ya sababu au matokeo.
Nilichelewa kufika shuleni kwa hivyo mwalimu aliniadhibu.
  1. Na
Hutumiwa kuleta dhana zifuatazo:
  • Vifupisho vya nafsi.
Mfano:
Na + mimi   =  nami Na + sisi = nasi
Na + wewe =nawe Na + nyinyi = nanyi
Na + yeye   =  naye Na + wao = nao
  • Vifupisho vya viashiria vya ngeli kwa kuvirejelea.
Na + hicho > nacho
Na + hizo   > nazo
Na + hayo > nayo
  • Hali ya umilikaji wa kitu au vitu.
Hutokea pale ambapo kiwakilishi ngeli/nafsi huchukua –na tamati.
Mfano
Mimi nina kitu. Sisi tuna vitu.
Kiatu kina doa. Viatu vina vitu.
Pale pana uchafu. Pale pana uchafu.
  • Kama kiunganishi.
Mfano.
Nilinunua kitabu, kalamu na sukari.
Huyu na Yule ni wanangu.
Kuchezacheza na kuibaiba vitu vya wenzako darasani ni tabia mbaya.
  • Wakati uliopo.
Mfano.
Ninaandika.
Tunaosha.
Wanatembea.
  • Hali / kauli ya kutendana / kutendeana.
Njeri na Nekesa wanafaana kwa raha na dhiki.
Watoto wale wanarukana.
  • Kama kiambishi kiwakilishi cha nafsi ya kwanza umoja.
Mfano.
Naenda darasani.
Namtembelea leo jioni.
  • Mtendi / mtendaji wa jambo Fulani(kihusishi).
Hua alilengwa kwa panda na mtoto mkorofi.
Aliadhibiwa na mamaye.
  1. Jinsi/Namna.
Ni nomino ambayo huleta dhana zifuatazo:
  • Njia ya kutekeleza jambo.
Alimweleza kwa kina jinsi ya kuandika kukmbukumbu.
  • Kuonyesha mwenendo.
Hatukupendezwa na jinsi walivyotukaripia.
  • Kuonyesha aina au sampuli.
Mimea ya jinsi hii ndiyo huleta mvua.
Kitambaa chajinsi hii ni chema.
  1. Ila.
Huweza kutumika kama nomino na pia kiunganishi.
  • Kama kiunganishi huwa na maana ya lakini/isipokuwa mf.
Walipanda wakapalilia ila hawakupata mavuno mazuri.
Amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga.
Sina cha kutegemea ila mshahara wangu mdogo.
  • Kama nomino huleta dhana ya kasoro, dosari, upungufu, fedheha au aibu.
Mbwa ni mnyama mzuri wa kufugwa mwenye tijara ; ila yake ni kula matapishi yake.
Inawezekana kupata kitu kisicho na ila.

  1. Ikiwa.
  • Kiunganishi hiki hutumiwa kuonyesha hali ya kudhania au kutokuwa na uhakika.
Tutamkuta kwake ikiwa hakuenda kazi leo.
Ikiwa nitamwona, nitampa kitabu hicho.
  • Kuonyesha masharti.
Atapona ikiwa atakunywa dawa.
Watapita mtihani ikiwa watasoma.
  1. Japo/Ijapokuwa/Ingawa/Ingawaje.
Hutumika kama kiunganishi na huleta maana ya: hata kama/ walau mf.
Japo hadhira ilimzomea, aliendelea kuhutubu.
Yeye ni mwerevu katika somo la Kiswahili ijapokuwa ni mtundu.
Japo wanafunzi wengi hupita mtihani wa kidato cha nne,hawapati nafasi katika vyuo vikuu.
Waziri huyo hutekeleza kazi yake vizuri ingawa  ni mzee.
  1. Wala.
Hiki ni kiunganishi.
Hutumiwa kuunganisha mambo mawili au zaidi katika hali ya kukanusha.
Mfano.
Sikula wala kunywa chochote siku nzima.
Hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
Vivu halimi wala hapalilii.
  1. Walakini.
  • Ni nomino inayoonyesha kitu kina dosari/kasoro.
Kama nyama hii haina walakini mbona umeificha guniani?
Mtu Yule anacheka pekee yake huenda ana walakini.
  • Hutumiwa pia kuleta maana ya `lakini`, `ila`
Pendo alitamani sana kupata mtoto walakini alipopata pacha hakuamini.
Jambo hilo lilikuwa gumu walakini baada ya muda mrefu wa kujaribu tulifanikiwa.
  1. Labda/pengine/huenda ikawa.
Hutumika kuonyesha uwezekano wa jambo kutendeka/ shaka.
Labda mkikimbia mwalimu atawasaidia.
Hebu hakikisha, labda hatukufunga mlango.
Hapendi kutembea na waseja siku hizi labda ameolewa.






Matumizi ya viambishi:
  1. “-ni-”
  • Kuonyesha viishio vya viulizi.
Nani. Gani.
Lini. Nini.
  • Kuonyesha ufupisho wa nafsi.
Ni nyinyi - ninyi
  • Kielezi cha mahali(ndani).
Nyoka yumo shimoni.
  • Kitenzi kishirikishi kipungufu.
Mimi ni mwanafunzi.
  • Nafsi ya kwanza umoja.
Nilienda.
  • Kuamrisha/wingi/.
Simameni!
  1. “-ku-”
  • Kuonyesha mahali.
Kule ndiko anakoishi.
  • Kiambishi awali cha nomino ya kitenzi jina.
Kuimba.
Kuongea.
  • Kuonyesha wakati uliopita katika ukanusho.
Hakusoma.
Hakuimba.
  • Nafsi ya pili umoja.
Nitakulipa.
Alikuchapa.
  • Kiwakilishi cha ngeli hasa KU-KU
Kulinipendeza.
  1. “-ki-”
  • Masharti(kutendeka kwa jambo fulani kunategemea kutendeka kwa jingine).
Ukiuliza swali la kijinga, hutajibiwa.
Ukisoma kwa bidii, utapita mtihani.
  • Kuonyesha udogo wa maneno.
Mtoto – kitoto
  • Kiwakilishi cha ngeli KI-VI.
Kimevunjika.
Alikichukua.
  • Kuonyesha jinsi kitendo fulani kilivyofanyika(kielezi namna)
Alipigwa kinyama.
Alilala kichalichali.
  • Kitenzi kishirikishi kipungufu.
Kitabu ki mezani.
Kiatu ki sebuleni.
  • Kuonyesha kuwa kitendo Fulani kilikuwa kikiendelea wakati kitendo kingine kilipotendeka.
Nilikuwa nikiimba alipoingia nyumbani.
  • Kuonyesha kuwa tendo Fulani litakuwa likindelea wakati lingine litakapotendeka.
Ajapo nitakuwa nikisoma maktabani.
  • Kuwakilisha majina ya lugha.
Kifaransa.
Kiingereza.
Kiswahili.
  • Kuonyesha kuwa kitendo kimekuwa kikiendelea kwa muda.
Wanafunzi wamekuwa wakicheza.
  1. “-ka-”
  • Kuonyesha mfuatano wa vitendo. Mf.
Juma alifika, akatusalimia, akaeleza alichotaka,akafunga vitu vyake na akaondoka.
  • Kuamrisha.mf.
Kachezeni!
  • Kuonyesha kuwa kitendo fulani ni tokeo la kitendo kilichotangulia.
Alisoma kwa bidii akafuzu mtihani.
  1. “-a-”
  • Huweza kuonyesha hali isiyodhihirikaya wakati uliopobila kuonyesha wazi mwanzoau mwisho wa kitendo.
Mpishi apika.
Musa acheza mpira.
  1. “-po-”
Huwakilisha:
  1. Mahali.
Aliposimama ndipo palipozikwa hazina.
  1. wakati.
  • Kitokeapo kabla ya mzizi, huashiria wakati dhahiri.
Alipofika tulimlaki.
  • Kitokeapo baada ya mzizi, huonyesha wakati usio dhahiri.
Afikapo tutamlaki.
  1. Kama kiambishi cha kukanusha hali ya `ki` ya masharti.
Ukisoma kwa bidii utapita mtihani- usiposoma kwa bidii hutapita mtihani.
Ukija utanipata -          Usipokuja hutanipata.
  1. “-ji-”
  • Huwakilisha nafsi rejeshi.
Aliyejipeleka.
Anayejipenda.
  • Kiambishi cha nomino hali ya ukubwa.
Mtu – jitu
Mzee - jizee
  • Kiambishi cha unominishaji/kuonyesha uzoefu wa kufanya kitu Fulani..
Winda – mwindaji
Cheza -  mchezaji
  1. “ndi-”
  • Huwakilisha dhana ya kusisitiza.
Mimi ndimi niliyemuua simba.
  1. “-ja-”
  • Huwakilisha hali timilifu katika ukanusho.
Amesoma – hajasoma.
Amefuzu – hajafuzu.


SHAMIRISHO (SH)/YAMBWA.
Hutumiwa kuelezea nomino ambayo huchukua nafasi ya anayepokea kitendo Fulani(kipozi), anayetendewa(kitondo) na kinachotumiwa kutenda jambo Fulani(ala).
Yambwa tendwa hupokea kitendo kwa njia ya moja kwa moja(shamirisho kipozi)
Yambwa tendewa, japo huathiriwa na kitendo, haipokei kitendo hicho moja kwa moja.
Kuna aina tatu kuu za shamirisho:
  1. Shamirisho kipozi.
  2. Shamirisho kitondo.
  3. Shamirisho ala/kitumizi.
Shamirisho kipozi(yambwa tendwa).
Hutumiwa kueleza nomino inayopokea kitendo chenyewe(tendo linalofanywa linahusiana moja kwa moja na nomino hii). Mfano
  • Juma amenunua kitabu.
  • Wanyonyi amechinja kuku.
  • Mwalimu alimfunza Katana.
Shamirisho kitondo/yambwa tendewa.
Hutumiwa kuelezea kitu au mtu ambaye anafanyiwa jambo.
Ikiwa mtu anafanya jambo Fulani kwa nia ya kumfaidi mtu mwingine, huyo mwingine ambaye anafaidika atakuwa shamirisho kitondo(hapokei tendo lililopo moja kwa moja). Mfano
  • Manene alimfundishia Mwanaisha.
  • Aldina alimjengea mamake nyumba.
  • Susan alimpa mwanafunzi kitabu.
  • Rozina amempikia Tatu chakula.
Shamirisho ala/kitumizi.
Ni shamirisho inayotaja chombo kilichotumiwa kutenda kitendo Fulani. Mfano
Arunga alimkatia gauni Immaculate kwa makasi
Chagizo (CH).
Ni neno au fungu la maneno yanayochukuwa nafasi ya kielezi au yanayofanya kazi ya kielezi katika sentensi.
Ni sawa na kielezi japo tu kielezi ni aina ya maneno na chagizo ni sehemu ya sentensi kutegemea uamilifu.
Mfano.
  • Ali alicheza vizuri sana.
  • Dereva alifika Mombasa asubuhi na mapema.
  • Sumbi anatembea vibaya uwanjani.
  • Waziri alimpa mwanafunzi zawadi shuleni.
Kijalizo.
Ni sehemu inyoongezwa katika kiarifu kama yambwa lakini, tofauti na yambwa kijalizo hutumika wakati hatuma kitenzi elekezi.
Hutumika tunapokuwa na vitenzi vishirikishi.
Mfano.

  • Musa ni mkulima.
  • Kayamba Afrika ni wetu.
  • Amina ni mfupi.
  • Kumb: kijalizo huweza kuwa kivumishi au nomino.

Maoni 7 :