Jumatano, 20 Februari 2019

ISIMU


MAANA NA MALENGO YA ISIMU

Utangulizi

Somo hili linatoa utangulizi wa chombo hiki cha binadamu kinachoitwa lugha.  Kwa muda mrefu binadamu amejaribu kuielewa lugha bila mafanikio makubwa hadi mikabala ya kisayansi ilipoanza kutumika.  Mikabala hii imeweka wazi misingi thabiti ya kuichunguzia lugha.  Misingi hii inadhihirika kupitia somo la isimu.  Haya mambo ya kimsingi ndiyo yatakayoshughulikiwa katika somo hili.

Malengo:

Baada ya somo hili utaweza:
·         Kueleza mambo anayoyafahamu mjua lugha ye yote.
·         Kueleza maana ya isimu.
·         Kutaja malengo ya isimu.

Lugha na Ubinadamu

Kila wakati binadamu wanapokutana kwa shughuli mbalimbali, mazungumzo hutokea.  Tunazungumza na marafiki zetu, majirani, wenzi, wageni ana kwa ana na hata wakati mwingine kupitia simu, na tunasikiliza redio na televisheni.  Wakati mwingine tunajizungumzia wenyewe (uzungumzi nafsia). Hata tunapolala tunazungumza katika ndoto zetu.  Licha ya kuzungumza huwa tunasoma na kuandikiana nyaraka.  Basi unaona kwamba lugha hutawala maisha ya binadamu.

   Swali:

       Je, umewahi kushinda siku moja au mbili bila kuzungumza na mtu
yeyote?  Ulihisije?

Kipaji cha kutumia lugha ndiyo sifa kubwa inayomtambulisha binadamu na wanyama.  Ili tujielewe vyema lazima tuielewe hiyo lugha inayotupa ubinadamu.  Jinsi ndege walivyo na mabawa, samaki walivyo na mapezi, ndivyo binadamu alivyo na lugha.  Mabawa humwezesha ndege kupaa angani.  Mapezi humwezesha samaki kuogelea majini.  Nayo lugha humwezesha binadamu kuwasiliana na hukuza uwezo wake wa kufikiri hata akayaelewa mambo ya kidhahania.

Kwa mujibu wa falsafa inayojitokeza katika visasili na dini za watu wengi, lugha ndiyo asili ya maisha na nguvu za mtu.  Hii ndiyo sababu, katika bara la Afrika, mtoto anapozaliwa huitwa ‘kuntu’ (kitu).  Inabidi ajifunze mambo fulani ya kibinadamu kabla ya kuitwa ‘muntu’ (mtu).  Tunapata ubinadamu wetu baada ya kujifunza lugha fulani.  Kwa watu wengi, lugha imekuwa ni fumbo lisiloeleweka kama vile asili ya jua, kuumbwa kwa dunia au asili ya moto.  Hii ndiyo sababu visasili vingi vimejitokeza katika juhudi za kutanzua fumbo hili.

Swali:


     Katika aya mbili za hapo juu lugha imelinganishwa na vitu
     gani?  Kwa nini?

Wataalamu wa lugha wanakubaliana kuwa mtoto ye yote wa binadamu akifikisha miaka mitano hivi, kama hana dosari zo zote katika ubongo wake, na amekulia katika jamii ya watu wanaozungumza lugha fulani, atakuwa amefikia kiwango cha kutosha cha kujua lugha hiyo.  Si lazima lugha hiyo iwe sawa na ile wanayoifahamu wazazi wake.
Kumbuka:
  Kila mwanadamu ana uwezo wa kujua lugha.  Mtoto hujifunza
  lugha inayozungumzwa katika mazingira anamoishi.

Kama anavyosema Besha (1994:2) lugha inachukuliwa kama tabia ya kawaida kabisa ya mwanadamu, na kwa sababu ya ukawaida huo, si mara nyingi wanadamu watakaa na kujiuliza kitu hiki ‘lugha’ kikoje.  Hii ni kwa sababu, kwa desturi, wanadamu hawadadisi sana kuhusu mambo ya kawaida.  Kwa mfano, watu wote hupumua lakini ni wangapi wanaojua lolote kuhusu jinsi mapafu yao yanavyofanya kazi.  Watu huona kwa kutumia macho, lakini ni wangapi wanafahamu jinsi macho yao yalivyoundwa?  Aidha, watu hula chakula kwa kukiweka mdomoni, kukitafuna na kukimeza; lakini wengi hawajui kinachotokea tangu chakula kinapoingia kinywani hadi kinapogeuzwa kuwa lishe muhimu ya miili yao.  Wataalamu tu ndio huchunguza mambo haya na kuyatafutia majibu.  Utaalamu wao hutuwezesha kuelewa mambo haya.

Kozi hii inalo jukumu la kuangalia kwa udani chombo hiki cha binadamu ‘lugha’ na kukichambua kisayansi ili ifahamike jinsi kilivyo na kinavyofanya kazi.

Ujuzi wa Lugha

Tumeona kwamba kila binadamu asiye na dosari atafahamu lugha fulani.  Hata hivyo ule uwezo wa kuwasiliana kwa kutumia lugha huhitaji kwamba mzungumzaji awe na ujuzi wa kina katika lugha hiyo.

Swali:

  Unaposema kuwa unajua lugha (Kiingereza, Kifaransa,
  Kiswahili, Kikikuyu, Kiarabu n.k.) huwa hasa unajua nini?  
  Ni ujuzi gani alionao mtu anayeijua lugha fulani?

Kuijua lugha fulani kuna maana kwamba unaweza kuzungumza na ukaeleweka na wenzako wanaoifahamu lugha unayoitumia; vile vile waweza kuelewa au kufasiri sauti zinazotolewa na wenzako katika lugha husika.  Ufuatao ndio ujuzi alio nao mtu anayeijua lugha fulani:

1.  Ujuzi wa Mfumo wa Sauti
Kuijua lugha ni kufahamu sauti zinazopatikana katika lugha hiyo na zile zisizopatikana humo.  Kwa mfano, Wafaransa hutamka maneno ya Kiingereza ‘this’ na ‘that’ kama ‘zis’ na ‘zat’ kwa sababu hawana sauti [ð], yaani dh.  Vivyo hivyo, Wakikuyu hutamka ‘Githurai’ na ‘Thika’ kama [giðurai] na [ðika] yaani Gidhurai na Dhika kwa sababu hawana sauti [θ] yaani th katika orodha yao ya sauti.

Zoezi:

   Orodhesha sauti zinazopatikana katika lugha yako ya kwanza.

Kuijua lugha pia humaanisha kujua zile sauti zinazowekwa mwanzoni mwa maneno, mwishoni au kujua mfuatano wa sauti unaokubalika katika lugha hiyo.  Kwa mfano, katika lugha ya Kiingereza hakuna maneno yanayoanza kwa sauti [ŋ] yaani ng’.  Aidha, unafahamu kwamba katika Kiswahili mfuatano wa sauti kama ‘baba’ unakubalika, lakini si ‘abba’, ‘bbaa’, ‘aabb’ au ‘baab’.

Utagundua kwamba hata binadamu anapotoa vilio vya vihisishi huwa anajifunga katika lugha anazozungumza.  Katika Kiingereza tutapata eh, um, uh na katika Kiswahili: Aaa! Oooo!  Lo!

2.  Ujuzi wa Maana za Maneno
Umeona kuwa kujua sauti na ruwaza ya sauti hizo katika lugha ni sehemu moja tu ya ujuzi wa kiisimu alio nao binadamu.  Pia, kuijua lugha ni kufahamu kwamba mfuatano fulani wa sauti huashiria dhana au maana fulani.  Hivyo basi kujua lugha ni kujua namna ya kuhusisha sauti na maana.  Kwa mfano, wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili watafahamu kwamba neno ‘mvulana’ lina maana iliyo tofauti na neno ‘msichana’.

Ikiwa hujui lugha, ule mfuatano wa maneno hauna maana kwako.  Hii ni kutokana na sababu kuwa ule uhusiano uliopo baina ya sauti na maana ni wa kinasibu.  Unapojifunza lugha itakubidi ujue kwamba mfuatano wa sauti ‘nyumba’ huashiria dhana ya                 ; ikiwa unafahamu Kiingereza dhana hii huwakilishwa na mfuatano wa sauti ‘house’, Kifaransa – ‘maison’, Kirusi – ‘dom’, na Kikuria – ‘inyumba’.

Hii inamaanisha kwamba sauti za maneno hupewa maana na lugha ambamo sauti hizo zinapatikana.  Hata hivyo, kuna maneno machache ambayo yanaiga sauti ya kile yanachowakilisha.  Haya ni maneno ya kionomatopea au ya tanakali sauti.  Sauti za maneno huiga sauti za maumbile au viumbe husika.  Kwa mfano: pikipiki, nyau, kengele, filimbi, tingatinga.
Zoezi:
  Andika maneno mengine matano ya kionomatopea katika
  lugha ya Kiswahili

3.  Usarufi wa Tungo
Ukiwa na ufasaha wa lugha fulani unaweza kutambua mara moja ikiwa kanuni fulani za lugha zimevunjwa na zimevunjwa kwa namna gani.  Lazima mzungumzaji wa lugha awe na uwezo wa kutambua usarufi na utosarufi wa tungo.

Kumbuka:

    Usarufi ni sifa ya tungo kutii kanuni za kisarufi za lugha husika;
    na utosarufi ni ukiukaji wa kanuni za lugha.

Kwa mfano, mzungumzaji wa lugha ya Kiswahili atatambua kuwa sentensi hizi zimevunja kanuni fulani:
    *  Ile mtoto imechana kitabu yake.
    *  Juma Maria alimbusu.
    *  Asha na Mwangi mekimbia.
Wakati huo huo, mtu anayejua lugha ya Kiswahili atakubali usarufi wa tungo ifuatayo, hata kama maneno ya tungo hiyo ni mageni kwake:
    Vile vikokoka vimekoa kokakao.
Mjua Kiswahili anaweza kufikiri kuwa maneno yaliyomo ni ya kisayansi au ni msamiati maalum, au kama amesikia tungo hiyo kutoka kwa watoto wadogo, anaweza kufikiri kuwa ni mchezo wa kitoto.  Lakini hawezi kuwa na mashaka juu ya usahihi wa muundo wa tungo hiyo kwa vile anaweza kuihusisha kwa urahisi na tungo nyingine za Kiswahili kama hii ifuatayo:
Vile vijiko vimeanguka sakafuni.
Hivi ni kusema kwamba mjua lugha anafahamu sheria za kuunda sentensi katika lugha yake.  Sheria hizi zimo katika akili yake.

Swali:

  Je, kuna mambo mengine mbali na usarufi wa tungo
   anayofahamu mjua lugha kuhusu sentensi au tungo
   katika lugha yake?



Ndiyo.  Mjua lugha ye yote anayo maarifa yanayomwezesha kutofautisha kati ya aina za sentensi katika lugha yake kutegemea kusudio la sentensi hiyo.  Anajua, kwa mfano, ni tungo zipi ni za kuuliza, na aina za maswali yanayoweza kuulizwa, pamoja na majibu yanayotegemewa.  Atajua kwamba aliyoisikia ni taarifa, utani, kebehi, mshangao na kadhalika.  Kwa mfano, ikiwa mjua Kiswahili ataulizwa “Mtoto yuko wapi?” atatambua kwa urahisi kuwa jibu lake ni “Amelala” na wala si “Ndiyo”.

Ishara hii * inadhihirisha kuwa sentensi fulani si sahihi.
Aidha, mjua lugha anayo maarifa yanayompa utambuzi kuwa tungo zifuatazo hazihitaji kujibiwa kwa maneno, ila pengine kwa vitendo, kwa sababu ni tungo za utendaji.
    Tafadhali nipe maji ya kunywa.
    Simba huyo ananguruma, tutoroke.

4.  Ubunifu
Mjuzi wa lugha huwa na ubunifu.  Ujuzi wa lugha humwezesha mtu kuunganisha maneno kuunda virai, na kuunganisha virai kuunda sentensi.

Huwezi kununua kamusi ya lugha iliyoorodhesha sentensi zote zinazopatikana katika lugha hiyo.  Utakachopata ni orodha ya maneno ya lugha hiyo.  Kujua lugha ni kuwa na uwezo wa kubuni sentensi mpya ambazo hazijawahi kutamkwa.  Vile vile ni kuelewa sentensi ambazo hazijawahi kutamkwa.

Kujua lugha ni kujua zile sentensi ambazo zinakubalika katika hali fulani.  Kwa mfano, ukisema, “Chapati huuzwa shilingi kumi” baada ya mtu kukukanyaga anapopita utakuwa si usemi mwafaka.

Swali:

   Je, kuna wakati katika mazungumzo unapokariri aina fulani za
   sentensi au maneno?  Toa mifano.

Katika kurasa chache zilizopita tumeeleza yale ambayo mtu aliye na ujuzi wa lugha anafahamu.  Mambo haya hufahamikaje?  Huwa yanawekwa wazi katika taaluma inaoyitwa isimu.  Hebu sasa tueleze maana ya Isimu.

Maana ya Isimu

Wataalamu mbalimbali wameeleza maana ya isimu.  Besha (1994:11) anaeleza kuwa isimu ni taaluma ambayo inachunguza na kuweka wazi kanuni ambazo ndizo msingi wa kila lugha.  Nayo Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) inaeleza kuwa isimu ni sayansi ya lugha.  Basi, tunaweza kusema kuwa isimu ni taaluma inayohakiki lugha kisayansi.  Isimu ni sayansi ya matamshi, maumbo, miundo, maana na matumizi ya lugha.  Isimu inatumia mtazamo wa kisayansi kuchambua lugha kinyume na ilivyokuwa hapo zamani ambapo wafanya utafiti waliathiriwa na hisia na mielekeo yao.

Taaluma hii hujaribu kujibu maswali kuhusu lugha ambayo watu wametaka kujua tangu zamani.  Maswali haya ni kama:
    Lugha ni nini?
    Lugha hufanyaje kazi?
    Huwa unajua nini unaposema kuwa unajua lugha fulani?
    Je, lugha ni sifa ya binadamu pekee?
    Lugha ya binadamu hutofautianaje na mawasiliano ya wanyama?
    Asili ya lugha ni ipi?
    Kwa nini kuna lugha nyingi?
    Lugha hubadilikaje?
    Watoto hujifunzaje lugha?
    Lugha au lahaja fulani ni rahisi kuliko nyingine?
Mtu huandikaje na kuchanganua lugha ambayo bado haina maandishi?

Wataalamu ambao wanashughulikia haya maswala ya lugha huitwa wanaisimu.  Kwa muda mrefu watu wamefikiria kwamba mwanaisimu ni mtu anayezungumza lugha nyingi.  Walichukulia mwanaisimu kama mtu anayezungumza, kwa mfano, Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kizulu na Kijerumani.  Lakini maana ya ‘mwanaisimu’ katika taaluma ya isimu si hiyo.  Si lazima mwanaisimu azungumze au awe na ufasaha wa lugha mbalimbali; anatakiwa tu kuwa na ujuzi au tajriba itakayomwezesha kuchambua lugha mbalimbali.  Mwanaisimu ni mtu anayechunguza lugha kisayansi.  Yeye ni mjuzi wa kanuni zinazotawala lugha.  Ni muhimu kwake kuchanganua na kueleza matukio ya kiisimu kama vile mfumo wa vokali katika lugha ya Kifaransa, au vitenzi vya Kiswahili, kuliko kujaribu kueleweka awapo Paris au Mombasa.

Baada ya kuelezea maana ya isimu na mwanaisimu ni nani, sasa tutakueleza machache kuhusu malengo ya isimu.

Malengo ya Isimu

Lengo la kwanza la taaluma ya isimu ni kuchambua na kueleza maarifa aliyo nayo mjua lugha kuhusu lugha yake.  Ili kufanya hivyo, mwanaisimu anachunguza lugha tofauti na kuona taratibu zinazotawala sarufi za lugha hizi, na kutokana na taratibu hizo anatoa majumlisho kuhusu lugha za wanadamu.

Ifahamike kwamba lengo la isimu si kuwafundisha watu jinsi ya kuzungumza lugha yao, yaani kipi waseme na kipi waache.  Isimu inaweka wazi kanuni zinazotawala lugha, ambazo wazungumzaji wanazitumia bila wao wenyewe kuzijua.  Mwanaisimu anachambua lugha yo yote bila kujali inazungumzwa wapi, na nani, au kwa madhumuni gani.  Mwanaisimu anaangalia maneno na miundo ya lugha husika na kuichambua bila ubaguzi, na kuchunguza kanuni zinazotawala matumizi hayo.

Lengo la pili la isimu ni kuunda nadharia.  Hili ni lengo la sayansi zote.  Watu wengi hutetemeshwa na neno ‘nadharia’.  Wengi huona kuwa nadharia inarejelea mambo tata yanayohitaji urazini wa hali ya juu na yaliyojitenga na uhalisia; lakini hili si kweli.  

Nadharia ni mwongozo unaotoa mfumo wa kanuni na kategoria ambazo zinaweza kutumiwa kuchanganua data iliyotolewa.  Nadharia huundwa ili kueleza ukweli au uhalisia wa maisha.  Uhalisia tunaozungumzia hapa ni lugha.  Nadharia itasaidia kuonyesha ruwaza zilizomo katika lugha na jinsi inavyofanya kazi.  Nadharia itatupa maelezo ya kijumla yatakayoafiki si data ya awali tu bali nyingine yo yote mradi tu malengo yaingiliane.  Maelezo zaidi ya nadharia yapo katika somo la pili.  Mwanaisimu, kwa kuchunguza sarufi za lugha tafauti, hufikia mahitimisho fulani kuhusu muundo wa lugha ya wanadamu kwa jumla.

Kumbuka:

  Kila tunapotenda jambo tunaongozwa na nadharia fulani ingawa
  mara nyingi hatutambui hivyo.

Lengo la tatu la isimu ni kubainisha mbinu za kisayansi za kuchambua lugha ili matokeo yaweze kukubalika na yawe yamejengwa kwa misingi thabiti.  Hizi ni sifa za uchambuzi wo wote wa kisayansi, na kwa sababu ya umuhimu wake zitazungumziwa baadaye.

Muhtasari:

Katika somo hili mambo matatu yameshughulikiwa: ujuzi wa lugha, maana ya isimu, na malengo ya isimu.  Tumeona kuwa mtu anayejua lugha anao ujuzi wa haya yafuatayo:

·         Kutambua sauti zinazotumika katika kuunda maneno ya lugha na mfuatano au ruwaza ya sauti inayokubalika katika maneno.
·         Kutambua uhusiano uliopo baina ya sauti na maana.
·         Kutambua tungo ambazo zinavunja kanuni za sarufi ya lugha yake na zile ambazo hazivunji kanuni hizo.
·         Kutambua kwa urahisi kusudio la sentensi.
·         Kuwa na ubunifu.
Mjua lugha huyapata maarifa haya anapojifunza lugha yake kama mtoto mdogo katika mazingira ya kawaida ya kijamii.  Ni maarifa ambayo yakishakamilika hayafutiki tena kwa urahisi. Mjua lugha anatumia lugha yake bila yeye mwenyewe kuwa na habari kuwa anatumia maarifa changamano sana.  

Aidha, imebainika kwamba isimu ni taaluma inayohakiki lugha kisayansi na inayo malengo maalumu.









Zoezi:
    Angalia sentensi zifuatazo:

a.                   Batoto bake balikwenda manyumbani.
b.                   Mwanafunzi hodari hujulikana kutokana na kazi yake.
c.                   Hiyo mitoto yako naleta macheso hapa.
d.                   Watoto wamefika wa Hamisi na Tatu.
e.                   Leo ni leo, asemaye kesho ni mwongo.

Jibu maswali haya:
i.                        Ni sentensi zipi zinazokubalika.
ii.                        Sentensi zipi zina matatizo?  Eleza matatizo hayo.

Maelezo ya dhana:

    Kiarifu     -    Sehemu ya pili ya sentensi ambayo huwa na kitenzi,
                mtendwa na     chagizo.
    Kihisishi   -    Maneno yanayoonyesha hali ya kufurahi, uchungu,
                kushangaa nk.
    Kiima      -        Sehemu ya kwanza ya sentensi ambayo huelezwa na kiarifu.
    Onomatopea-     Neno linaloiga au kuwakilisha mlio wa kitu fulani.
    Ruwaza   -        Mpangilio wa vipashio vya lugha unaofuata utaratibu
                maalum.
    Tungo     -        Matokeo ya kuweka au kupanga pamoja vipashio sahihi ili
                kujenga vipashio vikubwa zaidi.
    Unasibu   -    Hali ya kutokuwepo kwa uhusiano wa moja kwa moja baina
                ya     neno na kiashiriwa.
    Virai        -    Kipashio cha kimuundo chenye zaidi ya neno moja lakini
                ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu.

Ishara zilizotumiwa:

    [  ]    Mabano haya hutumika kuonyesha ishara za kifonetiki yaani jinsi sauti
             zinavyotamkwa.

    &       na



  Marejeleo:


  1.      Besha, R.M. (1994), Utangulizi wa Isimu na Lugha.  Dar es Salaam,
                    Dar es Salaam University Press.
  2.  Fromkin, V. & Rodman, R. (1988), An Introduction to Language,  Fort
                     Worth,  Holt Rinehart and Winston Inc.
  3.  TUKI (1990), Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha,  Chuo Kikuu cha
                       Dar es Salaam.

SOMO LA NNE

VIWANGO VYA ISIMU


Utangulizi

Hapo mwanzoni mwa kitabu hiki tumeeleza kuwa isimu ni sayansi ya lugha (Tazama Somo la Kwanza). Katika somo hili tungependa kufafanua viwango mbalimbali vya isimu.  Tutajaribu kuonyesha uhusiano baina  ya  viwango hivi na jinsi uhusiano huu unavyomwezesha mtafiti wa lugha kuchunguza lugha kwa utaratibu maalumu.
 Malengo:

     Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutaja viwango vya kiisimu
·         Kufafanua mambo yanayozingatiwa katika kila kiwango.

Kwa kawaida tunachunguza lugha katika viwango mbalimbali,  navyo ni:
    (a)    Sauti
    (b)    Neno
c.       Sentensi
d.       Maana
e.                   Matumizi ya lugha

Viwango hivi vimepewa majina yafuatayo katika isimu:
Kiwango            Istilahi ya Kiisimu
Sauti                fonetiki na fonolojia
Neno                mofolojia
Sentensi            sintaksia
Maana                semantiki
Matumizi ya lugha        pragmatiki
Sasa tutazungumzia kila mojawapo ya viwango hivi ili tuone ni mambo yapi yanayozingatiwa katika kila kiwango.

1.    Fonetiki
Katika kiwango cha fonetiki tunashughulikia sauti za binadamu pamoja na kuchunguza ala za matamshi, namna ya kutamka, uelewa wa sauti, aina za vitamkwa, kusafiri kwa sauti na kusikika kwa sauti.

Katika fonetiki tunahakiki sauti za lugha ya mwanadamu katika viwango vitatu ambavyo ni:  fonetiki matamshi, fonetiki akustika na fonetiki sikizi.
a.                   Fonetiki matamshi ni tawi la fonetiki ambalo hushughulikia uchambuzi wa ala za kutamka na jinsi ya kutamka. Ala za kutamkia ni kama vile midomo, ulimi, meno na kinywa.
b.                   Fonetiki akustika ni tawi  la fonetiki ambalo hushughulikia misikiko ya sauti na namna sauti hizo zinavyosafiri baina ya kinywa cha msemaji na sikio la msikilizaji.
c.                   Fonetiki sikizi ni tawi la fonetiki ambalo hushughulikia upokeaji wa sauti na ufasiri wake.
Ujuzi wa fonetiki ni muhimu kwa mwanaisimu yeyote.  Jinsi tunavyohitaji kujifunza namna ya kusoma kabla ya kuchambua fasihi ndivyo tunavyohitaji ujuzi wa fonetiki kabla ya kuhakiki isimu.

Kumbuka:

Binadamu hutoa sauti za aina mbalimbali.  Sauti tunazoshughulikia hapa ni zile za lugha.  Binadamu anaweza kuwasiliana kwa sauti nyingine kama kukohoa au kupiga mwayo.  Hizi si sauti za lugha.

Fonetiki huhakiki sauti za lugha bila ya kuzihusisha na utaratibu wa mfumo wa lugha yaani matumizi yake.  Kwa hivyo, tunaweza kusema kwamba fonetiki huchunguza sauti ya lugha ya mwanadamu katika ujumla wake.  Kwa mfano [t] ni sauti ya lugha ya mwanadamu.  Kiungo cha kimsingi cha fonetiki ni foni.  Foni ni sauti za lugha ambazo hazijapewa hadhi.  Kwa mfano hizi ni foni katika lugha ya binadamu [a], [b], [g], [k].  Foni inapoandikwa inafungiwa katika mabano ya mrada – [ ].


2.    Fonolojia
Katika kiwango hiki tunashughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika lugha.  Kiwango hiki kinahakiki jinsi sauti zinavyofanya kazi katika lugha maalumu.  Kwa mfano /p/ ni fonimu ya neno ‘pahali’ katika lugha ya Kiswahili Uhakiki wa fonolojia umegawika katika sehemu nne muhimu zifuatazo:
1.       Kuorodhesha fonimu za lugha mbalimbali.
2.       Mfuatano wa fonimu na silabi unaokubalika katika lugha fulani.  
Kwa mfano, Kiswahili kina muundo wa konsonanti, vokali, konsonanti vokali (KVKV), kama katika neno ‘kata’.
3.                   Harakati au mifanyiko ya kifonolojia.  
Kwa mfano, katika Kiswahili sauti /k/ ikifuatwa na /i/ hubadilika na kuwa /sh/; kama vile  pika  mpiki mpishi.
Huu ni uhusiano wa fonimu katika matumizi yake.
4.                   Fonolojia arudhi/sifa arudhi.  
Sehemu hii huangalia vipashio kama toni, shadda, kiimbo na wakaa.

Kuna vipashio ambavyo ni muhimu katika fonolojia. Kipashio cha kwanza muhimu cha fonolojia ni fonimu.  Fonimu ni kiungo cha kimsingi katika uhakiki wa fonolojia.  Fonimu ni kiungo kidogo kabisa cha sauti katika lugha kinachoweza kutenga maneno mawili kimaana.
Kwa mfano:    Pata    Haya ni maneno mawili yenye maana tofauti inayotokana na
        Bata    sauti /p/ na /b/.  Kwa hivyo /p/ na /b/ ni fonimu za lugha ya
            Kiswahili.

Tofauti inaweza kuwa mwanzoni mwa neno kama toa au katikati kama ala                                                                                               
                                                                       doa                        ada

Tofauti inaweza kuwa mwishoni mwa neno kama  hama
                                                 hamu

Fonimu zenyewe hazina maana lakini zimepewa hadhi ya kusaidia kuleta  tofauti za kimaana.  
Kipashio cha pili ni alofoni. Neno hili  lina sehemu mbili: alo na foni.  Mzizi wa neno hilo ni foni, ambacho ni kipashio kidogo cha sauti kisichohusishwa na lugha yoyote ile.  Alo ni kiambishi chenye maana ya wingi.  Wataalamu wameeleza alofoni kwa njia tofauti:
a.                   Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha inaeleza kuwa alofoni ni umbo jingine la fonimu moja.  Kwa hivyo ikiwa sauti mbili zinaweza kuchukua nafasi sawa katika neno bila kubadili maana basi sauti hizi zitaitwa alofoni za fonimu moja.
b.                   Maelezo ya Hartman (1972) yanaingiliana na hayo ya hapo juu lakini anatoa habari za ziada.  Anasema kuwa alofoni ni sauti mojawapo miongoni mwa kundi la sauti na kwamba alofoni hutokea katika mazingira mahsusi.
c.                   Maoni hayo ndiyo yanayoshadidiwa na Ladefoged (1962) anapoeleza kuwa alofoni ni matamshi tofauti ya fonimu moja, na hizo alofoni huunda kundi moja la sauti ambazo:
(i)         hazibadili maana ya neno.
                               ii.            hutokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki.
iii.                        hufanana sana kifonetiki.
Hapa kuna mfano wa alofoni ambazo zinatokea katika mazingira tofauti ya kifonetiki, hazibadili maana ya neno, na zinafanana kifonetiki.



            [t]    Sauti hii hutokea katika Kiingereza ikiwa kipasuo
kitakuwa katikati mwa neno.  Kwa mfano, star.

[th]    Sauti hii ya mpumuo hutokea ikiwa vipasuo sighuna
/t/                vitakuwa mwanzoni mwa neno la Kiingereza.
Kwa mfano: tar.

             t    Hii ni sauti inayotamkiwa kwenye meno badala ya
                              Π    ufizini.     

            [t ¬ ]    Sauti hii hutokea ikiwa itakuwa mwishoni mwa neno
la Kiingereza. Kwa mfano, start.  Hii ni sauti isiyoachiliwa kwa haraka.

Ikiwa basi lazima alofoni itimize sifa hizo tatu zilizotajwa na Ladefoged (1962), basi hakuna alofoni katika lugha ya Kiswahili.
3.    Mofolojia

Mofolojia ni kiwango CHA ISIMU kinachoshughulikia uchambuzi wa muundo wa maneno katika lugha.  Mofolojia ni uhakiki wa viungo vidogo kabisa katika lugha vyenye maana na mpangilio wake katika maneno.  Kuna vipashio ambavyo ni muhimu katika mofolojia.
Kipashio cha kwanza ni mofimu.  Mofimu ni kiungo kidogo kabisa katika lugha chenye maana.

Kwa mfano:  Mtoto       tofauti kati ya maneno haya ni (m) na (wa)
        Watoto

M/ toto      -    {m}      ni mofimu ya ngeli ya kwanza inayorejelea umoja.

        -    {toto}  ni shina au mzizi wa neno wenye maana ya kiumbe
 mdogo  ambaye bado hajakomaa

Wa/ toto          -    { wa}  ni mofimu ya ngeli ya pili inayorejelea wingi.

Mfano mwingine ni huu wa sentensi ‘Alitaka’

A\li\tak\a           {a} -  ni kiambishi cha mtenda katika ngeli ya kwanza.
            {li} -   ni kiambishi cha wakati uliopita.
               {tak} - ni mzizi wa kitenzi.
             {a}   -  ni kiishio

Mofimu huonyeshwa kwa mabano ya mbinuko yaani { }.

Kipashio cha pili ni mofu.  Mofu ni muundo halisi unaodhihirisha mofimu.  Mofu ni segmenti za neno zinawakilisha mofimu.  Kwa hivyo, mofu ni lile umbo tunalotamka na kuliandika lakini mofimu ni ile maana.
Kwa mfano:

Neno        Mofu            mofimu
1.    watched    watch-ed        watch + past
2.    alipiga        a-li-pig-a         a        -     ni nafasi yatatu umoja
                         li    -     ni wakati uliopita
                         pig     -     ni mzizi wa kitenzi
                          a     -     ni kiishio.

Mofu huonyeshwa kwa mabano ya msharazi, yaani //

Kipashio cha tatu ni alomofu.  Alomofu ni sura tofauti za mofimu moja.  Hizi ni mofimu mbili zenye maana sawa lakini maumbo tofauti.  Kwa mfano, mofimu ya umoja katika ngeli ya kwanza katika Kiswahili huweza kuonyeshwa kwa njia tofauti.
           /m/        mtu
{m}          /mu/        muumba
          /mw/     mwalimu

Kwa hivyo /m/  /mu/  na /mw/  ni alomofu za mofimu {m}.

Pia katika Kiingereza, kimsingi, wingi huonyeshwa kwa mofimu {s} ambayo inaweza kuwa na sura mbalimbali.  Sura hizi mbalimbali hujitokeza katika matamshi.

z____      katika boys, dogs, ribs
    s ____  katika lamps, cats, books
    iz ____ katika sizes, boxes, churches
Ø ____ katika sheep
en ___  katika oxen

Hali hii inaweza kuonyeshwa hivi.
            /z/
            /s/
    {s}        /iz/       
            /Ø/       
            /en/

Kwa hivyo /z/, /s/ iz/  /Ø/  /en/ ni alomofu za mofimu {s} katika Kiingereza.


Swali:


Onyesha mofimu zinazojitokeza katika maneno haya
1.       anahubiri
2.       aliandika
3.       hakuwapiga
4.       siendi
5.       tuliomba

Kumbuka kuwa unapoonyesha mofimu sharti ueleze maana ya maumbo yaliyotengwa.

Uundaji wa maneno pia huzingatiwa katika mofolojia.  Katika lugha ya Kiswahili, maneno huundwa kwa kuzingatia mbinu mbalimbali.  Maneno huweza kuundwa kwa njia zifuatazo:
1.       Kuunda majina kutokana na vitenzi.  Kwa mfano, kutokana na neno ‘lima’ tunapata ‘mkulima’,  ‘pika’ tunapata ‘mpishi’.
2.       Kukopa msamiati kwa kutohoa.  Kwa mfano, bicycle baiskeli, television   televisheni.
3.       Kutafsiri – Kwa mfano:  army worm – viwavijeshi.
4.       Kubuni kwa kutumia vigezo maalumu kwa mfano, kunguni, kifaru nk.
5.       Akronimu, yaani kule kuchukua sehemu za kwanza za kila neno katika kishazi ili kuziunganisha na kuwa neno moja.  Kwa mfano, Upungufu wa Kinga Mwili  linakuwa Ukimwi.
6.       Onamatopea.  Haya  ni maneno yanayoiga au kuwakilisha kitu fulani.  Kwa mfano, pikipiki.

Swali:

Huku ukitumia mbinu tulizotaja hapo juu kuhusu uundaji wa maneno, onyesha jinsi maneno yafuatayo yameundwa katika Kiswahili.

a.                   Tingatinga
b.                   Mpishi
c.                   Hospitali
d.                   Chajio
e.                   Skuli

4.    Sintaksia

Sintaksia ni kiwango kinachoshughulikia uchanganuzi wa mpangilio na uhusiano wa vipashio katika sentensi.  Hapa tunahakiki namna maneno yanavyopangwa ili kuunda sentensi zenye maana katika lugha.

Lugha ya binadamu hufuata utaratibu ambao unaongozwa na sheria maalumu za kiisimu.  Kwa hivyo, maneno huungana kwa kufuata sheria za kiisimu ili kuunda sentensi zenye maana. Kwa mfano, katika Kiswahili mojawapo ya sheria za kiisimu ni kuwa vivumishi hufuata nomino katika sentensi.  Basi, sentensi; ‘Kijana mrefu amekuja’ ni sentensi ambayo inafuata sheria hii ya sarufi ya Kiswahili, kwa sababu kivumishi ‘mrefu’ kinafuata nomino ‘kijana’.  Lakini mfuatano wa maneno; ‘mrefu kijana amekuja’ si sahihi kwa sababu sheria iliyotajwa hapo juu haikufuatwa.

Kipashio muhimu cha sintaksia ni sentensi.  Sintaksia pia huchunguza kategoria mbalimbali za maneno kulingana na utendakazi wake katika sentensi.  Kategoria hizi ni nomino, viwakilishi, vitenzi, vivumishi, vielezi, viunganishi, vihusishi na vihisishi.  Kategoria hizi za maneno ndizo hutumiwa katika sentensi.
Kumbuka:


Kila lugha ina sheria zake za kuunda sentensi ambazo ni tofauti na za lugha nyingine.

Dhana nyingine inayojitokeza ni ile ya kuigawa sentensi katika sehemu kulingana na uamilifu wa sehemu hizo.  Kuna kiima na kiarifu.  Kiima ni sehemu ya kwanza ya tungo ambayo huelezwa na kiarifu.  Kiarifu ni sehemu ya pili ya sentensi yenye kitenzi, shamirisho na chagizo.

Sintaksia pia hueleza juu ya aina za sentensi. Kuna aina tatu kuu za sentensi:
1.       Sentensi sahili.  Hii ni sentensi ya kimsingi kabisa. Kwa mfano; Juma ni mvulana mzuri.  Huwa na kikundi nomino kimoja tu katika kiima.
Aghalabu huwa na kitenzi kimoja na hutoa habari chache.
2.                   Sentensi changamano.  Hii ni sentensi iliyo na vishazi viwili: kishazi huru na kishazi tegemezi .  Kishazi huru hujisimamia kama sentensi kamili, kwa kweli huwa ni sentensi sahili.  Kishazi tegemezi huwa ni kishazi kisicho kamili, kinategemea kishazi huru ili kukamilika.  Kishazi kitegemezi hutoa habari za ziada kuhusu kishazi huru.  Angalia sentensi hizi:
(a)    Mwanafunzi aliyeleta vitabu hivi ameondoka.  
   Kishazi huru:   Mwanafunzi ameondoka.  
   Kishazi tegemezi: Mwanafunzi aliyeleta vitabu hivi.
(b)    Ochieng ambaye ni mkufunzi wa chuo kikuu amepotea.
    Kishazi huru:  Ochieng amepotea.
    Kishazi tegemezi:  Ochieng ambaye ni mkufunzi wa chuo kikuu.
    3.  Sentensi ambatano/unganishi.
Aina hii huwa na sentensi  mbili zenye uzito sawa au vishazi huru viwili.  Sentensi hizi huwa na kiunganishi kama; na,  pamoja,  kisha,  halafu na   lakini.
Kwa mfano:    Juma analima lakini Maria anasoma.
Sentensi 1:    Juma analima
Sentensi 2:    Maria anasoma.

Swali:   

Tunga sentensi mbilimbili za aina ya sahili, changamano na ambatano.

5.    Semantiki
Kiwango hiki kinashughulikia maana katika lugha.  Semantiki ni sayansi ya maana na matumizi ya maneno.  Kwa mfano:  (a)    Yule farasi anakwenda kupika.
b.       Nyumba yetu imeandika kitabu kizuri sana.

Sentensi  hizi hapa juu hazina maana kwa sababu hazina mantiki lakini ni sahihi kisarufi.  Kwa hivyo, sentensi inaweza kufuata sheria zote za kisintaksia lakini isikubalike kwa sababu haina maana.
Katika semantiki, tunachunguza maana katika viwango viwili.
a.       neno
b.       sentensi.
Katika kiwango cha neno, tunaweza kuwa na:
1.    Visawe au sinonimu
Maneno yenye maana sawa au zinazokaribiana huitwa visawe.
Kwa mfano: rafiki-sahibu,  mahabubu, mpenzi,  muhibu,  mwandani.

2.    Antonimu
Haya ni maneno yanayoonyesha kinyume.  Maana katika antonimu hukinzana.
Kwa mfano:        panda    -    shuka
            ukweli    -    uwongo
            moto    -    baridi
            kubwa    -    ndogo
3.    Polisemia
Hili ni neno moja lenye maana nyingi.
Kwa mfano:  Neno ‘kata’ lina maana mbalimbali:
1.       Majani au kitambaa kilichoviringwa cha kubebea mizigo kichwani.
2.       Kamba ndefu iliyoviringwa
3.       Kipande cha pamba afungiwacho mtoto baada ya kutahiriwa.
4.       Mtaa.
5.       Chombo kinachotengenezwa kutokana na kifuu cha nazi na kutiwa mpini; hutumiwa kuchotea maji.
Swali:

Andika mifano ya maneno matatu matatu yanayowakilisha dhana hizi:  visawe, antonimu na polisemia.

Katika kiwango cha sentensi, maana hupatikana kwa njia mbalimbali.  Njia ya kwanza ni kutokana na jumla ya maneno yaliyomo katika sentensi.

Njia ya pili ni ile ya maana kiarudhi.  
Hii ina maana kwamba maana ya  sentensi inaweza kubadilika kulingana na kiimbo, muundo au shadda;
Kwa mfano:
(i)    Kiimbo   -    Mtoto amekula chakula chote (taarifa)
  -    Mtoto amekula chakula chote? (Swali)
·         Mtoto amekula chakula chote! (mshangao)

(ii)    Shadda -     Mwalimu alinunua gari jekundu
Shadda imewekwa kwenye neno ‘gari’.  Hii ina maana alinunua ‘gari’ sio
baiskeli.
Mwalimu alinunua gari jekundu
Shadda imewekwa kwenye neno ‘jekundu’.  Hii ina maana alinunua gari
jekundu sio la kijani.
Mwalimu alinunua gari jekundu.
Shadda imewekwa kwenye neno ‘mwalimu’.   Hii ina maana ni ‘mwalimu’ sio
mkulima.
                  iii.Maana kimuundo/kisarufi
Mfano:    Juma alimpiga Maria
        Maria alipigwa na Juma
Katika sentensi hizi mpangilio ni tofauti lakini maana ni sawa.
Swali:

Andika sentensi mbili mbili zinazowakilisha kiimbo, shadda na maana kimuundo.

Pragmatiki

Tawi hili la isimu huchanganua lugha kwa kuzingatia muktadha, desturi, na vikwazo vya kijamii.  Pia huitwa isimu – amali.  Pragmatiki ni uchunguzi wa maana isiyo wazi, au jinsi tunavyoweza kutambua maana iliyokusudiwa hata kama haikusemwa bayana.  Katika pragmatiki msikilizaji anajitahidi kuelewa si tu maana ya maneno yaliyotumika bali pia lile alilokusudiwa kuwasilisha mzungumzaji.
Kumbuka:


Ni muhimu kutambua kwamba lugha ni mfumo na mfumo huu unajitojeza kupitia viwango vya fonetiki, fonolojia, mofolojia, sintaksia, semantiki na pragmatiki.

Swali:

Fafanua viwango mbalimbali vya kiisimu kwa kueleza mambo yanayozingatiwa katika kila kimoja.

Zoezi:

Huku ukizingatia viwango vyote vya kiisimu, onyesha shida zinazowakabili wanafunzi katika ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili.

Muhtasari:

Katika somo hili tumetaja na kueleza viwango vya isimu.  Tumeonyesha kinachozingatiwa katika kila kiwango na imebainika kwamba viwango hivi vinategemeana katika kufanikisha uchanganuzi wa lugha.

Marejeleo:


Besha, R.M. (1994), Utangulizi wa Lugha na Isimu, Dar es Salaam, Dar es Salaam
                   University Press.
Crystal, D (1995), The Cambridge Encyclopaedia of Language, New
                   York, Oxford University Press.
Crystal,  D. (1971), Linguistics, London, Penguin Books.
Fromkin, V. & Rodman, B. (1988), An Introduction to Language,     
                    Forth Worth, Holt Rinehart and Winston Inc.
Hartman, R. (1972), Dictionary of Language and Linguistics, London,
                    Applied Science Publisher.
Mfaume, G.E. (1985), Misingi ya Isimu na Lugha ya Kiswahili, Dar-es-
                     Salaam Utamaduni Publishers.
Mgullu, R.S. (1999), Mtalaa wa Isimu, Nairobi, Longhorn Publishers.
TUKI (1990), Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha.  Dar es Salaam, TUKI
Widdowson, H.G. (1996) Linguistics, Oxford, Oxford University Press
SOMO LA SITA
MAANA NA SIFA ZA LUGHA
Utangulizi
Katika somo hili tungependa kufafanua dhana ya lugha.  Dhana hii ni ngumu kueleza na basi tutachunguza fafanuzi za wataalamu mbalimbali ili kutokana na fafanuzi hizi tuweze kuitolea dhana hii ufafanuzi unaofaa.  Baadaye tutajaribu kueleza sifa kuu za lugha.
Malengo:
Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutoa fafanuzi zilizotolewa na wataalamu mbalimbali za dhana ya lugha.
·         Kueleza maana ya lugha.
·         Kutaja na kueleza sifa kuu za lugha.

Dhana ya lugha ni ngumu kufafanua.  Hebu zingatia mifano ifuatayo ya maana ya lugha iliyotolewa na wanafunzi mbalimbali.
1.       Lugha ni njia ya mawasiliano.
2.       Lugha ni kusema.
3.       Luga ni kama Kiswahili, Kiingereza na kadhalika.
4.       Lugha ni njia ya kubadilishana mawazo.
5.       Lugha ni chombo cha fikra.
Majibu haya yote yana upungufu na yanaonyesha ugumu wa kueleza dhana ya lugha.  

Swali:

Je, wewe unaweza kusema lugha ni nini?

Wanaisimu wengi wametoa fafanuzi za lugha.  Kutokana na fafanuzi hizi tunaweza kuelewa vizuri maana ya lugha.Hebu sasa tuzingatie baadhi ya fafanuzi hizi.
Sapir (1921) katika kitabu Language: amesema kuwa lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie kuwasilisha mawazo, maono na mahitaji yake.  Mfumo huu hutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari. Bloch na Trager (1942) katika Outline of Linguistic Analysis wanasema kuwa lugha  ni mfumo wa ishara nasibu za sauti ambazo hutumiwa katika ushirika wa jamii. Trudgil (1983) katika Sociolinguistics: An Introduction to Language and Society anasema kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.  Chomsky (1957) katika  Syntactic Structures anasema kuwa lugha ni mkusanyiko wa sentensi zenye urefu unaotabirika na zinazoundwa kutokana na idadi maalumu ya viambajengo.  Crystal (1985) katika A Dictionary of Phonetics and Linguistics:  anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa mawasiliano ya wanadamu ambao hutumia mpangilio  maalumu wa sauti kuunda vipashio.
TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha inasema kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.
Kutokana na fafanuzi hizi za wataalamu mbalimbali, tunaelekezwa kwenye fasiri ya kijumula ambayo ndiyo tutatumia katika kozi hii.  Nayo ni, “Lugha ni mfumo wa ishara nasibu za sauti wenye maana unaotumiwa na mwandamu katika mawasiliano”.

Sifa Kuu za Lugha

Fasiri ya kijumla ya lugha tuliyotoa hapo juu inatuelekeza kwenye sifa za lugha.  Hebu sasa tuzifafanue sifa zenyewe.

1.  Lugha ni Mfumo

Mfumo ni mkusanyiko wa vitu unaofuata ruwaza fulani na uhusiano maalumu.  Katika lugha, mfumo humaanisha mpangilio maalumu wa vipashio vinavyotegemeana na  kukamilishana katika lugha.
Kila lugha huwa na mifumo miwili, mfumo wa sauti na mfumo wa maana.  Ni sauti fulani tu zinazotumika na wazungumzaji wa lugha fulani, na sauti hizi sharti zifuate mpangilio maalumu unaokubalika katika lugha hiyo. Kwa mfano:
tunasema  ‘bapa’     sio ‘baap’      (Kiswahili)
tunasema ‘bank’      sio    ‘nbka’    (Kiingereza)
tunasema ‘Nilifika hapa Jumamosi’ sio
        ‘Jumamosi hapa nilifika’.
Mfumo wa sauti huwezesha idadi ndogo ya sauti kutumiwa tena na tena  zikiwa zinaunganishwa kwa njia mbalimbali ili kuunda vipashio vyenye maana. Nao mfumo wa maana huwezesha vipashio hivi kupangwa kwa njia zisizo kikomo ili kuwasilisha dhana sahili na tata.
Kumbuka:

Kila lugha huwa na mfumo wake hivi kwamba sauti za lugha fulani hupangwa kwa njia maalumu.

2.    Lugha ni Ishara
Lugha huundwa na viungo vya sauti ambavyo huungana kujenga semi zenye maana.  Matamshi hayo ni ishara kwani huwakilisha kitu fulani.  Kwa mfano, ‘mtu’ ni ishara  inayosimamia maana fulani.  Sauti hizi zenyewe huwa hazina uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachowakilishwa na sauti hizo.  Huwa ni kiwakilishi tu cha dhana zinazorejelewa.
3.    Lugha ni Nasibu
Hii ina maana kwamba hatuwezi kutabiri sifa maalumu zitakazopatikana katika lugha fulani ikiwa hatuifahamu lugha hiyo.  Huwezi kutabiri maana ya neno, katika lugha hiyo ngeni, unapolisikia, au idadi ya sauti – konsonanti na vokali-zilizomo.
Aidha hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya sauti na maana  ya sauti hiyo.  Hakuna sababu yoyote kwa mfano ya kuita chombo  unachokalia ‘kiti’ kwa sababu chombo hicho kitabakia hicho hicho kwa neno lingine lolote lile kama  ‘chair’ kwa Kiingereza.  Muundo wa neno unaotumika kuwakilisha dhana yoyote  unatokana na makubaliano na mazoea ya watu wa jamii ya lugha inayohusika.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanadai kuwa baadhi ya maneno katika lugha fulani huundwa kwa njia ya kionomatopea.  Haya  ni maneno yanayoiga au kuwakilisha milio ya vitu fulani.  Kwa mfano, neno ‘pikipiki’ linatokana na mlio wa  chombo hicho.
Zoezi:

Andika maneno mengine matano ya kionomatopea katika lugha ya Kiswahili.

4.    Lugha ni Sauti
Msingi wa lugha yoyote ni matamshi au maongezi, si maandishi.  Lugha zote ulimwenguni hutegemea vitamkwa kuleta maana. Ithibati zilizopo kuhusu kustawi kwa jamii kongwe, kujifunza lugha kwa watoto wachanga na kuwepo kwa rekodi za kihistoria, zote zinathibitisha kwamba mazungumzo yalitangulia maandishi.  Maandishi ni namna ya kuweka matamshi na maana yake katika hifadhi.

5.    Lugha ni  Mawasiliano

Lengo kuu la lugha ni kuwasiliana.  Lugha huwawezesha watu kupashana habari.  Lugha ndiyo nguzo ya jamii kwa sababu inawawezesha watu kuishi, kufanya kazi, kucheza pamoja, kusema ukweli na uwongo. Lugha huwawezesha watu kuzungumza juu ya jambo lolote lililo katika ufahamu wao kwa kutumia sauti.  Maingiliano baina ya binadamu hutegemea lugha.  Lakini lazima tukumbuke kwamba binadamu hawasiliani kwa lugha tu, zipo njia nyingine anazotumia.
Zoezi:

Taja njia nyingine tatu, mbali na lugha, anazotumia binadamu kuwasiliana.
6.    Lugha hutumiwa na Jamii yenye Utamaduni wake
Ni kweli kwamba wanadamu wamepewa lugha nyingi sana na hizi lugha ni miongoni mwa sifa ambazo hutumiwa kuwatofautisha watu wa jamii tofauti.  Utagundua kuwa aghalabu watu hujulikana kwa lugha wanazozungumza; Mteso huzungumza Kiteso, Mkamba huzungumza Kikamba, na Mkuria huzungumza Kikuria.  Kwa jinsi hii tunaona kwamba lugha ni kitambulisho cha jamii.
Pia kila lugha hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama sehemu mojawapo muhimu ya utamaduni wa jamii.  Kwa hali hiyo, lugha huwa ni mali ya jamii fulani ambayo ina utamaduni wake.

7.       Lugha ni Sifa au Chombo cha Binadamu Pekee

Wanaisimu pamoja na watafiti wengine wa lugha wamegundua kuwa hakuna wanyama wenye uwezo wa kutumia lugha kama binadamu.  Binadamu ameumbwa na uwezo wa kuimudu lugha, hazaliwi akiwa anafahamu lugha.  Wanyama wengine huzaliwa na kutoa milio fulani tu.  Hata wakifundishwa lugha ya binadamu hawataimudu.  Ili kulifafanua swala hili vyema itabidi tuangalie sifa bia ambazo zimejadiliwa katika somo la nane.
Kumbuka:

Ni muhimu tutambue kwamba ufafanuzi kamilifu wa dhana  ya lugha lazima uzingatie sifa saba tulizofafanua hapo juu.
Zoezi:
Eleza maana ya lugha huku ukirejelea sifa zake muhimu.

Muhtasari:


Katika somo hili tumejaribu kufafanua maana ya lugha.  Kwanza tumerejelea maana zilizotolewa na wataalamu mbalimbali, kisha kutokana na maelezo  hayo tumeweza kufafanua maana ya lugha kwa kurejelea sifa zake muhimu.

Maelezo ya dhana:

Ruwaza    -    ni mpangilio wa vipashio vya lugha unaofuata
                            utaratibu maalumu
Kiambajengo    -    Kipashio ambacho hushirikiana na vipashio vingine        
                             katika kukamilisha muundo wa kipashio kikubwa         
                             zaidi katika utaratibu wa kidaraja.
Kipashio    -    Umbo lenye sifa na hadhi ya kiisimu, kwa mfano        
                             katika fonolojia kuna fonimu, katika sintaksia kuna          
                             sentensi na katika mofolojia kuna fonimu.

Marejeleo:

Bloch, B. & Trager, G.L. (1942), Outline of Linguistic Analysis, Baltimore,  
                                  Waverly Press
Chomsky, N. (1957), Syntactic structures,  The Hague Morton.
Crystal, D. (1985), A Dictionary of Phonetics and Linguistics, Basic Blackwell,
                           Oxford.
Fromkin V. & Rodman B. (1988), An introduction to Language, Forth   
                   Worth, Holt Rinehart and Winston.

Mgullu, R.S. (1999)  Mtalaa wa Isimu, Nairobi, Longman Publishers.

Sapir, R. (1921) Language,  New York,  Harcourt, BraceWord.

Trudgill, P. (1983), Sociolinguistics:  An Introduction to Language and
                    Society (2nd ed.),  Hartmondworth, Penguin.

TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha,  Dar es Salaam, TUKI.

SOMO LA SITA
MAANA NA SIFA ZA LUGHA
Utangulizi
Katika somo hili tungependa kufafanua dhana ya lugha.  Dhana hii ni ngumu kueleza na basi tutachunguza fafanuzi za wataalamu mbalimbali ili kutokana na fafanuzi hizi tuweze kuitolea dhana hii ufafanuzi unaofaa.  Baadaye tutajaribu kueleza sifa kuu za lugha.
Malengo:
Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutoa fafanuzi zilizotolewa na wataalamu mbalimbali za dhana ya lugha.
·         Kueleza maana ya lugha.
·         Kutaja na kueleza sifa kuu za lugha.

Dhana ya lugha ni ngumu kufafanua.  Hebu zingatia mifano ifuatayo ya maana ya lugha iliyotolewa na wanafunzi mbalimbali.
6.                   Lugha ni njia ya mawasiliano.
7.                   Lugha ni kusema.
8.                   Luga ni kama Kiswahili, Kiingereza na kadhalika.
9.                   Lugha ni njia ya kubadilishana mawazo.
10.               Lugha ni chombo cha fikra.
Majibu haya yote yana upungufu na yanaonyesha ugumu wa kueleza dhana ya lugha.  

Swali:

Je, wewe unaweza kusema lugha ni nini?

Wanaisimu wengi wametoa fafanuzi za lugha.  Kutokana na fafanuzi hizi tunaweza kuelewa vizuri maana ya lugha.Hebu sasa tuzingatie baadhi ya fafanuzi hizi.
Sapir (1921) katika kitabu Language: amesema kuwa lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie kuwasilisha mawazo, maono na mahitaji yake.  Mfumo huu hutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari. Bloch na Trager (1942) katika Outline of Linguistic Analysis wanasema kuwa lugha  ni mfumo wa ishara nasibu za sauti ambazo hutumiwa katika ushirika wa jamii. Trudgil (1983) katika Sociolinguistics: An Introduction to Language and Society anasema kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.  Chomsky (1957) katika  Syntactic Structures anasema kuwa lugha ni mkusanyiko wa sentensi zenye urefu unaotabirika na zinazoundwa kutokana na idadi maalumu ya viambajengo.  Crystal (1985) katika A Dictionary of Phonetics and Linguistics:  anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa mawasiliano ya wanadamu ambao hutumia mpangilio  maalumu wa sauti kuunda vipashio.
TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha inasema kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.
Kutokana na fafanuzi hizi za wataalamu mbalimbali, tunaelekezwa kwenye fasiri ya kijumula ambayo ndiyo tutatumia katika kozi hii.  Nayo ni, “Lugha ni mfumo wa ishara nasibu za sauti wenye maana unaotumiwa na mwandamu katika mawasiliano”.

Sifa Kuu za Lugha

Fasiri ya kijumla ya lugha tuliyotoa hapo juu inatuelekeza kwenye sifa za lugha.  Hebu sasa tuzifafanue sifa zenyewe.

1.  Lugha ni Mfumo

Mfumo ni mkusanyiko wa vitu unaofuata ruwaza fulani na uhusiano maalumu.  Katika lugha, mfumo humaanisha mpangilio maalumu wa vipashio vinavyotegemeana na  kukamilishana katika lugha.
Kila lugha huwa na mifumo miwili, mfumo wa sauti na mfumo wa maana.  Ni sauti fulani tu zinazotumika na wazungumzaji wa lugha fulani, na sauti hizi sharti zifuate mpangilio maalumu unaokubalika katika lugha hiyo. Kwa mfano:
tunasema  ‘bapa’     sio ‘baap’      (Kiswahili)
tunasema ‘bank’      sio    ‘nbka’    (Kiingereza)
tunasema ‘Nilifika hapa Jumamosi’ sio
        ‘Jumamosi hapa nilifika’.
Mfumo wa sauti huwezesha idadi ndogo ya sauti kutumiwa tena na tena  zikiwa zinaunganishwa kwa njia mbalimbali ili kuunda vipashio vyenye maana. Nao mfumo wa maana huwezesha vipashio hivi kupangwa kwa njia zisizo kikomo ili kuwasilisha dhana sahili na tata.
Kumbuka:

Kila lugha huwa na mfumo wake hivi kwamba sauti za lugha fulani hupangwa kwa njia maalumu.

2.    Lugha ni Ishara
Lugha huundwa na viungo vya sauti ambavyo huungana kujenga semi zenye maana.  Matamshi hayo ni ishara kwani huwakilisha kitu fulani.  Kwa mfano, ‘mtu’ ni ishara  inayosimamia maana fulani.  Sauti hizi zenyewe huwa hazina uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachowakilishwa na sauti hizo.  Huwa ni kiwakilishi tu cha dhana zinazorejelewa.
3.    Lugha ni Nasibu
Hii ina maana kwamba hatuwezi kutabiri sifa maalumu zitakazopatikana katika lugha fulani ikiwa hatuifahamu lugha hiyo.  Huwezi kutabiri maana ya neno, katika lugha hiyo ngeni, unapolisikia, au idadi ya sauti – konsonanti na vokali-zilizomo.
Aidha hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya sauti na maana  ya sauti hiyo.  Hakuna sababu yoyote kwa mfano ya kuita chombo  unachokalia ‘kiti’ kwa sababu chombo hicho kitabakia hicho hicho kwa neno lingine lolote lile kama  ‘chair’ kwa Kiingereza.  Muundo wa neno unaotumika kuwakilisha dhana yoyote  unatokana na makubaliano na mazoea ya watu wa jamii ya lugha inayohusika.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanadai kuwa baadhi ya maneno katika lugha fulani huundwa kwa njia ya kionomatopea.  Haya  ni maneno yanayoiga au kuwakilisha milio ya vitu fulani.  Kwa mfano, neno ‘pikipiki’ linatokana na mlio wa  chombo hicho.
Zoezi:

Andika maneno mengine matano ya kionomatopea katika lugha ya Kiswahili.

4.    Lugha ni Sauti
Msingi wa lugha yoyote ni matamshi au maongezi, si maandishi.  Lugha zote ulimwenguni hutegemea vitamkwa kuleta maana. Ithibati zilizopo kuhusu kustawi kwa jamii kongwe, kujifunza lugha kwa watoto wachanga na kuwepo kwa rekodi za kihistoria, zote zinathibitisha kwamba mazungumzo yalitangulia maandishi.  Maandishi ni namna ya kuweka matamshi na maana yake katika hifadhi.

5.    Lugha ni  Mawasiliano

Lengo kuu la lugha ni kuwasiliana.  Lugha huwawezesha watu kupashana habari.  Lugha ndiyo nguzo ya jamii kwa sababu inawawezesha watu kuishi, kufanya kazi, kucheza pamoja, kusema ukweli na uwongo. Lugha huwawezesha watu kuzungumza juu ya jambo lolote lililo katika ufahamu wao kwa kutumia sauti.  Maingiliano baina ya binadamu hutegemea lugha.  Lakini lazima tukumbuke kwamba binadamu hawasiliani kwa lugha tu, zipo njia nyingine anazotumia.
Zoezi:

Taja njia nyingine tatu, mbali na lugha, anazotumia binadamu kuwasiliana.
6.    Lugha hutumiwa na Jamii yenye Utamaduni wake
Ni kweli kwamba wanadamu wamepewa lugha nyingi sana na hizi lugha ni miongoni mwa sifa ambazo hutumiwa kuwatofautisha watu wa jamii tofauti.  Utagundua kuwa aghalabu watu hujulikana kwa lugha wanazozungumza; Mteso huzungumza Kiteso, Mkamba huzungumza Kikamba, na Mkuria huzungumza Kikuria.  Kwa jinsi hii tunaona kwamba lugha ni kitambulisho cha jamii.
Pia kila lugha hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama sehemu mojawapo muhimu ya utamaduni wa jamii.  Kwa hali hiyo, lugha huwa ni mali ya jamii fulani ambayo ina utamaduni wake.

7.       Lugha ni Sifa au Chombo cha Binadamu Pekee

Wanaisimu pamoja na watafiti wengine wa lugha wamegundua kuwa hakuna wanyama wenye uwezo wa kutumia lugha kama binadamu.  Binadamu ameumbwa na uwezo wa kuimudu lugha, hazaliwi akiwa anafahamu lugha.  Wanyama wengine huzaliwa na kutoa milio fulani tu.  Hata wakifundishwa lugha ya binadamu hawataimudu.  Ili kulifafanua swala hili vyema itabidi tuangalie sifa bia ambazo zimejadiliwa katika somo la nane.
Kumbuka:

Ni muhimu tutambue kwamba ufafanuzi kamilifu wa dhana  ya lugha lazima uzingatie sifa saba tulizofafanua hapo juu.
Zoezi:
Eleza maana ya lugha huku ukirejelea sifa zake muhimu.

Muhtasari:


Katika somo hili tumejaribu kufafanua maana ya lugha.  Kwanza tumerejelea maana zilizotolewa na wataalamu mbalimbali, kisha kutokana na maelezo  hayo tumeweza kufafanua maana ya lugha kwa kurejelea sifa zake muhimu.

Maelezo ya dhana:

Ruwaza    -    ni mpangilio wa vipashio vya lugha unaofuata
                            utaratibu maalumu
Kiambajengo    -    Kipashio ambacho hushirikiana na vipashio vingine        
                             katika kukamilisha muundo wa kipashio kikubwa         
                             zaidi katika utaratibu wa kidaraja.
Kipashio    -    Umbo lenye sifa na hadhi ya kiisimu, kwa mfano        
                             katika fonolojia kuna fonimu, katika sintaksia kuna          
                             sentensi na katika mofolojia kuna fonimu.

Marejeleo:

Bloch, B. & Trager, G.L. (1942), Outline of Linguistic Analysis, Baltimore,  
                                  Waverly Press
Chomsky, N. (1957), Syntactic structures,  The Hague Morton.
Crystal, D. (1985), A Dictionary of Phonetics and Linguistics, Basic Blackwell,
                           Oxford.
Fromkin V. & Rodman B. (1988), An introduction to Language, Forth   
                   Worth, Holt Rinehart and Winston.

Mgullu, R.S. (1999)  Mtalaa wa Isimu, Nairobi, Longman Publishers.

Sapir, R. (1921) Language,  New York,  Harcourt, BraceWord.

Trudgill, P. (1983), Sociolinguistics:  An Introduction to Language and
                    Society (2nd ed.),  Hartmondworth, Penguin.

TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha,  Dar es Salaam, TUKI.

SOMO LA SABA

ASILI YA LUGHA

Utangulizi

Swala kuhusu asili ya lugha limeulizwa na kushughulikiwa na wataalamu wengi wa lugha na watu wengine kwa jumla.  Hili ni swala la kimsingi katika kuelewa binadamu na wanyama wengine.  Maoni mengi yamewahi kutoloewa lakini mpaka sasa hakuna jibu kamili lililowahi kupatikana na pengine halitapatikana.  Hii ni kwa sababu swala la asili ya lugha ni sawa na swala la asili ya binadamu au asili ya maisha kwa jumla.  Nadharia kadhaa zimependekezwa kueleza chimbuko la lugha lakini hizi zimebakia kuwa nadharia tu, uhakika haujapatikana.  Katika somo hili swala hili la asili ya lugha litajadiliwa hasa kwa kuzingatia nadharia mbalimbali zilizopendekezwa.

Malengo:

    Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutaja nadharia mbalimbali zinazotumiwa kuelezea asili ya lugha.
·         Kufafanua angalau nadharia moja yenye misingi ya kidini.
·         Kutoa tathmini kuhusu nadharia mbalimbali za asili ya lugha.

Swala hili la asili ya lugha limejadiliwa kwa muda mrefu.  Hakuna anayefahamu lugha imeanza kutumiwa lini lakini inaonekana kwamba maandishi yameanza kutumiwa kama miaka elfu sita iliyopita.  Haya yalitumiwa kwanza na Wasumeria.  Rekodi kama hizi zilijitokeza baada ya miaka mingi ya kutumia lugha na katu hazitupi fununu kuhusu asili ya lugha.

Nadharia kadhaa zimependekezwa kueleza chimbuko la lugha.  Nadharia hizo zaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo:
(a)        Nadharia za kale au zenye misingi ya kidini.
(b)        Nadharia za kipindi cha kati au za kimazingira.
(c)        Nadharia za kisasa au zenye misingi ya kisayansi.

Nadharia zenye Misingi ya Kidini

Nadharia za kale zinajumlisha nadharia za kidini na masimulizi katika makundi ya watu mbalimbali kuhusu asili ya lugha.  Wanaoshikilia msimamo huu wanaihusisha lugha na Mungu.  Wanaamini kuwa lugha ilibuniwa na Mungu.  Haya ni kwa mujibu wa imani za Kikristo na Kiyahudi.  Kwa mfano, katika Biblia kuna mstari unaosema kwamba:
    “Hapo mwanzo kulikuwako na neno, naye neno alitoka kwa
    Mungu, naye neno alikuwa Mungu.”  (Yohana 1:1)
Mawazo yanayojitokeza hapa ni kwamba hata kabla ulimwengu haujaumbwa kulikuwa na lugha.

Zoezi:

   
     “Mungu aliuumba ulimwengu kwa neno lake.  Alisema ‘ulimwengu
    na uwepo’ na ukawepo”.  Onyesha jinsi sentensi hii inavyoweza
     kutumiwa kufafanua asili ya lugha.

Aidha, inadhaniwa kuwa baada ya Mungu kuumba ulimwengu alimpa Adamu uwezo wa kuvipa vitu majina (Mwanzo 2:19).  Majina ambayo Adamu aliwapa wanyama hayakuwa ya kinasibu, jina lilihusiana na kuingiliana vizuri na kitajwa.

Swali:

  Unafikiri Adamu alitumia lugha gani alipokuwa akiwapa
  wanyama majina?

Wengine hudai kuwa Mungu alipomuumba Hawa ili akae na Adamu, palitokea mahitaji ya watu hawa kuongea.  Mungu akawapa lugha ili wawasiliane.

Inaonekana kwamba nadharia hii ya kidini inaingiliana sana na sifa za kimiujiza au kimazingaombwe ambazo zinahusishwa na lugha hasa ya mazungumzo.  Watoto katika tamaduni mbalimbali hutumia maneno ya kimazingaombwe kama ‘abracadabra’ ili kujiepusha na uovu au kuleta bahati nzuri.  Maneno yana nguvu fulani kwani mtu anapokutusi unaweza kumshtaki.  Watu huapiza na hubariki kwa kutumia maneno, na hata huendesha sala na kuzungumza na Mungu wakitumia maneno.  Kwa mujibu wa Biblia Takatifu, ni Mungu tu anayeweza kujibainisha anapoitwa kwani masanamu (vijimungu) hayafahamu lugha ya Mungu.  Vile vile, kuna maneno ambayo ni mwiko kuyataja katika tamaduni mbalimbali.

Zoezi:

    Ni maneno gani ambayo hamtakiwi kutaja ovyo ovyo katika jamii yenu?  
    Kwa nini?

Hata katika jamii za Wakristo na Wayahudi watu hukatazwa kutaja bure jina la Mungu wao.  Haya yote yanaonyesha kwamba lugha ina nguvu fulani na kama ni hivyo basi asili yake ni Mungu.

Yaonekana kuwa lugha ilikuwa moja ulimwenguni hadi wakati wa mnara wa Babeli ambapo watu walitaka kumfikia Mungu.  Mnara ukaanguka na watu wakazungumza ‘ndimi’ tofauti (Mwanzo 11:9).  Fikra kwamba kulikuwepo na lugha moja zamani kumepelekea watu kufanya utafiti ili kugundua sifa bia za lugha (Tazama somo la nane).

Kwa mujibu wa utamaduni wa Kihindi, lugha ilitolewa na Sarasvati, mke wa Brahma – muumba wa ulimwengu.  Makuhani wa Kihindu waligundua kwamba lugha yao ya ibada ilikuwa tofauti na lugha ya kawaida, na hivyo wakakubali ifanyiwe uchunguzi ili ihifadhiwe.  Hivyo ndivyo sarufi ya sanskrit ilivyoandikwa.

Wamisri wanadai kwamba mungu wao, Thoth, ndiye aliyeasisi mazungumzo na maandishi.  Watu wa Babylonia waliamini kuwa lugha imetoka kwa mungu wao anayeitwa Nabu.  Wachina wanaamini kuwa kasa mwenye maandishi mgongoni ndiye aliyetumwa kutoka mbinguni kuwaletea maandishi.

Zoezi:

  Andika masimulizi yanayotolewa na kabila lako kuhusu asili ya lugha.

Katika nadharia hizi za kidini tunaona mambo yafuatayo:
(a)  Lugha imetokea ghafla.
(b)  Lugha inahusishwa na majina au kuvipa vitu majina.
(c)  Lugha zote zilikuwa na chanzo kimoja.
(d)  Huwezi kuthibitisha au kukanusha nadharia hizi kwani kuwepo kwa Mungu
      hakuwezi kupimwa kisayansi.

Lugha ya Mwanzo Ulimwenguni

Kati ya wale waasisi wa nadharia za kidini za asili ya lugha kulitokea mshawasha wa kutaka kujua lugha ya kwanza iliyotumiwa ulimwenguni.  Walitaka kujua lugha iliyotumiwa na Mungu, Adamu na Hawa katika shamba la Edeni.  Watu wakajaribu kutafuta ukweli huo kwa kufanya majaribio kadha wa kadha.

Mwanahistoria wa Kigiriki, Herodotus, anaeleza kuwa katika karne ya tano KK Farao wa Misri aliyeitwa Psammetichus aliwatenga watoto wawili kwenye kibanda milimani palipo pweke, ambapo walihudumiwa na mtumishi bubu.  Farao aliamini kwamba watoto hawa wasiposikia sauti zo zote za binadamu watazua lugha yao wenyewe na hivyo kubainisha lugha asili ya binadamu.  Baada ya muda waliweza kuzungumza na neno la kwanza walilolitamka ni ‘bekos’ ambalo ni la lugha ya Phrygian lenye maana ya mkate.  Kwa hivyo iliamuliwa kuwa Phrygian ndiyo lugha asilia.

Utafiti mwingine uliofanywa na Mfalme James IV wa Scotland katika miaka ya 1500 BK ulionyesha kuwa watoto hao waliotengwa walizungumza Kiebrania.  Hivyo basi ilichukuliwa kwamba hii ndiyo iliyokuwa lugha asilia.

Naye Mswidi Andreas Kempe amependekeza kuwa Adamu alizungumza lugha ya Danish, nyoka – Kifaransa na Mungu – Kiswidi.  Naye Becanus J.G. katika karne ya 16 alidai kuwa Kijerumani ndiyo lugha ya asili na ilitumiwa na Mungu na Adamu huko Edeni.  Baadaye Mungu aliwawezesha watu kutafsiri Agano la Kale kutoka kwa Kijerumani hadi kwa Kiebrania.

Maoni haya ya kidini hayana ithibati tosha za utafiti wa kisayansi; yanategemea imani ambayo haina msingi katika mahitimisho ya kisayansi.  Kwa hivyo msimamo huu wa kidini hauna mashiko.

Zoezi:

1.       Toa maoni yako kuhusu nadharia za kidini za asili ya lugha.
2.       Tathmini nadharia hizi za kidini.

Nadharia za Kimazingira

Nadharia hizi zina uyakinifu kwa kiwango fulani.  Zinadai kuwa kadri mwanadamu alivyoishi na wanadamu wengine ndivyo hali ya kutegemeana ilivyodhihirika.  Na kwa kuwa wanadamu hutegemeana, basi lazima wawasiliane.  Kwa hivyo wanadamu wakajifunza lugha na lugha ikawa chombo muhimu cha mawasiliano yao.  Nadharia hizi zinaonyesha kuwa lugha ilitokana na mazingira, yaani maingiliano ya binadamu na mazingira yake.  Kuna nadharia kadha wa kadha zinazoelezea hali hii.

1.  Nadharia ya “Bow-wow”
Inatuhumiwa kwamba lugha ya binadamu imechipuka kutoka kwa sauti asilia zinazopatikana katika mazingira alimoishi binadamu.  Maneno ya kwanza ya lugha yalikuwa ni ya sauti alizozisikia binadamu.  Sauti hizi ni kama za miito ya wanyama, ndege, sauti za mito, na tufani.  Binadamu aliiga sauti alizozisikia.  Kwa mfano katika nadharia hii ya ‘bow-wow’, ambayo pia tungeiita ya tanakali sauti au kionomatopea, jina lake limetokana na mbweko wa mbwa.  Ni kweli kwamba lugha zote duniani zina maneno ya kionomatopea.

Ingawa maneno fulani katika lugha ni ya kionomatopea, ni vigumu kuelewa jinsi mambo ya kidhahania yatakavyoshughulikiwa na nadharia hii.

Zoezi:

1.       Andika maneno matano ya kionomatopea katika lugha ya Kiswahili.
2.       Orodhesha maneno matano ya kionomatopea katika lugha yako ya
Kwanza.
3.                        Mtoto mdogo huwa na msamiati mwingi wa kionomatopea.  Kisia jinsi
anavyoweza kuita wanyama hawa ikiwa bado hajaimudu ‘lugha nasibu’:
(a)  Ng’ombe _______________________________
b.       Mbuzi __________________________________
c.                   Paka ___________________________________
d.                   Kuku ___________________________________

2.  Nadharia ya ‘Pooh-pooh’
Imependekezwa kwamba maneno ya kwanza ya lugha yalitokana na milio ya kihisia kama uchungu, woga, mshangao, hasira na furaha.  Inasemekana kwamba binadamu alitumia lugha kama hii ili kudanganya.  Aligundua jinsi wenzake wanavyonyenyekea anapotoa ukelele wa hasira, kwa hivyo akaukuza mfumo huu wa mawasiliano ili kudhibiti mambo yake.  Akawa anajifanya amekasirika hata wakati hakukasirika.  Hivyo ndivyo uongo ulivyoanza.

Ni kweli kuwa katika lugha tuna sauti zinazodhihirisha hisia mbalimbali lakini hizi huwa si nyingi katika lugha.

Zoezi:

     Andika maneno au sauti kumi zinazodhihirisha hisia katika lugha ya
    Kiswahili.

3.  Nadharia ya ‘Ding-dong’
Sauti za lugha zimetokana na uhusiano uliopo baina ya ishara na sauti zinazotolewa.  Nadharia hii inashikilia kwamba miondoko na ishara vilitumiwa kama namna ya kuwasiliana hapo zamani.  Watu walitumia mwili, mikono na uso kuwasiliana.  Hasa walitumia ishara za mikono.  Lakini wakagundua kwamba hawawezi kutumia ishara hizi kwenye giza na pia pale ambapo mikono imeshika silaha.  Ikabidi wavumbue mfumo mwingine wa mawasiliano.  Zile ishara walizotoa kwa mikono zikaelekezwa kwenye ala za matamshi kama midomo na ulimi.  Kwa mfano, mwendo wa ulimi mtu anapotamka ‘bye-bye’ (kwaheri) huingiliana na kupatana na kupunga mkono unapomuaga mtu.  Nalo neno ‘mama’ hufanana na midomo inapokaribia matiti.

Swali:

   Ni ishara zipi tena zinazoingiliana na mwendo wa ala za matamshi?
Ukifikiria juu ya uzungumzaji bubu utaona uhusiano baina ya mwendo wa ala za sauti na miondoko iliyotumiwa kwa maana hiyo.  Miondoko na lugha huwa sawa utotoni, na huathiriwa kwa njia sawa ikiwa mtu amepata madhara ya ubongo.  Hata hivyo kuna aina mbalimbali za ujumbe tusioweza kuwasilisha kupitia kwa miondoko tu, kwa mfano, “Mjomba wangu anafikiri haonekani”.

Kumbuka:

·   Watu wanapozungumza hufanya miondoko mingi
    hasa ya mikono ili kusisitiza jambo.
·   Miondoko mingi hufafanua kilichozungumzwa.
·   Miondoko huiga umbo, mwendo au huwa na maana iliyojificha.   
·   Miondoko inapotangulia maneno huonyesha kuwa mzungumzaji
    anashindwa kupata maneno mwafaka haraka kuelezea dhana
    alizo nazo akilini.

4.  Nadharia ya ‘Yo-he-ho’
Hapa tunaelezwa kuwa chanzo cha lugha ni ile mighuno ya watu wengi waliofanya kazi pamoja.  Sauti zilizohusishwa na vitendo fulani zikawa majina ya vitendo hivyo.  Inasemekana kwamba sauti za watu wanaobeba vitu vizito, huku wakiongozwa namna ya kufanya kazi hiyo, ndiyo chanzo cha lugha.  Kikundi hiki cha watu huguna na kutoa sauti wanapobeba vitu hivyo vizito kama vile magogo na mizoga ya wanyama.

Ubora wa nadharia hii ni kuwa inayaweka maendeleo ya lugha ya binadamu katika muktadha wa kijamii.

Wanaopinga nadharia hii wanasema kwamba kwa muda mrefu wanyama wa familia ya nyani wamekuwa wakitoa miguno katika jamii zao lakini hawana uwezo wa kuzungumza.

Nadharia za Kisasa au Kisayansi

Nadharia hizi zinamulika biolojia kama msingi wa kuchipuka na kukua kwa lugha.  Zinaangalia vitu alivyo navyo binadamu katika maumbile yake ambavyo wanyama hawana vinavyomwezesha kutumia lugha.

Inasemekana kwamba mtu katika hali yake ya mwanzo hakupishana na wanyama wengine.  Aliishi mtini na akaenda kwa mikono na miguu.  Wakati fulani, kutokana na mabadiliko ya kimazingira, mtu alilazimika kusimama wima na kwenda kwa miguu miwili.  Mikono ikawa huru kufanyia kazi nyingine.  Ubongo wa binadamu ukakua zaidi.  Mabadiliko haya yalileta tofauti kubwa kati ya binadamu na wanyama wengine.

Wataalamu wanaamini kwamba maendeleo ya lugha yanahusiana na mabadiliko ya kimaumbile ya binadamu.  Wanaona kuwa binadamu amezaliwa na uwezo wa kufahamu lugha, uwezo ulio katika akili yake, ambao wanyama hawana.

Binadamu amepitia mabadiliko mbalimbali.  Kufikia mwaka 60,000 KK fuvu la sokwe lilikuwa tofauti na lile la binadamu katika hatua ya Neanderthal.  Ala za sauti katika binadamu ziliumbika kwa njia ambayo angeweza kutamka sauti za konsonanti.  Kufikia mwaka 35,000 KK binadamu akawa kama tunavyomfahamu leo – homo sapien.  Katika mabadiliko haya binadamu alipata sifa zinazomwezesha kuzungumza.  Sifa hizi ni:
(a)  Meno yake yamesimama wima, hayajapinda nje kama yale ya wanyama
      wengine.  Sifa hii si muhimu katika kula ila katika kutoa sauti kama f, v, th.
(b)  Midomo ya binadamu ina misuli mingi kuliko ilivyo katika wanyama wengine.  
       Hili humwezesha binadamu kuitembeza kwa urahisi hasa anapotoa sauti p,
       b, w.
(c)  Kinywa cha binadamu ni kidogo na kinaweza kikafunguliwa na kufungwa
      kwa haraka.  Pia humo kinywani kuna ulimi unaoweza kupindwa kwa njia
      tofauti ili kutoa sauti mbalimbali.
(d)  Nyuzi za sauti katika binadamu ziko chini zikilinganishwa na za wanyama
kama nyani. Ziliteremka kwa sababu ya umbile la wima alilolipata binadamu. Hali hii ilisababisha koromeo, iliyo juu ya nyuzi za sauti, kuwa ndefu na kuvumisha sauti.
(e)  Ubongo wa binadamu umegawanywa, kila sehemu ikiwa na kazi maalumu.  
      Dhima kama za matumizi ya lugha, uchanganuzi, na matumizi ya vifaa
      huongozwa na upande wa kushoto wa ubongo.

Muhtasari:

Katika somo hili nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza asili ya lugha zimetolewa.  Kila moja ya nadharia hizo ina upungufu wake na ubora wake.  Hata hivyo nadharia ya kisayansi iliyojengwa kwenye misingi ya maendeleo na mabadiliko ya binadamu yaliyomwezesha kutumia lugha ndiyo yenye uzito zaidi.  Ni vizuri kutahadharisha kuwa bado utafiti unafanywa kuhusu jambo hili ili ukweli upatikane.

Maswali:
  1.  Ukweli kwamba watoto wote duniani hujifunza lugha kwa namna
       moja unatufahamisha nini kuhusu asili ya lugha?
  2.  “Hakuna nadharia inayoweza kueleza kikamilifu asili ya lugha.”
       Fafanua.

 Marejeleo:
 
1.       Aitchison, J. (1976), The Articulate Mammal,  London: Hutchison Union.
2.       Fromkin, V. na Rodman, B. (1988), An Introduction to Language,  Fort
             Worth, Holt Rinehart and Winston Inc.
3.                   Harnad, S.R. et.al. (1975), Origin and Evolution of Language and Speech,  
                 New York  The New York Academy.
4.  Vema, S.K. & Krishnaswamy, N. (1989), Modern Linguistics: An
                     Introduction, New Delhi,  Oxford University Press.
5.                   Yule, G. (1996), The Study of Language,  Cambridge, Cambridge University
                  Press.
SOMO LA NANE

SIFA BIA ZA LUGHA


Utangulizi

Kuna sifa za kilimwengu ambazo hupatikana katika lugha zote. Kwa mfano, mtoto anapozaliwa huwa na kipawa cha kumiliki muundo wa lugha yoyote.  Kipawa hiki hudhihirika tu pale mtoto anapokabiliwa na mazingira kunapozungumzwa lugha fulani. Bila mazingira haya kipawa hiki hakiwezi kujitokeza. Ikiwa basi binadamu anaweza kujifunza lugha yoyote ulimwenguni, inaonekana kuwa kuna muundo maalumu katika bongo za binadamu ambao hungojea mpaka mazingira mnamozungumzwa lugha kuibuka.

Katika somo hili tutafafanua sifa bia hizi za lugha, yaani sifa zinazopatikana  katika lugha zote za binadamu.  Hizi ndizo sifa tunazotumia kuamua kama lugha ni chombo cha binadamu pekee au hata wanyama wanaweza kuitumia.
Malengo:

Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutaja sifa bia za lugha.
·         Kufafanua maana ya kila mojawapo ya sifa bia hizo.
·         Kutoa uamuzi unaoweza kuthibitishwa kwa hoja madhubuti, kama lugha ni chombo cha binadamu pekee.
   

Mtaalamu Hockett (1958) katika kitabu chake A Course in General Linguistics ameorodhesha sifa bia za lugha kumi na sita.  Hapa kuna baadhi ya sifa hizo:
1.       Uwili
2.       Uzalishaji
3.       Unasibu
4.       Uhamishaji
5.       Umakinikaji
6.       Ubadilishaji
7.       Uwasilishaji kiutamaduni
8.       Kuongopa
Hebu sasa tuzifafanue kila mojawapo ya sifa bia hizi.

1.    Uwili
Hii ina maana kwamba lugha ya binadamu imepangwa katika safu mbili: sauti na maana.  Vipashio vya sauti kama K A T A havina maana.  Vinapata tu maana vinapounganishwa na kuwa KATA.  Kwa njia hii lugha inapata iktisadi kwa sababu vipashio tofauti vya sauti huwekwa pamoja kuleta maana, na vipashio hivyo vya maana huwekwa pamoja kuunda sentensi.  Hakuna mfumo wa mawasiliano ya wanyama ulio na uwili.

Kwa mfano, mbwa anapobweka huwezi kuchanganua mbweko huo katika vipashio vidogo vya sauti na maana.  Hata hivyo, inasemekana kuwa uwili hupatikana katika miluzi au nyimbo za ndege wachache ambapo kila sauti moja haina maana lakini muungano wa sauti hizo huleta maana.

2.    Uzalishaji/Ubunifu
Dhana ya uzalishaji inaelezwa pia kama ubunifu.  Hii ina maana kwamba lugha humwezesha binadamu kutoa kauli ambazo hazijawahi kutamkwa tena na pia kuelewa kauli mpya.  Binadamu anaweza kuzungumza juu ya kitu chochote apendacho bila utata wowote wa kueleweka.  Anaweza kuzungumzia mambo rahisi pamoja na ya kidhahania.  Mambo mapya yanapotokea kama teknolojia anabuni maneno ya kusimamia dhana hizo.

Pia ingawa lugha ya binadamu ina idadi maalum ya maneno, anaweza  kutunga sentensi  nyingi zisizo  kikomo kujieleza. Harudii sentensi zile zile au maneno yale yale kila wakati.  Kuna miktadha michache tu katika maisha ya binadamu ambapo maongezi yanafuata kaida fulani.  Kwa mfano, salamu na kutoa rambirambi mtu akifa.  

Kwa upande mwingine, wanyama wana idadi maalum ya ishara wanazotumia kutoa ujumbe.  Ujumbe huo unatolewa kwa njia zisizo wazi.  
Kwa mfano, ng’ombe akihisi njaa, akimtaka ndama wake, akichoka na kadhalika, atatoa sauti moja tu  -  ‘moooo’.  Inasemekana kuwa tumbili huwa na sauti 36 tu.  Sauti hizi zote hazitumiwi kwa mawasiliano.
 Swali:



Tofauti na binadamu, utagundua kuwa wanyama hawana au wana ubunifu mdogo sana katika sauti wanazotoa.  Kwa mfano, ndege wote wana sauti maalum tu wanazotoa.  Hata hivyo, densi ya nyuki ina kiwango fulani cha uzalishaji kwa sababu inaweza kutumika kuwasiliana juu ya nekta iliyo upande wo wote na maili kadha kutoka kwa mzinga.


Lakini kumbuka kuwa nyuki hawezi kuwasiliana juu ya watu, wanyama, matarajio  yake au kushindwa kwake.  Aidha, nyuki wanaweza kuwasiliana tu juu ya kitu kilicho masafa fulani mbali lakini hawana dhana ya ‘juu’.  Kwa hivyo ni wazi kuwa wanyama hawawezi kubuni sauti mpya kuelezea hali ngeni wanayokumbana nayo.
Kumbuka:

       
Swali:

3.    Unasibu
Hii ni sifa bia nyingine.  Lugha ya binadamu hutumia ishara ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachorejelewa. Hakuna uhusiano kati ya neno ‘mbwa’ na yule mnyama anayerejelewa na jina hili.  Angeweza pia kuitwa:
    un chien     -    Kifaransa
    ein hund    -    Kijerumani   
    canis        -    Kilatini
    esese        -    Kikuria
Hata anapoitwa kwa majina haya mengine tunatambua kwamba ni jina tu linalobadilika, yeye anabakia yule yule.
Hata hivyo, tunajua kuwa kuna maneno machache katika lugha yanayozingatia uhusiano wa moja kwa  moja kati ya kitaja na kitajwa.  Maneno haya ni kama ‘filimbi’, ‘pikipiki’, ‘kuku’ na ‘tingatinga’.
Zoezi:

Taja maneno mengine kumi ya kionomatopea katika lugha ya Kiswahili

Katika mawasiliano ya wanyama kuna uhusiano mkubwa kati ya ishara wanazotumia na ujumbe wanaotoa.  Kwa mfano, mbwa akitaka kukutisha atatoa mlio wa kutisha na akenue meno yake.  Paka aliye tayari kushambulia atarefusha makucha yake.  Ikiwa paka huyo anataka kuonyesha urafiki atajisugua kwenye mguu wako.  Hata densi ya nyuki huwa na uhusiano wa moja kwa moja na mahali nekta ilipo.

Hata hivyo, sifa hii ya unasibu inapatikana katika mawasiliano ya wanyama fulani.  Shakwe huonyesha kuwa yuko tayari kushambulia adui kwa kupinduka na kumpa adui mgongo huku aking’oa nyasi.

Swali:

Je, unafikiri unasibu ulio katika lugha ya binadamu unaweza kulinganishwa na huo uliotajwa hapo juu katika kitendo cha shakwe?

4.    Uhamishaji
Ukitaka kuwasiliana na mnyama unayefuga kwako  nyumbani utagundua kwamba utafanikiwa kwa kiasi fulani tu.  Mnaweza kuelewana kulingana na muktadha wa wakati huo, lakini huwezi kumwuliza mambo yaliyofanyika jana au yatakayofanyika.  Inaonekana kuwa mawasiliano ya wanyama huwa ya papo hapo.  Hawawezi kuwasiliana juu ya mambo yaliyopita, yajayo au yasiyoonekana wakati huo.

Sifa hii inaonyesha kuwa lugha ya binadamu humpa uwezo wa kuzungumza juu ya vitu ambavyo havioni.  Anaweza kujadili juu ya mambo yaliyotokea wakati uliopita, sasa na wakati ujao.  Kwa mfano, binadamu anaweza kusema: Mwalimu wangu wa zamani, Bwana Tumbo, anayesihi Uganda, alivunjika mkono wake miaka miwili iliyopita.  Ni vigumu kwa wanyama kutoa ujumbe kama huu.  Kwa mfano, kuku huita vifaranga apatapo chakula, hawezi kuwaeleza vifaranga juu ya chakula alichokula mwaka jana.
Zoezi:
Je, hali hizi zinaonyesha uhamishaji au la?
a.                   Ndege ataendelea kutoa kilio hata baada ya paka aliyekuwa akimvizia kuondoka.
b.                   Kuku atazidi kutoa sauti za tahadhari hata baada ya ruhange aliyekuwa akimvizia kuondoka.
c.                   Ukizoea kumrushia mbwa fulani mawe, kila anapokuona atatoroka.

Wataalmu wanaeleza kwamba mawasiliano ya nyuki yana kiwango fulani cha uhamishaji.  Nyuki hueleza kuwa wamepata nekta wakiwa wameshatoka palipo na nekta hiyo, lakini lazima wawasiliane mara moja warudipo kwenye mzinga.  Hawawezi kudensi juu ya nekta waliyopata mwaka jana au watakayopata mwaka ujao.  Kwa hivyo, inaonekana kuwa sifa hii ya uhamishaji huipambanua lugha ya binadamu na mawasiliano ya wanyama.

5.    Umakinikaji
Hii ina maana kwamba wale wanaowasiliana wasizame zaidi katika kitendo hicho.  Wasiache kile wanachofanya ili kuwasiliana.  Binadamu wanaweza kuzungumza huku wakishughulika na vitendo vingine visivyohusiana na mada ya mazungumzo.  Si lazima waache wanachofanya ili kujibu waliloulizwa.  Lakini nyuki anaposhiriki katika ile densi yake anajihusisha kikamilifu katika mawasiliano hayo.

6.    Ubadilishaji
Binadamu anaweza kuwa mtoaji na mpokeaji ujumbe.  Mtu mmoja hutuma ujumbe na mwingine huupokea.  Mfumo wa mawasiliano wa nyani na nyuki una sifa hii, lakini ule wa wanyama wengine hauna.  Kwa mfano, baadhi ya ndege dume huwa na wito ambao ni tofauti na ule wa ndege jike.  Pia kuna aina ya samaki walio na namna za mawasiliano yanayopatikana katika nke au dume tu.

7.    Uwasilishaji Kiutamaduni
Lugha ya binadamu hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.  Hii ina maana kwamba inabidi kila mzungumzaji wa lugha ajifunze mfumo wa lugha yake.  Binadamu ana kipawa cha kujifunza lugha lakini mnyama huzaliwa na milio anayotoa kisilka.

Kumbuka:



Binadamu atarithi rangi, sura, na hata urefu kutoka kwa wazazi wake lakini hawezi kurithi lugha.  Anajifunza lugha kutokana na utamaduni aliomo.

Mifumo ya mawasiliano ya wanyama huwasilishwa kibiolojia hivi kwamba ng’ombe wote duniani hutoa sauti sawa, kama ilivyo kwa kuku na mbuzi.  Wao huongozwa na silka.  Mtoto wa binadamu akikuzwa katika upweke, hatakuwa na lugha; lakini wanyama wakikuzwa katika upweke bado watatoa milio ya wanyama wa aina yao.

8.    Kuongopa
Kuongopa ni kudanganya.  Lugha inaweza kutumiwa kusema uongo au kuelezea mambo  yasiyo ya kweli au kuzungumzia mambo ya upuzi.  Kwa mfano, mtu anaweza kusema kuwa kutoka duniani hadi mwezini ni maili kumi au kuwa vitu vyote vigumu huwa na rangi ya kijani hadi vinapopatwa na miale ya jua.

Sifa hii hutegemea sifa zingine kama uhamishaji, ubunifu, na usemantiki.  Bila usemantiki, hatuwezi kutathmini ujumbe ili kuona kama una uhalali na ukweli.  Bila uhamishaji, tutazungumzia tu hali zilizopo kwenye muktadha, hivi kwamba itakuwa vigumu kudanganya.  Bila ubunifu, ni vigumu kuwa na mazungumzo ya upuzi, ingawa unaweza kudanganya.

Wataalamu  wamesema kwamba hata wanyama wana kiasi fulani cha kudanganya.  Hapa kuna mifano:
a.                   Jogoo anapotaka kufanya mapenzi hutoa sauti fulani na ishara kama ya kumwitia kuku jike chakula ili akimkaribia ‘amshike’.
b.                   Chatu hutoa sauti  kama ya mbuzi au swala ili wanyama hao wakimkaribia awashike.
c.                   Kuna wadudu ambao wakiguswa na adui mwenye nguvu kuwashinda wanajilaza chali na kujifanya wamekufa.
d.                   Mmea wa kifauongo hujikunja na kujifanya umenyauka unapoguswa.
Zoezi:

1.     Toa mifano mingine mitano ya hali ambazo wanyama au mimea
        hudanganya.

2.     Eleza tofauti zinazotenganisha lugha ya mwanadamu na mawasiliano   
        ya wanyama.

Muhtasari:


Katika somo hili tumezungumzia sifa bia za lugha.  Tumepitia sifa bia zifuatazo: uwili, uzalishaji, unasibu, uhamishaji, umakinikaji, ubadilishaji, uwasilishaji kiutamaduni, na kuongopa.  Kuna sifa zingine nane ambazo hazikupitiwa kukiwemo ubayana wa vipashio, usemantiki, urejeaji, na kufifia haraka.  Mwanafunzi anashauriwa kujisomea sifa bia hizo nyingine.

Swali la kuuliza katika hitimisho hili ni kwamba:  Je, wanyama wanaweza kuzungumza kama binadamu? Ili wanyama waweze kuzungumza kama binadamu lazima wawe na sifa bia zote zilizojadiliwa katika somo hili.  Jibu lake ni ‘hapana’. Kutokana  na mjadala uliomo katika somo hili imedhihirika kuwa hakuna mfumo wa mawasiliano ya wanyama ulio na sifa bia zote zilizotajwa.  Sifa bia zilizopatikana katika mawasiliano ya wanyama ni za kiwango cha chini sana zikilinganishwa na zile alizo nazo binadamu.  Basi tunaweza kusema kuwa lugha ni chombo au sifa ya binadamu pekee.

        Maelezo ya dhana:


Iktisadi    -    Hiki ni kigezo cha  isimu kinachohitaji
                             uchanganuzi ulenge katika kutumia vipashio     
                             vichache zaidi kadri iwezekanavyo.

                Marejeleo:

Hockett, C.A. (1958), A Course in Modern Linguistics, New York:
                              Macmillan.

Yule, G. (1996), The Study of Language, Cambridge,  Cambridge
                       University Press

SOMO LA NANE

SIFA BIA ZA LUGHA


Utangulizi

Kuna sifa za kilimwengu ambazo hupatikana katika lugha zote. Kwa mfano, mtoto anapozaliwa huwa na kipawa cha kumiliki muundo wa lugha yoyote.  Kipawa hiki hudhihirika tu pale mtoto anapokabiliwa na mazingira kunapozungumzwa lugha fulani. Bila mazingira haya kipawa hiki hakiwezi kujitokeza. Ikiwa basi binadamu anaweza kujifunza lugha yoyote ulimwenguni, inaonekana kuwa kuna muundo maalumu katika bongo za binadamu ambao hungojea mpaka mazingira mnamozungumzwa lugha kuibuka.

Katika somo hili tutafafanua sifa bia hizi za lugha, yaani sifa zinazopatikana  katika lugha zote za binadamu.  Hizi ndizo sifa tunazotumia kuamua kama lugha ni chombo cha binadamu pekee au hata wanyama wanaweza kuitumia.
Malengo:

Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutaja sifa bia za lugha.
·         Kufafanua maana ya kila mojawapo ya sifa bia hizo.
·         Kutoa uamuzi unaoweza kuthibitishwa kwa hoja madhubuti, kama lugha ni chombo cha binadamu pekee.
   

Mtaalamu Hockett (1958) katika kitabu chake A Course in General Linguistics ameorodhesha sifa bia za lugha kumi na sita.  Hapa kuna baadhi ya sifa hizo:
9.                   Uwili
10.               Uzalishaji
11.               Unasibu
12.               Uhamishaji
13.               Umakinikaji
14.               Ubadilishaji
15.               Uwasilishaji kiutamaduni
16.               Kuongopa
Hebu sasa tuzifafanue kila mojawapo ya sifa bia hizi.

1.    Uwili
Hii ina maana kwamba lugha ya binadamu imepangwa katika safu mbili: sauti na maana.  Vipashio vya sauti kama K A T A havina maana.  Vinapata tu maana vinapounganishwa na kuwa KATA.  Kwa njia hii lugha inapata iktisadi kwa sababu vipashio tofauti vya sauti huwekwa pamoja kuleta maana, na vipashio hivyo vya maana huwekwa pamoja kuunda sentensi.  Hakuna mfumo wa mawasiliano ya wanyama ulio na uwili.

Kwa mfano, mbwa anapobweka huwezi kuchanganua mbweko huo katika vipashio vidogo vya sauti na maana.  Hata hivyo, inasemekana kuwa uwili hupatikana katika miluzi au nyimbo za ndege wachache ambapo kila sauti moja haina maana lakini muungano wa sauti hizo huleta maana.

2.    Uzalishaji/Ubunifu
Dhana ya uzalishaji inaelezwa pia kama ubunifu.  Hii ina maana kwamba lugha humwezesha binadamu kutoa kauli ambazo hazijawahi kutamkwa tena na pia kuelewa kauli mpya.  Binadamu anaweza kuzungumza juu ya kitu chochote apendacho bila utata wowote wa kueleweka.  Anaweza kuzungumzia mambo rahisi pamoja na ya kidhahania.  Mambo mapya yanapotokea kama teknolojia anabuni maneno ya kusimamia dhana hizo.

Pia ingawa lugha ya binadamu ina idadi maalum ya maneno, anaweza  kutunga sentensi  nyingi zisizo  kikomo kujieleza. Harudii sentensi zile zile au maneno yale yale kila wakati.  Kuna miktadha michache tu katika maisha ya binadamu ambapo maongezi yanafuata kaida fulani.  Kwa mfano, salamu na kutoa rambirambi mtu akifa.  

Kwa upande mwingine, wanyama wana idadi maalum ya ishara wanazotumia kutoa ujumbe.  Ujumbe huo unatolewa kwa njia zisizo wazi.  
Kwa mfano, ng’ombe akihisi njaa, akimtaka ndama wake, akichoka na kadhalika, atatoa sauti moja tu  -  ‘moooo’.  Inasemekana kuwa tumbili huwa na sauti 36 tu.  Sauti hizi zote hazitumiwi kwa mawasiliano.
 Swali:



Tofauti na binadamu, utagundua kuwa wanyama hawana au wana ubunifu mdogo sana katika sauti wanazotoa.  Kwa mfano, ndege wote wana sauti maalum tu wanazotoa.  Hata hivyo, densi ya nyuki ina kiwango fulani cha uzalishaji kwa sababu inaweza kutumika kuwasiliana juu ya nekta iliyo upande wo wote na maili kadha kutoka kwa mzinga.


Lakini kumbuka kuwa nyuki hawezi kuwasiliana juu ya watu, wanyama, matarajio  yake au kushindwa kwake.  Aidha, nyuki wanaweza kuwasiliana tu juu ya kitu kilicho masafa fulani mbali lakini hawana dhana ya ‘juu’.  Kwa hivyo ni wazi kuwa wanyama hawawezi kubuni sauti mpya kuelezea hali ngeni wanayokumbana nayo.
Kumbuka:

       
Swali:

3.    Unasibu
Hii ni sifa bia nyingine.  Lugha ya binadamu hutumia ishara ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachorejelewa. Hakuna uhusiano kati ya neno ‘mbwa’ na yule mnyama anayerejelewa na jina hili.  Angeweza pia kuitwa:
    un chien     -    Kifaransa
    ein hund    -    Kijerumani   
    canis        -    Kilatini
    esese        -    Kikuria
Hata anapoitwa kwa majina haya mengine tunatambua kwamba ni jina tu linalobadilika, yeye anabakia yule yule.
Hata hivyo, tunajua kuwa kuna maneno machache katika lugha yanayozingatia uhusiano wa moja kwa  moja kati ya kitaja na kitajwa.  Maneno haya ni kama ‘filimbi’, ‘pikipiki’, ‘kuku’ na ‘tingatinga’.
Zoezi:

Taja maneno mengine kumi ya kionomatopea katika lugha ya Kiswahili

Katika mawasiliano ya wanyama kuna uhusiano mkubwa kati ya ishara wanazotumia na ujumbe wanaotoa.  Kwa mfano, mbwa akitaka kukutisha atatoa mlio wa kutisha na akenue meno yake.  Paka aliye tayari kushambulia atarefusha makucha yake.  Ikiwa paka huyo anataka kuonyesha urafiki atajisugua kwenye mguu wako.  Hata densi ya nyuki huwa na uhusiano wa moja kwa moja na mahali nekta ilipo.

Hata hivyo, sifa hii ya unasibu inapatikana katika mawasiliano ya wanyama fulani.  Shakwe huonyesha kuwa yuko tayari kushambulia adui kwa kupinduka na kumpa adui mgongo huku aking’oa nyasi.

Swali:

Je, unafikiri unasibu ulio katika lugha ya binadamu unaweza kulinganishwa na huo uliotajwa hapo juu katika kitendo cha shakwe?

4.    Uhamishaji
Ukitaka kuwasiliana na mnyama unayefuga kwako  nyumbani utagundua kwamba utafanikiwa kwa kiasi fulani tu.  Mnaweza kuelewana kulingana na muktadha wa wakati huo, lakini huwezi kumwuliza mambo yaliyofanyika jana au yatakayofanyika.  Inaonekana kuwa mawasiliano ya wanyama huwa ya papo hapo.  Hawawezi kuwasiliana juu ya mambo yaliyopita, yajayo au yasiyoonekana wakati huo.

Sifa hii inaonyesha kuwa lugha ya binadamu humpa uwezo wa kuzungumza juu ya vitu ambavyo havioni.  Anaweza kujadili juu ya mambo yaliyotokea wakati uliopita, sasa na wakati ujao.  Kwa mfano, binadamu anaweza kusema: Mwalimu wangu wa zamani, Bwana Tumbo, anayesihi Uganda, alivunjika mkono wake miaka miwili iliyopita.  Ni vigumu kwa wanyama kutoa ujumbe kama huu.  Kwa mfano, kuku huita vifaranga apatapo chakula, hawezi kuwaeleza vifaranga juu ya chakula alichokula mwaka jana.
Zoezi:
Je, hali hizi zinaonyesha uhamishaji au la?
d.       Ndege ataendelea kutoa kilio hata baada ya paka aliyekuwa akimvizia kuondoka.
e.                   Kuku atazidi kutoa sauti za tahadhari hata baada ya ruhange aliyekuwa akimvizia kuondoka.
f.                    Ukizoea kumrushia mbwa fulani mawe, kila anapokuona atatoroka.

Wataalmu wanaeleza kwamba mawasiliano ya nyuki yana kiwango fulani cha uhamishaji.  Nyuki hueleza kuwa wamepata nekta wakiwa wameshatoka palipo na nekta hiyo, lakini lazima wawasiliane mara moja warudipo kwenye mzinga.  Hawawezi kudensi juu ya nekta waliyopata mwaka jana au watakayopata mwaka ujao.  Kwa hivyo, inaonekana kuwa sifa hii ya uhamishaji huipambanua lugha ya binadamu na mawasiliano ya wanyama.

5.    Umakinikaji
Hii ina maana kwamba wale wanaowasiliana wasizame zaidi katika kitendo hicho.  Wasiache kile wanachofanya ili kuwasiliana.  Binadamu wanaweza kuzungumza huku wakishughulika na vitendo vingine visivyohusiana na mada ya mazungumzo.  Si lazima waache wanachofanya ili kujibu waliloulizwa.  Lakini nyuki anaposhiriki katika ile densi yake anajihusisha kikamilifu katika mawasiliano hayo.

6.    Ubadilishaji
Binadamu anaweza kuwa mtoaji na mpokeaji ujumbe.  Mtu mmoja hutuma ujumbe na mwingine huupokea.  Mfumo wa mawasiliano wa nyani na nyuki una sifa hii, lakini ule wa wanyama wengine hauna.  Kwa mfano, baadhi ya ndege dume huwa na wito ambao ni tofauti na ule wa ndege jike.  Pia kuna aina ya samaki walio na namna za mawasiliano yanayopatikana katika nke au dume tu.

7.    Uwasilishaji Kiutamaduni
Lugha ya binadamu hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.  Hii ina maana kwamba inabidi kila mzungumzaji wa lugha ajifunze mfumo wa lugha yake.  Binadamu ana kipawa cha kujifunza lugha lakini mnyama huzaliwa na milio anayotoa kisilka.

Kumbuka:



Binadamu atarithi rangi, sura, na hata urefu kutoka kwa wazazi wake lakini hawezi kurithi lugha.  Anajifunza lugha kutokana na utamaduni aliomo.

Mifumo ya mawasiliano ya wanyama huwasilishwa kibiolojia hivi kwamba ng’ombe wote duniani hutoa sauti sawa, kama ilivyo kwa kuku na mbuzi.  Wao huongozwa na silka.  Mtoto wa binadamu akikuzwa katika upweke, hatakuwa na lugha; lakini wanyama wakikuzwa katika upweke bado watatoa milio ya wanyama wa aina yao.

8.    Kuongopa
Kuongopa ni kudanganya.  Lugha inaweza kutumiwa kusema uongo au kuelezea mambo  yasiyo ya kweli au kuzungumzia mambo ya upuzi.  Kwa mfano, mtu anaweza kusema kuwa kutoka duniani hadi mwezini ni maili kumi au kuwa vitu vyote vigumu huwa na rangi ya kijani hadi vinapopatwa na miale ya jua.

Sifa hii hutegemea sifa zingine kama uhamishaji, ubunifu, na usemantiki.  Bila usemantiki, hatuwezi kutathmini ujumbe ili kuona kama una uhalali na ukweli.  Bila uhamishaji, tutazungumzia tu hali zilizopo kwenye muktadha, hivi kwamba itakuwa vigumu kudanganya.  Bila ubunifu, ni vigumu kuwa na mazungumzo ya upuzi, ingawa unaweza kudanganya.

Wataalamu  wamesema kwamba hata wanyama wana kiasi fulani cha kudanganya.  Hapa kuna mifano:
e.       Jogoo anapotaka kufanya mapenzi hutoa sauti fulani na ishara kama ya kumwitia kuku jike chakula ili akimkaribia ‘amshike’.
f.                    Chatu hutoa sauti  kama ya mbuzi au swala ili wanyama hao wakimkaribia awashike.
g.                   Kuna wadudu ambao wakiguswa na adui mwenye nguvu kuwashinda wanajilaza chali na kujifanya wamekufa.
h.                   Mmea wa kifauongo hujikunja na kujifanya umenyauka unapoguswa.
Zoezi:

1.     Toa mifano mingine mitano ya hali ambazo wanyama au mimea
        hudanganya.

2.     Eleza tofauti zinazotenganisha lugha ya mwanadamu na mawasiliano   
        ya wanyama.

Muhtasari:


Katika somo hili tumezungumzia sifa bia za lugha.  Tumepitia sifa bia zifuatazo: uwili, uzalishaji, unasibu, uhamishaji, umakinikaji, ubadilishaji, uwasilishaji kiutamaduni, na kuongopa.  Kuna sifa zingine nane ambazo hazikupitiwa kukiwemo ubayana wa vipashio, usemantiki, urejeaji, na kufifia haraka.  Mwanafunzi anashauriwa kujisomea sifa bia hizo nyingine.

Swali la kuuliza katika hitimisho hili ni kwamba:  Je, wanyama wanaweza kuzungumza kama binadamu? Ili wanyama waweze kuzungumza kama binadamu lazima wawe na sifa bia zote zilizojadiliwa katika somo hili.  Jibu lake ni ‘hapana’. Kutokana  na mjadala uliomo katika somo hili imedhihirika kuwa hakuna mfumo wa mawasiliano ya wanyama ulio na sifa bia zote zilizotajwa.  Sifa bia zilizopatikana katika mawasiliano ya wanyama ni za kiwango cha chini sana zikilinganishwa na zile alizo nazo binadamu.  Basi tunaweza kusema kuwa lugha ni chombo au sifa ya binadamu pekee.

        Maelezo ya dhana:


Iktisadi    -    Hiki ni kigezo cha  isimu kinachohitaji
                             uchanganuzi ulenge katika kutumia vipashio     
                             vichache zaidi kadri iwezekanavyo.

                Marejeleo:

Hockett, C.A. (1958), A Course in Modern Linguistics, New York:
                              Macmillan.

Yule, G. (1996), The Study of Language, Cambridge,  Cambridge
                       University Press

SOMO LA TISA

AINA ZA LUGHA NA KAZI ZA LUGHA

Utangulizi

Katika somo la nane tuliangalia sifa bia za lugha kwa lengo la kuthibitisha kuwa lugha zote ulimwenguni zina sifa sawa.  Katika somo hili, tumeigawa mada yetu katika sehemu mbili.  Sehemu ya kwanza itachunguza aina za lugha kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ambavyo hutumiwa kuweka lugha kwenye makundi mbalimbali.  Sehemu ya pili itachunguza kazi za lugha katika jamii.
Malengo:


Baada ya somo hili utaweza:
·         Kueleza aina mbalimbali za lugha kwa kutumia kigezo cha uamilifu.
·         Kubainisha kazi mbalimbali za lugha katika jamii.


I.   Aina za Lugha

Lugha huweza kuainishwa katika makundi mbalimbali.  Kazi hii hufanywa na wataalamu wa Isimu-linganishi.  Katika kuainisha lugha hizi vigezo vinne hutumiwa.  Vigezo hivi ni:
i.                        nasaba
ii.                        muundo
iii.                        eneo la kijiografia
iv.                        uamilifu
Kila kigezo kinachotumika huweza kutenga lugha za ulimwengu kwenye makundi tofauti tofauti.  
Katika somo hili tutaziainisha lugha kwa kutumia kigezo cha uamilifu. Hii haimaanishi kuwa kigezo hiki ndicho muhimu kuliko vyote. La! Sababu ni kuwa kigezo hiki ndicho kinachofaa kutolewa katika awamu hii ya kwanza ya masomo yetu.

Uainishaji Kiuamilifu

Tunapozungumza juu ya uamilifu wa kitu, huwa tunaangalia kazi ya kitu hicho.  Kwa hivyo, tunapoangalia uamilifu wa lugha tunazingatia kazi au majukumu ya lugha hizo katika jamii.  Wataalamu wamezipa lugha majina mbalimbali kulingana na namna lugha hizo zinavyotumika katika jamii.

Hebu basi tuzieleze lugha hizi:
1.    Lugha mame
Hii ni lugha ambayo bado imo katika umbo lake la awali.  Lugha –mame ni lugha ambayo inatuhumiwa kuwa lugha nyingine zimechipuka kutokana nayo.  Lugha zote zinazotokana na lugha hiyo zinakuwa ni za “familia ya lugha” hiyo.  Hivyo basi lugha hizi zinakuwa na uhusiano wa ‘kidugu’ kama walivyo ndugu au dada wanaohusiana kutokana na mzazi mmoja.

Kila lugha baadaye hubadilika kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki. (Taz. somo la nne kwa maelezo zaidi ya viwango hivi).  Hata hivyo lugha katika familia hiyo hubaki kuwa lugha za asili moja na lugha hizi huwa zina uhusiano mkubwa.  Kwa mfano, lugha ya Kiingereza, Kijerumani, Kideni (Danish), lugha za Kiseltiki, lugha za Kibalto-Slavoni, Kiromansi, lugha za Kihindi – ki-iran, Kigriki, Kialbania na Kiarmenia, hizi zote zinachukuliwa kuwa zimetokana na familia moja ya lugha za Ulaya na za Kihindi (Indo-European languages).

Tutatumia mchoro kuonyesha uhusiano wa lugha za Ulaya na za Kihindi.
           


Lugha mame


           Kiwelsh       Kifaransa    Kihindi      Kichina
Kiingereza  Kijerumani

Katika mchoro huu tunaona kuwa Kingereza kiinakaribiana sana na Kijerumani na kiko mbali kidogo na lugha ya Kiwelsh na Kifaransa na hata Kihindi.  Lugha ya Kichina iko mbali na mchoro ili kuonyesha kuwa haina uhusiano wowote na lugha hizo nyingine.  Umuhimu wa kielelezo au mchoro huu kwa wanaisimu – historia  ni kwamba huwasaidia kuonyesha wazi uhusiano wa kihistoria uliopo katika lugha hizi.

Mfano mwingine ni wa familia ya lugha za mame-Bantu.  Hiki ni Kibantu ‘kilichozaa’ lugha mbalimbali ambazo zimewekwa kwenye kikundi cha Kibantu.  Hizi ni lugha zenye  asili moja  kihistoria zilizoko kusini mwa ikweta katika bara la Afrika.  Lugha ya Kiswahili, kwa mfano, ilikuwa na umbo lake la awali.  Kiswahili hicho cha awali huitwa Kingozi.  Hivyo basi Kiswahili kina usuli wake katika familia ya lugha za Kibantu.
Swali:

Taja lugha-mame zinazopatikana humu nchini.  Toa mifano ya lugha zinazotokana na lugha mame hizi.

Lingua franca

Lingua franca ni neno linalotokana na lugha ya Kifaransa.  Linarejelea lugha inayotumiwa na watu wanozungumza lugha mbalimbali.  Pia huitwa lugha enezi.

Nchi ikiwa na lugha nyingi huwa kunazuka haja ya kupata lugha moja ambayo inaweza kutumika na makundi haya ya watu wanaozungumza lugha mbalimbali.  Lugha hiyo inayochaguliwa ndiyo hujulikana kama lingua franca.  Aghalabu lingua franca huchukuliwa kuwa lugha ya biashara.  Ni lugha ambayo hutumiwa na watu wote katika eneo kubwa hata kama wana lugha zao nyingine.  Kwa mfano, lugha ya Kiswahili ni lingua franca ya nchi za Afrika Mashariki na kati.  Hii ni lugha ambayo imetanda sehemu kubwa ya janibu hizi na imechaguliwa kuwa lugha ya mawasiliano.   Vile vile utapata kwamba katika bara la Afrika, lugha nyingi zilizokuwa za kikoloni ndizo zimefanywa kuwa lingua franca.  Kwa mfano, lugha ya Kiingereza na Kifaransa ni lingua franca katika nchi nyingi.  Kiingereza ni lingua franca ya ulimwengu wote.
 Swali:

Je, kuna umuhimu wa kuwa na lingua franca katika  nchi za Afrika? Fafanua jibu lako.

Lugha rasmi

Hii ni lugha ambayo inateuliwa katika nchi fulani ili itumiwe katika mawasiliano yote rasmi katika nchi.  Lugha hii huchaguliwa ili kutumiwa katika shughuli za serikali, kwa mfano, inatumiwa afisini, kuzungumza na wageni, katika taasisi mbalimbali, na ndiyo hutumiwa kwenye vyeti na shahada.

Nchi nyingi zilizotawaliwa zinatumia lugha za waliokuwa watawala wao kama lugha zao rasmi.  Wakati mwingine baada ya nchi kupata uhuru, huamua kutumia lugha ya humo nchini kama lugha rasmi.  Kwa mfano, Kenya na Uganda hutumia lugha ya Kiingereza kama lugha rasmi ilhali nchi ya Tanzania hutumia Kiswahili kama lugha rasmi.

Lugha ya taifa

Hii ni lugha ambayo kisiasa, kijamii na kiutamaduni inawakilisha watu  fulani.  Viongozi wa nchi huchagua lugha ya taifa hasa wanapogundua kuwa lugha ni kipengele muhimu katika utamaduni wa taifa.  Hivyo basi lugha ya taifa huwa ni lugha inayotambulisha na  kutumiwa na taifa fulani.  Lugha hii huweza vilevile kuwaunganisha wananchi wa matabaka mbalimbali.  Tukitazama kwa  mfano, viongozi wanaoshika hatamu, tunaona kuwa wanaweza kuchukuliwa tu kama viongozi wa taifa zima bali sio wa makabila mbalimbali iwapo watatumia lugha moja ya taifa.

Lugha ya taifa inaweza kulinganishwa na bendera ya taifa.  Kwa ambavyo tunajua kuwa bendera huitambulisha nchi, vivyo hivyo lugha hulitambulisha taifa.  Lugha ya taifa huwa na kusudi la kuibusha uzalendo miongoni mwa watu.

Katika baadhi ya nchi utapata kuwa lugha rasmi ndiyo pia lugha ya taifa ingawa sio lazima mambo yawe hivyo.  Kwa mfano, katika nchi ya Tanzania, Kiswahili ni lugha rasmi na pia lugha ya taifa.
Kumbuka:

Si lazima kila nchi iwe na lugha ya taifa ingawa ni lazima kila nchi iwe na lugha rasmi.

Swali:

Onyesha tofauti iliyopo kati ya lingua franca, lugha rasmi na lugha ya taifa.

Lugha mzazi

Makala ya UNESCO (1968: 689-90) yanaeleza lugha mzazi kama lugha ambayo mtoto huipata au huirithi katika siku zake za mwanzo na lugha hii baadaye  huwa lugha yake asili na huitumia kama chombo cha fikra na mawasiliano.
 Swali:

Lugha mzazi ni lugha gani?

Lugha mzazi ni lugha ambayo mtoto hujifunza kutoka kwa wazazi wake ambayo hao wazazi wanaiongea kama lugha yao kindakindaki.  Hii ni lugha ambayo hutumiwa kupitisha utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine na ndiyo hutumiwa kumkuza mtoto.

Wataalamu kama vile Sifuna (1980), Parry (2000) na Milon (1992) wameona umuhimu wa kufunzia katika lugha mzazi kwa sababu lugha hii inaaminika kuwa huendeleza ukuaji wa mtoto katika kuzikuza dhana ambazo humsaidia mtoto kung’amua mambo kwa haraka katika lugha ya pili.

Lugha ya kwanza

Hii ni lugha ambayo mtu anajifunza kwanza maishani mwake kabla ya lugha nyingine.
Swali:

Kuna tofauti gani kati ya lugha mzazi na lugha ya kwanza?

Lugha ya pili

Hii ni lugha ambayo mtu hujifunza baada ya kujifunza lugha ya kwanza.  Mtu huweza kijifunza lugha ya pili katika mazingira tofauti.  Kwa mfano, mtu anaweza kujifunza lugha hii kwa njia zisizo rasmi.  Hii inamaanisha kuwa anaipata lugha hii kupitia kule kuwasikiliza wenzake wakiongea au anajifunza kirasmi.  Hapa ni pale ambapo anaenda darasani akajifunza lugha hiyo.  Mtu hujifunza lugha ya pili kwa sababu mbalimbali.  Mara nyingi ujifunzaji wa lugha ya pili hutokana na swala la sera ya lugha katika nchi fulani.
Swali:

Je, wewe unafahamu lugha ngapi?
Ni sababu gani zilizokufanya ukajifundisha lugha hizo?

 Zoezi:

Huku ukitoa mifano, eleza dhana hizi
1. Lugha-mame   2.  lingua franca    3.  Lugha Rasmi    
4.  Lugha ya   Taifa   5.  Lugha mzazi

Muhtasari


Katika somo hili tumefafanua aina mbalimbali za lugha kwa kutumia kigezo cha uamilifu. Tumeona kuwa lugha hutenda kazi mbalimbali katika jamii.  Tumeona kuwa lugha mame hutuonyesha historia ya lugha zilizopo sasa.  Tumeona pia kuwa katika jamii ambayo watu wana lugha tofauti  tofauti, lugha moja huweza kuchaguliwa ili itumike kama lingua franca.  Hii ni lugha ambayo itatoa vizuizi vya mawasiliano.  Vile vile tumeona kuwa lugha moja huchaguliwa ili kutumika katika shughuli rasmi.  Na tumeona umuhimu wa lugha ya taifa kama lugha ambayo inawaunganisha wananchi na inachukuliwa kama kitambulisho cha nchi fulani.  Tumeona kuwa lugha mzazi ni lugha muhimu katika maisha ya mtoto kwa ambavyo ustadi katika lugha hii huwa kitangulizi cha ustadi katika lugha nyinginezo atakazojifundisha mtoto.  Kwa hivyo aina hizi za lugha haziifaidi tu jamii bali pia humfaidi mtu binafsi.

II.    Kazi za Lugha

Utangulizi
Katika sehemu iliyopita, tuliona kwamba lugha huweza kuainishwa katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kigezo cha uamilifu.  Hata hivyo, binadamu amepewa chombo ambacho anakitumia kutekeleza mambo mbalimbali ama kijamii au kibinafsi.  Katika sehemu hii tunataka kuangalia kazi mbalimbali za lugha katika jamii.

Lugha ni mali ya mtu binafsi na vile vile ni mali ya jamii kwa ujumla.  Kupitia kwa lugha watu  huweza kutekeleza mambo mbalimbali.  Hebu basi tuangalie kazi za lugha.

1.    Mawasiliano
Ni kweli kwamba binadamu amevumbua mbinu tofauti za kumwezesha kuwasiliana na wenzake.  Kwa mfano, kupitia mavazi, makazi, namna tunavyoashiria tabia zetu na kadhalika.  Lakini muhimu kabisa ni kwamba binadamu huwasiliana kupitia kwa lugha.  Kwa hivyo tunaona hapa kuwa dhima au kazi kuu ya lugha ni kuwasilisha dhana au mawazo tuliyonayo akilini mwetu.  Lugha huwawezesha wanadamu kuwasiliana na hivyo basi kuelewana.

Kupitia lugha, tunaweza kueleza au kuuliza mambo fulani na hata kubadilisha mawazo ya watu kuhusiana na jambo fulani.  Hivyo basi tunaona kuwa kila lugha ni mfumo ambao huwaruhusu watumiaji wa lugha hiyo kuingiliana na wenzao.
Lugha huweza kutumiwa kama chombo cha mawasiliano kwa sababu matumizi ya lugha hiyo ni ya kimfumo.  Hii inamaanisha kuwa kila lugha ina mpangilio maalumu; kwamba hakuna matumizi ya lugha yaliyo ya kiholela.  Kila matumizi hudhihirisha sifa fulani, kwa mfano, mazungumzo, usimulizi, lugha ya kimawazo, uulizaji na kujibu maswali.  Yote haya hudhihirisha mfumo fulani wa kimatumizi.  Jambo hili linadhihirika wazi hasa pale ambapo mawasiliano yanatatizika ikiwa mtu hatatumia maneno yanayofaa katika muktadha unaofaa, au kusimulia hadithi isiyokuwa na mshikamano.
Swali:

Je, umewahi kujipata katika hali ambayo mawasiliano yalivurugika? Ni kitu gani kilichosababisha mvurugano huo?

2.    Lugha kama chombo cha kuendeleza jamii
Lugha husaidia katika kuendeleza jamii.  Watu wanaozungumza lugha moja wanaweza kuwasiliana na wenzao.  Na bila lugha moja watu hawa watakabiliana na matatizo ya lugha.  Lugha hapa inatumika kama kitambulisho cha kundi la watu.  Hivyo basi lugha ambayo watu wanaifahamu kwa pamoja huwasaidia watu kuja pamoja.

Lugha pia hufanya kazi inayojulikana kama uhusiano wa kifati (Phatic communion).  Hii ni dhana iliyoanzishwa na mtaalamu kwa jina Malinowski (1923).  Alidai kuwa kuwepo kwa lugha huwafanya watu wajihisi kwamba wako pamoja na wenzao.  Kwa mfano, maamkuzi ya asubuhi, adhuhuri na jioni ambayo tumezoea kuyatamka ni aina hii ya uhusiano wa kifati.  Nia yake ni kuweka uhusiano mwema kati yetu.  Katika uhusiano wa kifati, hakuna ujumbe mpya unaotolewa ila kwamba kuna uelewano na hivyo basi uhusiano wa kijamii unaendelezwa.
Swali:
Ni kwa njia gani lugha yako huendeleza uhusiano mwema katika jamii?

Kutawala uhalisia

Lugha huwa na nguvu na hutumiwa kutawala uhalisia.  Lugha huwasaidia watu kubadilisha vitu katika mazingira yao kupitia kwa matumizi ya maneno maalumu.  Maneno haya yanapotamkwa yanakifanya kitendo kitendeke.  Kwa mfano, mtu anaposema “Meli hii naiita uhuru” au padri anaposema, “Ninawatangaza bwana na bibi” Mtu anapoyatamka maneno haya katika hali maalumu basi binadamu huyachukulia jinsi hiyo.

Vile vile aina yoyote ya imani huhusisha matumizi ya lugha kama njia moja ya kutawala nguvu ambazo waumini wanaona kuwa zinaathiri maisha yao.  Kwa mfano, kasisi anapombatiza mtoto au mtu huwa anasema”, Ninakubatiza kwa jina la --“,  na baada  ya maneno hayo mtu huyu huwa amebatizwa.

Kuwasilisha hisia

Lugha hutumiwa kueleza hisi zetu.  Tunapokuwa na mfadhaiko au shida tunajipata tukijizungumzia wenyewe.  Wakati mwingine tunaapa pale ambapo tumekasirika.  Lakini tunaweza pia kuonyesha hisia zenye furaha au zinazoonyesha kuvutiwa na kitu fulani kwa kutamka sauti fulani.  Kwa hivyo, katika kila hali tunamojipata huwa tunatumia lugha katika kuwasilisha hisia zetu.

Chombo cha fikra

Swali:


Je, kama hungekuwa na lugha ungetumia nini kufikiria?
Imesemekana kuwa lugha ndiyo humwezesha mtu kufikiria. Jambo hili linadhihirika wazi pale ambapo mtu huwa amezama katika tafakuri na bila kufahamu akaanza kuyatamka yanayompita akilini.  Katika hali kama hii lugha ipo lakini katika hali isiyojitokeza kwenye sauti.  Wataalamu wamesema kuwa mtu hufikiria kwanza kabla ya kuongea au kuandika.  Hali hii inajulikana kama “mazungumzo ya ndani”.

Lugha kama kitambulishi cha mtu binafsi
Lugha hutumika kueleza hulka ya mtu.  Kila binadamu anao urazini unaomfanya kuelewa kuwa lugha ni sehemu ya nafsi yake.  Hivyo basi, binadamu wana “sauti” katika kila kitu kinachotendeka katika maisha yao.  Kila binadamu ana uhuru wa ama kusema au kutosema, kungungumza sana au kusema maneno machache tu. Na vile vile ana uhuru wa kuchagua namna ya kusema kile anachotaka kusema.  Hivyo basi lugha inatumika kama chombo cha kujieleza kwa kutumia njia mbalimbali.

Lugha kama chombo cha kujipatia mafunzo

Kupitia kwa lugha, binadamu huweza kuelimika na kuuelewa ulimwengu wake.  Lugha hutumika katika ujifunzaji. Tunatumia lugha kuuliza maswali na vile vile tunaitumia katika kuyajibu maswali.  Kupitia lugha tunaendeleza majadiliano ya kiusomi na kufikia mahitimisho.
Zoezi:


Kwa kuzingatia miktadha ifuatayo, fafanua kazi za lugha:  kanisani, shuleni, kazini na hali zisizo rasmi.
  Muhtasari:


Katika somo hili tumeonyesha kazi mbalimbali zinazofanywa na lugha.  Tumeonyesha kuwa lugha hutenda kazi katika kiwango cha mtu binafsi na cha kijamii.  Hivyo basi hatuwezi kupuuza swala la lugha katika jamii.

Maelezo ya dhana:

Uamilifu:    Hali inayoonyesha kazi ya lugha katika jamii.
                   au utendakazi wa kitu.
SOMO LA KUMI
DHANA ZA KIMSINGI KATIKA LUGHA
Utangulizi
Katika somo hili dhana mbalimbali za kimsingi katika lugha zitashughulikiwa.  Dhana hizi ni umilisi, utendaji ‘langue’ ‘parole’,  lafudhi, lahaja, lugha sanifu, jumuia lugha, uwili lugha, ulumbi, (wingi lugha), pijini na krioli.  Baadhi ya dhana hizi zinawakilisha mabadiliko ambayo hutokea katika lugha.
 Malengo:
    Baada ya somo hili utaweza:
·         Kutaja sifa za dhana za kimsingi katika lugha.
·         Kueleza tofauti iliyopo baina ya
(a)  Umilisi na utendaji
    (b)  ‘Langue’ na ‘Parole”
    (c)  lafudhi na lahaja
    (d)  uwili lugha na ulumbi
    (e)  pijini na krioli
·         Kueleza athari ya hali hizi katika lugha.

Umilisi na Utendaji

Dhana hizi mbili zimefafanuliwa kwa undani sana na mwanaisimu Noam Chomsky aliyekuwa mwasisi wa  nadharia ya sarufi zalishi. Tunaweza kusema kuwa umilisi ni ujuzi alio nao mzungumzaji au msikilizaji kuhusu lugha yake.  Huu ni ujuzi wa kanuni zinazotawala lugha. Huu ni ujuzi alionao mzawa katika lugha yake.

Tunafahamu kwamba mzawa wa lugha fulani huwa na uwezo kamili wa lugha hiyo tofauti na yule aliyejifunza lugha hiyo kama lugha ya pili.  Mtu aliye na umilisi si lazima awe amesoma; anaweza kuwa ni mzee tu wa pale vijijini.
Bornstein (1977:36) anaona kuwa umilisi wa lugha utajumlisha uwezo ufuatao:
a)    Kuzalisha na kuelewa sentensi nyingi zisizo kikomo.  Umilisi humwezesha mzungumzaji kutumia sentensi nyingi hata zile ambazo hajawahi kusikia.
b)    Kutambua sentensi zilizo sahihi kisarufi na zile zisiso sahihi.
c)    Kutambua muundo wa sentensi.
d)    Kutambua sentensi ambazo zina maana sawa.
e)    Kutambua aina mbalimbali za sentensi kama vile, taarifa na swali, kukiri na kukanusha.
f)    Kugundua utata.
Kwa mfano: Mtoto alikuwa amebeba kanga.  Katika sentensi hii ni vigumu kufahamu maana ya neno ‘kanga’ iliyokusudiwa.
Kumbuka:

·         Umilisi unahusu sheria anazozifahamu mzungumzaji asilia zinazomwongoza anapozungumza.

·         Sheria hizi zimo akilini mwa mzungumzaji.

  Zoezi:

1.  Andika sentensi mbili ambazo zina utata halafu uonyeshe
    kinachosababisha utata huo.
2.  Andika sentensi mbili zenye miundo tofauti lakini maana moja.

Utendaji ni ule usemaji au utumizi wa lugha wa mzungumzaji.  Hii ni jinsi mtumiaji wa lugha anavyotumia umilisi wake katika mawasiliano ya kawaida.  Utendaji  hurejelea jinsi mzungumzaji anavyotumia lugha maishani.
Utendaji hutegemea mambo mengine kama vile mazingira, utamaduni, jinsia na muktadha.  Kuna mambo yanayoweza kuathiri utendaji kama vile uchovu, furaha, ulevi, usingizi, hamaki na usahaulivu.

Kwa kweli utendaji ni ile hali ambayo mzungumzaji anajaribu kutumia umilisi alio nao akilini.  Lakini kumbuka kwamba kuna vikwazo vya kisaikolojia na kifisiolojia ambavyo huathiri utendaji kama ilivyotajwa katika aya iliyotangulia.  Mtu anaweza kuishiwa na pumzi anapozungumza; anaweza kutaja neno ambalo hakukusudia; anaweza kutunga sentensi kimakosa na akagundua itambidi kurejearejea nyuma; hata matatizo ya kimatamshi yanaweza kutokea.

Uhusiano kati ya  umilisi na utendaji unakaribiana sana na ule wa umbo na yaliyomo.  Wanaisimu wa siku hizi  hujihusisha zaidi na umilisi wa lugha kuliko utendaji wake.  Wanaamini kwamba katika kufanya uchunguzi kuhusu lugha,ule uwezo au umilisi wa mzungumzaji asilia wa lugha fulani ndio muhimu.
 Swali:

Je, utendaji wa mzungumzaji unawakilisha moja kwa moja umilisi wake?  Eleza.

‘Langue’ na ‘Parole’

Maana nyingi za neno ‘lugha’ zilimfanya Ferdinand de Saussure kuanzisha mfumo wa istilahi tatu za Kifaransa zinazoingiliana. Istilahi hizi ni ‘langage’, ‘langue’ na ‘parole’.  Aliona kuwa ‘langage’ ni uelekevu wa lugha unaopatikana katika binadamu wote.  Ni ile hali kwamba binadamu ye yote asiye na kasoro fulani anaweza kuitumia lugha.  Hii ni dhana ya kijumla na inahusu viwango viwili:  langue’ na ‘parole’.

Kwa mujibu wa Ferdinand de Saussure, lugha inaweza kuchanganuliwa kutoka kwa mitazamo miwili ambayo ameiita ‘langue’ na ‘parole’.  Mitazamo hii inafanana kwa kiasi kikubwa na ile iliyopendekezwa na Chomsky: umilisi na utendaji.  

‘Langue’ (Mfumo-Lugha)
Kwa mujibu wa Ferdinand de Saussure ‘langue’ ni mfumo dhahania wa lugha fulani ambao unatumiwa na jamii fulani.  Huu ni uwezo wote wa lugha alionao binadamu na huwa umehifadhiwa katika akili yake.  Ni jumla ya ishara-maneno yaliyo katika akili ya mtumiaji wa lugha.  Mfumo-lugha ni asasi ya kijamii na hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Swali:

Je, kuna tofauti gani basi kati ya umilisi na ‘langue’?

Umilisi wa lugha wa Chomsky hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na mfumo lugha au ‘langue’, bali na ujuzi wa mfumo-lugha.  Tofauti iliyopo ni kwamba Saussure alisisitiza sana sifa ya kijamii ya mfumo-lugha.

Istilahi ya kifaransa ‘langue’ ina maana ya kawaida ya ‘lugha’.  Inapotumiwa kitaalamu kama alivyokusudia Ferdinand hubakia hivyo tu.

‘Parole’ (Utendaji)
Hii ni ile hali halisi ya kuzungumza.  Ni usemaji wenyewe wa lugha ambao hufanywa na kila mtu.  Haya ni matamshi halisi anayotoa mzungumzaji yaani ule utendaji.  Ni kile tunachotenda na lugha tunayoirithi.

Kumbuka:


Parole’ (utendaji) ni tendo la mtu binafsi kinyume na ‘langue’ ambayo ni asasi ya kijamii.

Ferdinand de Saussure ametahadhirisha kuwa utendaji huwa si sahihi wakati wote kutokana na udhaifu wa maumbile ya mwanadamu.  Kwa hivyo utendaji wo wote si kiwakilishi sahihi cha mfumo-lugha alio nao mzungumzaji.

Kwa hivyo, tofauti kati ya ‘langue’ na ‘parole’ ni ile ya uwezo tulio nao na matamshi halisi tunayotoa; pia hali ya kijamii na hali ya mtu binafsi.

Lafudhi

Lugha anayozungumza mtu inaweza kumtambulisha kijiografia au kijamii.  Hata hivyo katika lugha hiyo hiyo, kuna mambo yanayojitokeza ambayo humtofautisha mzungumzaji mmoja na mwingine.  Kila mwanajamii yeyote huwa na utofauti wa aina fulani katika matumizi yake ya lugha.

Kwa mfano, wewe unaweza kufikiria kuwa unaongea Kiswahili Sanifu.  Labda ni ukweli,  lakini  utaona kuwa katika mazungumzo yako utazungumza kwa njia iliyo tofauti na mwenzako anayeongea lugha hiyo hiyo.

Kuna watu wanaodai kwamba baadhi ya watu wana lafudhi na wengine hawana.  Tunaloweza kusema ni kwamba baadhi ya lafudhi za watu huwa zinajitokeza kwa uwazi zaidi kuliko wengine.  Lakini kila mzungumzaji wa lugha huzungumza kwa lafudhi yake.

Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa lafudhi ni namna ya uzungumzi unaohusishwa na mtu binafsi.  Hii ina maana kwamba, hata kama tunazungumza lugha sanifu, kuna kitu kinachotutofautisha na watu wengine.  Kitu hicho ni: ile namna tunayotamka maneno.  Ni kweli kwamba wazungumzaji wote wa lugha moja huelewana wanapozungumza, lakini hakuna  watu wawili wanaozungumza kwa namna moja.

Kumbuka:

·         Lafudhi ni sifa ya kiisimu inayotambulisha mtu.
·         Lafudhi ya mtu huweza kubadilika katika vipindi mbalimbali vya maisha yake.

Hivyo basi, kuwepo kwa lafudhi kunamaanisha kuwa kuna mfumo fulani wa kiisimu unaohusishwa na kila mzungumzaji.  Jambo hili hudhihirika wazi pale tunamtambulisha mtu na matamshi au sauti yake bila kumwona.  Hii inamaanisha kuwa kila mtu ana mtindo wa kipekee wa lugha.  

Wardhaugh (1994) anasema kuwa tofauti hizi ni sifa muhimu za lugha yoyote ile.  Na kama ambavyo tumesema, tofauti hizi zinahusiana sana na mambo kama kule anakotoka mtu kijiografia, tabaka lake, umri na hata jinsia ya mtu.
Swali:


Jaribu kutambua tofauti za kimatamshi zinazodhihirika miongoni mwa rafiki zako na familia yako hasa wanapozungumza lugha ya Kiswahili.

Lahaja

Tumeona katika sehemu iliyotangulia kuwa watu wanaweza kuongea lugha moja lakini hakuna watu wawili wanaoongea kwa namna moja.  Kila mtu ana tofauti zake za kiisimu. Tunapochunguza lugha yoyote ile, tunatambua kuna tofauti fulani katika jinsi watu wanavyotumia sauti, msamiati na hata miundo ya kisarufi.
Kuwepo kwa istilahi ya lahaja katika muktadha wa lugha kunamaanisha kuwa kuna tofauti fulani zinazopatikana  katika lugha.

Je, lahaja ni nini?

Wataalamu  mbalimbali wamefafanua dhana hii.  Hebu tuone wamesema nini?
Massamba na wengine (1999) wanasema kuwa lahaja ni mojawapo kati ya vijilugha ambavyo huhesabika kama lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani  fulani, kama vile fonolojia, msamiati na hata sarufi.

Musau (1990) anaeleza kuwa lahaja ni aina za uzungumzaji katika jamii inayozungumza lugha moja.  Aina hizi za uzungumzaji huwa zinatofautiana kimsamiati, kifonolojia, kimofolojia na kwa nadra sana kisintaksia.

Aghalabu aina hizi za uzungumzaji huwa hazitatizi mawasiliano kati ya kikundi kimoja cha jamii inayozungumza lugha moja na kile kingine.  Lahaja basi ni sehemu moja ya ule mgawanyiko wa mkondo wa lugha fulani.  Mkusanyiko wa hizo lahaja ndio unaitwa lugha fulani.

Kwa mfano, lugha ya Kiswahili ina lahaja mbalimbali kama vile, Kimvita, Kiamu, Kiunguja, Kimtang’ata na Kimrima.

Swali:


Je, lugha yako ina lahaja ngapi?
Taja lahaja hizo.

Kile kinachodhihirika wazi katika lahaja mbalimbali ni tofauti katika matumizi ya msamiati wa vitu mbalimbali pamoja na utamkaji wa sauti zinazopatikana katika lugha hiyo.  Mbali na tofauti hizi, kuna ile hali ya kusikilizana katika watumiaji wa lahaja hizi.

Madai kuwa lahaja moja ni bora kuliko nyingine yanatokana na ile hali ya lahaja moja kupewa hadhi kuliko nyingine.  Jambo hili hutokana na sababu za kijamii au kisiasa.  Mara nyingi lahaja hiyo huwa ni ya watu wa tabaka la juu.
Kumbuka:


Kiisimu hakuna lugha au lahaja iliyo bora  kuliko nyingine duniani, zote ni sawa, kwa sababu zinatimiza majukumu ya kiisimu ya jamii husika.


Kuzuka kwa Lahaja

Kuzuka kwa lahaja mbalimbali duniani ni dhihirisho kuwa daima lugha inabadilika.  Wakati mwingine mabadiliko haya huzidi hivi kwamba hakuna uelewano kabisa kati ya watu waliokuwa wakizungumza lugha moja.  Inapotokea hivyo basi zile lahaja hujitosheleza zenyewe na kuwa lugha kamilifu.  Jambo hili linadhihirika katika lugha ya Kilatini ambapo lahaja kadhaa zilibadilika kuwa lugha za Kifaransa, Kihispania, Kiitaliano na Kireno.

Lahaja huzuka kutokana na vizuizi vya  mawasiliano vinavyoibuka kati ya makundi ya watu wanaozungumza lugha moja.  Vizuizi hivi vinaweza kuwa vya kijiografia, kiuchumi, kisiasa au kijamii. Tunapoangalia jinsi lahaja huzuka, mambo mawili huwa ya kimsingi kuzingatia.  Kwanza ni wakati na pili ni umbali.

Tunajua kwamba lugha hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na baada ya muda mabadiliko ya matamshi, msamiati na sarufi yanayoletwa na kizazi kipya huanza kutokea.  Mabadiliko haya yakikosa kusambaa katika eneo lote basi tofauti zinajitokeza na tofauti hizi ndizo hujulikana kama lahaja.  Katika mabadiliko haya, wakati ndio jambo la kimsingi.  Tunahitaji vizazi kadha wa kadha kutumia neno fulani tena kwa muda mrefu ili neno hili lionekane tofauti na neno linalotumika katika lahaja nyingine.

Mtaalamu Trudgill (1983) anaona kuwa kipengele cha kijiografia ni muhimu katika kuleta tofauti za kilahaja.  Watu wanaozungumza lugha moja wakihamia maeneo tofauti na kutengwa na wenzao kwa umbali fulani, baada ya muda, lugha yao itaanza kuwa tofauti hasa ikiwa hakuna uhusiano mkubwa wa kimawasiliano kati ya makundi haya.  Hii ndiyo itakuwa lahaja kijiografia.  Lahaja kijiografia ni lahaja zinazozungumzwa katika eneo fulani la kijiografia.

Kwa upande mwingine, inaweza kutokea kuwa wazungumzaji wa lugha moja wametenganishwa na vikwazo vya kitabaka kama elimu au uchumi.  Kila tabaka litaathirika kivyake kiisimu.  Hii inakuwa lahaja kijamii.
Swali:

Ni vipi twaweza kujua ikiwa tunazungumzia juu ya lahaja au lugha?

Kuna vipengele ambavyo hutuwezesha kuamua tofauti za kiisimu zinazotambulisha lahaja na lugha.  Hebu tuone vipengele hivyo:

1.  Kusikilizana

Katika kipengele hiki tunaona kuwa ingawa lahaja hutofautiana, watu wanapozungumza wataelewana.  Ikiwa wazungumzaji wawili walio na tofauti fulani katika lugha zao wataelewana wanapozungumza, basi itachukuliwa kwamba wanatumia lahaja tofauti tu za lugha moja.  Iwapo hawataelewana basi inamaanisha kuwa wanazungumza lugha tofauti.

  

Mwendeleo lahaja hurejelea ule mfuatano wa jinsi lahaja zinavyopakana kijiografia.  Yule (1996) anadai kuwa kuna baadhi ya maneno ambayo yataendelea kutumika katika lahaja jirani kutoka kwa lahaja inayopakana nayo.  Hivyo basi hakuna ule mpaka  kamili kati ya lahaja moja na nyingine.  Mambo yanapotokea hivyo tunaweza kuchukulia lahaja kama kitu kinachopatikana kwenye mwendeleo bila kuwa na kikomo fulani.


Kwa mfano, tunaweza kupata mkururo kama huu wa lahaja A-B-C-D-E-F-G … Katika mkururo huu huwa kuna kuelewana katika lahaja zilizopakana kama vile A-B, B-C au C-D, lakini zile zilizotengana kwa mbali kama A-G huwa hakuna maelewano rahisi.  Tukiangalia kwa mfano lahaja za Kiswahili, wazungumzaji wa lahaja zinazopatikana katika sehemu ya kaskazini wataelewana kwa urahisi wenyewe kwa wenyewe kuliko ikiwa watazungumza na wale wanaopatikana katika sehemu ya kusini.  

Nchini Kenya kuna lugha nyingi ambazo zina lahaja; kwa mfano Kiswhaili na Kilugha. Kiswahili kinazo lahaja zifuatazo kuanzia kaskazini mwa pwani hadi kusini: Chimbalazi (Cimiini), Kitukuu (Kibajun) Kisiu, Kipate, Kiamu na Kishela ambazo ni lahaja za kaskazini.  Lahaja za kati ni Kimvita, Kijomvu, Kingare na Cifundi.  Nazo za kusini ya kati ni Kivumba, Kihadimu, Kitumbatu, Kipemba na Kimtang’ata.  Nazo za kusini kabisa ni:  Kimrima, Kingazija, Kingwana na Kiunguja.  Lugha ya Kiluhya, kulingana na Angogo (1980), inazo lahaja kumi na saba.  Nazo ni Kibukusu, Kihayo, Kimarachi, Kisaamia, Kinyala cha kaskazini, Kinyala cha Kusini, Kiwanga, Kimarama, Kikhisa, Kinyore, Kilogooli, Kiidakho, Kisukha, Kikabras, Kitsotso, Kitiriki na Kitachoni.  Kuna lugha nyingine ambazo zina lahaja nchini Kenya.  Kwa mfano, Kikamba kina lahaja sita, Kikuyu kinazo sita na Kidholuo kina lahaja sita.

Katika mipaka ya lahaja hizi unaweza kupata kuwa wazungumzaji wa lahaja moja wanazungumza lahaja jirani.  Watu kama hawa watachukuliwa kuwa wana uwili lahaja.
Zoezi:

Huku ukirejelea vitabu vya historia ya Kiswahili, onyesha jinsi lahaja za Kiswahili zinavyotofautiana kisauti na kimsamiati.

2.  Lugha Sanifu
Kuwepo kwa lugha sanifu au maandishi yanayotumiwa na kundi la watu fulani hutusaidia kujua kama zinazohusika ni lahaja au lugha.  Ikiwa makundi mawili au zaidi yanayotofautiana katika maongezi hukubaliana kuwa yana ‘lugha’ sanifu moja au kama yanatumia aina moja ya maandishi, basi inachukuliwa kuwa yanazungumza lahaja tofauti na si lugha tofauti.

3.  Vipashio visivyo vya Kiisimu
Vipashio fulani kama utamaduni mmoja, utii wa kisiasa, au dhamiri za wazungumzaji huweza kutumiwa kutofautisha kati ya lahaja na lugha.  Kwa mfano, wazungumzaji wa Kiswidi, Kideni na Kinorwegian wanasikilizana wanapozungumza lakini kwa sababu wanaishi katika nchi tofauti inachukuliwa kwamba wanazungumza lugha tofauti.  Kipengele cha kisiasa kinatumiwa kuwatenga katika nchi mbalimbali kwa sababu ya mipaka.  Katika mfano mwingine, wazungumzaji wa Kichina na Mandarini hawaelewani wanapozungumza, lakini inachukuliwa kuwa wanazungumza lahaja tofauti za lugha ya Kichina kwa sababu wanatumia mfumo mmoja wa maandishi na pia kwa sababu za kisiasa – wanaishi Uchina.

Lugha Sanifu

Katika mada ya lahaja ambayo tumezungumzia, tumeona kuwa kuna namna tofauti za jinsi makundi ya watu hutumia lugha kimatamshi na kimsamiati.

Kwa sababu ya tofauti hizi huwa kunazuka haja ya kuwa na lugha ya katikati ambayo inaweza kueleweka kwa kila msemaji.  Inabidi lahaja moja ichaguliwe na isanifishwe.
 Swali:

Kusanifisha lugha ni kufanya nini?

Wataalamu wengi wamelishughulikia swala la usanifishaji wa lugha na wamekubaliana kuwa, lugha sanifu au kwa maneno mengine lahaja sanifu yaweza kuelezwa kama lahaja iliyoteuliwa itumike kama chombo cha mawasiliano hasa upande wa elimu, utawala na sayansi.

Tunaweza kusema kuwa lugha sanifu ni lugha ambayo imekubaliwa kutumika katika shughuli zote rasmi na ambayo inakubaliwa kimatumizi na wasemaji wengi.
Usanifishaji wa lugha huanza kwa kuchagua mojawapo wa lahaja zilizopo.  Lahaja hiyo inapochaguliwa, miundo fulani ya kiisimu hufanyiwa marekebisho.  Miundo hii huendelezwa na kuchukuliwa kwamba ndiyo kaida za kufuatwa katika lugha hiyo.  Miundo hii pia husambazwa kupitia uchapishaji wa vitabu ili iweze kuwafikia watu wengi.

Lugha sanifu ni muhimu kwa sababu inazuia hali ya kutokuelewana ambayo hutokea pale ambapo kuna mitindo tofauti ya kuandika lugha moja.  Hivyo basi lugha hii husaidia katika kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji wa lugha nyingi au lahaja nyingi.

Lugha hii ndiyo hutumika katika maandishi rasmi, katika vyombo vya habari na ndiyo hufunzwa shuleni.  Ni aina ya lugha ambayo huwa tunawafunza wageni ambao wanataka kujifunza lugha ya pili. Lahaja sanifu inahusiana moja kwa moja na elimu na utangazaji na inaelezwa zaidi kupitia maandishi kuliko katika mazungumzo.  Lugha ya Kiswahili kwa mfano, imesanifishwa.  Lahaja iliyotumiwa kama msingi wa kuisanifisha ni Kiunguja.
Zoezi:

Onyesha uhusiano uliopo kati ya lafudhi, lahaja na lugha sanifu.

Jumuia Lugha

Kulingana na mtazamo wa wana-elimu jamii (wanasosholojia), ‘Jumuiya’ ni neno linalorejelea ile hali ya kundi la watu kufahamu jambo fulani kwa pamoja, wana umiliki sawa na vilevile tabia zinazofanana.  Wanaisimu huihusisha dhana hii na swala la lugha, ndipo tunapata dhana ya “jumuia lugha”.

Kimsingi dhana hii inasisitiza kwamba tabia au matendo ya lugha yanaweza kuwa kitu ambacho kinaunganisha kundi fulani la watu.  Hata hivyo kumekuwepo na utata mwingi juu ya maana halisi ya dhana hii.  Jambo hili linadhihirika wazi  kutokana na jinsi wataalamu mbalimbali walivyoifasiri.  

Hebu basi tuangalie walichosema wataalamu kuhusu dhana hii.
Yule (1996) anasema kuwa jumuia lugha ni kikundi cha watu ambao wana kaida, sheria na matarajio ya pamoja kuhusiana na matumizi ya lugha.

Lyons (1970:326) anasema kuwa, jumuia lugha ni jumuia ya watu wanaotumia lugha moja (au lahaja).

Kulingana na maelezo haya, jumuia lugha zinaweza kuingiliana (kwa mfano, pale kuna watu ambapo wanaoongea lugha zaidi ya moja) na watu hawa hawahitaji kuwa na umoja wowote wa kijamii au kitamaduni.  Ukweli ni kwamba ni rahisi kutenga jumuia lugha kwa njia hii, kwa sababu tunaweza kuzitenganisha lugha na hata lahaja.

Hockett (1958), Bloomfield (1933) na Gumperz (1962) wanakubaliana kuwa kila lugha huifasiri jumuia lugha na kwamba jumuia lugha ni kundi la watu wanaowasiliana ama moja kwa moja au kwa njia nyingine kupitia kwa lugha moja.

Katika fasiri hii, tunaona kuwa kigezo cha muingiliano wa mara kwa mara kinajitokeza.  Hii inaweza kuchukuliwa kuwa ikiwa jamii mbili zinazungumza lugha moja lakini hazina mtagusano basi zitachukuliwa kuwa jumuia lugha tofauti.  Fasiri hii imeondoa msisitizo wa lugha ya pamoja na kuzingatia mawasiliano.

Nao Hymes (1972) na Halliday (1978), wanasema kuwa, tunapozungumzia jumuia lugha ni muhimu kuzingatia sheria za pamoja za uzungumzaji na ufasiri wa matendo ya uzungumzaji.  Katika fasiri hii, tunaona kuwa msisitizo unawekwa kwa jumuia lugha kama ni kikundi cha watu ambao wanahisi kuwa wao ni jumuia.

Naye Labov (1972) anatilia mkazo mielekeo ya watu kwa lugha na thamani zao kuhusu miundo ya lugha na matumizi.
Fasiri hizi zote ni sahihi kwa sababu zinaeleza jumuia lugha ni nini.  Kutokana na fasiri hizi basi tunapata sifa zifuatazo za jumuia lugha:
1.       Ni kundi la watu.
2.       Watu wanaowasiliana kwa lugha moja.
3.       Wanaweza kuwa wanaishi eneo moja au maeneo tofauti.
4.       Kuna mtagusano au kuingiliana kwa  watu hawa mara kwa mara.
5.       Ni watu walio na mielekeo sawa kuhusu lugha.
6.      Ni watu walio na utamaduni sawa.
Swali:

Kutokana na sifa hizi za jumuia lugha, waweza kusema nini kuhusiana na wazungumzaji wa lugha mbalimbali nchini Kenya?

Uwili-Lugha na Wingi Lugha

Katika nchi nyingi ulimwenguni, hatupati tu lahaja nyingi za lugha moja, bali tunapata lugha mbili au zaidi zikitumiwa katika nchi moja.  Kwa mfano, nchini Kenya kunazo lugha takribani arobaini ambazo tunaweza kuziita lugha-wenyeji.  Kando na lugha hizi kuna lugha ya Kiingereza ambayo ni lugha rasmi na vile vile kuna lugha ya Kiswahili ambayo in lugha ya taifa.

Kunapotokea mtagusano wa lugha mbalimbali, matokeo yake huwa ni watu kuwa wana-uwili lugha au wana wingi lugha.  Kwa sababu binadamu ni kiumbe aliye na uwezo wa kutumia lugha, yeye hujipata kuwa anazungumza lugha zaidi ya moja ili aweze kuwasiliana na wenzake.
Swali:

Je, uwili lugha au wingi lugha ni nini?

Dhana ya uwili-lugha ina utata mwingi, na kwa sababu hiyo, wataalamu wameibuka na fasiri mbalimbali kuhusiana na dhana hii.  Kila moja ya fasiri hizi inajitosheleza katika aina ya uwili-lugha. Hebu basi tuone wanasema nini:

Bloomfield (1932) anasema uwili-lugha ni umilisi kamili wa lugha mbili kama ule alio nao mzawa wa lugha moja katika lugha yake. Naye Mackey (1962) anasema uwili-lugha ni kule kutumia lugha mbili au zaidi, moja ikichukua nafasi ya nyingine katika miktadha mbalimbali. Haugen (1953) anaeleza kuwa, Uwili-lugha huanzia pale ambapo mzungumzaji wa lugha moja anaweza kutoa kauli kamili na zenye maana katika lugha nyingine.

Kutokana na fafanuzi hizi uwili lugha ni hali ambayo mzungumzaji mmoja anaweza kutumia lugha mbili.

Kumbuka:

Uwili-lugha ni hali ambapo mtu anaweza kuzungumza lugha mbili.
Wingi lugha ni hali ya mtu kuzungumza zaidi ya lugha mbili.

Mambo yanayosababisha Uwili-Lugha na Wingi Lugha


1.    Ndoa mseto
Hali ya ndoa mseto ni jambo la kawaida katika ulimwengu wa sasa.  Hali hii inapotokea mke au mume hulazimika kujifunza lugha ya pili.

2.    Elimu
Aghalabu watu wanapoenda shuleni wanafunzwa lugha ya pili.  Kwa mfano, mtoto anapokuwa mdogo hujikuta katika mazingira ambayo wazazi wake wanatumia lugha wenyeji.  Anapotimia umri wa miaka sita mtoto huyu huenda shuleni ambako anafunzwa Kiingereza na Kiswahili.  Ripoti ya hivi karibuni inaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi elfu mia nne kote ulimwenguni wako katika nchi mbalimbali kwa masomo ya juu.  Wale walio katika nchi zinazotumia lugha nyinginezo kama vile Kijerumani au Kifaransa hulazimika kujifunza lugha hizi.

3.    Biashara
Kutokana na ulimwengu kufungua masoko ya biashara mbalimbali watu hulazimika kujifundisha lugha nyingine ili waweze kuwasiliana kwa haraka.

4.    Dini
Dini anayofuata mtu inaweza kuwa katika lugha fulani, kwa mfano, Waisilamu wengi wanafahamu Kiarabu kwa sababu hii ndiyo lugha ambayo hutumiwa sana katika mahubiri hasa kukariri korani.  Aidha, mtu anaweza kuamua kuishi katika nchi fulani kwa sababu ya umuhimu wake kidini au akaamua kuondoka katika nchi fulani kwa sababu ya mateso na dhuluma za kidini.  Katika hali kama hizi upo uwezekano wa kujifunza lugha mpya.

5.    Siasa
Katika baadhi ya nchi, uwili-lugha hutokea katika jamii za walio wachache, na jambo hili hutokana na sababu za kihistoria na kisiasa.  Kwa mfano, nusu ya kabila fulani inaweza kujipata katika nchi nyingine.  Hivyo basi, kundi hili litalazimika kujifunza lugha ya nchi hiyo ambayo imetengwa kuwa lugha rasmi.

Vile vile, tunaweza kupata kuwa shughuli nyinginezo za kisiasa kama vile uhamaji kwa sababu ya vita.  Watu watahama nchi nyingine wakitoroka vita nchini mwao.  Wanalazimika kujifundisha lugha inayotumika katika nchi waliyohamia.  Kwa mfano, Wasomali wanaohamia nchi za Kenya au Tanzania hulazimika kujifunza Kiswahili.

6.  Majanga ya Kitaifa
Majanga kama mafuriko, njaa, milipuko ya volkeno, na ukame husababisha kuhama kwa umati wa watu.  Kwa njia hii watu wanaozungumza lugha mbalimbali hukutana.
 Swali:

Je, waweza kufikiria sababu zingine zinazomfanya mtu kutaka kujua zaidi ya lugha moja?

Mambo muhimu ya Kuzingatiwa katika Uwili-Lugha

Mtaalamu Mackey (1962) anapendekeza mambo manne ambayo fasiri yo yote ya uwili-lugha inahitaji kuzingatia:  kiwango, dhima, ubadilishaji na athari (au uingiliaji).
1.    Kiwango:
Tumeona kuwa mwana uwili-lugha ni mtu ambaye anazungumza lugha mbili kwa ustadi, kwa mfano Bloomfield anadai kuwa mwana uwili-lugha anahitaji kuwa na ustadi katika lugha ya pili kama alionao katika lugha yake ya kwanza.  
Swali:

·         Je, unazifahamu lugha ngapi?
·         Ufahamu wako wa lugha ya kwanza unalingana na ule wa lugha ya pili?

Tunapowasikia watu wakiongea, tunaona kuwa watu hawa hutofautiana katika jinsi wanavyodhibiti lugha yao ya kwanza, na hali hii inawakumba wale wanaojifunza lugha ya pili.  Ni lini tunaweza kuamua kuwa sasa mtu anazungumza lugha ya pili kama anavyoizungumza lugha yake ya kwanza?

Hivyo basi, swali tunalohitaji kujiuliza ni: Je, ni kwa kiasi gani mzungumzaji ana fahamu lugha hizo mbili au tatu?
Mtazamo tofauti na huu ni ule ambao unachukuliwa na wanaisimu ambao hawatazami uwili-lugha kwa kuzingatia kiwango bali kwa kuzingatia dhima ya lugha hiyo.

2.    Dhima
Wanauwili-lugha huchagua lugha kulingana na kile watakachofanya na lugha hiyo.  Kwa mfano, uhusiano wao na watu wanaoongea nao na kile wanachozungumzia.  Ruwaza ya uwili-lugha hubadilika kila mara kulingana na kazi itakayotendwa na lugha iliyochaguliwa kutumika.  Tuchukue mfano wa Kamau.

Kamau ameishi Ujerumani kwa miaka kadhaa. Anaporudi nyumbani anaenda benki na anaomba kumuona meneja wa benki.  Mara, anatambua kuwa hawezi kujieleza vilivyo kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu hajawahi kuwa na majadiliano ya aina hii kwa Kiswahili.  Itambidi achague lugha nyingine ambayo hasa ni Kingereza ili kuwasiliana na meneja.

Kuna hali nyingi ambazo wana uwili lugha wanaweza kujieleza vizuri kwa lugha moja kuliko katika lugha nyingine.  Lakini hii haimaanishi kuwa hawatawaelewa wenzao wanapozungumza katika lugha nyingine.  Swali muhimu la kuuliza hapa ni hili: Lugha hizo mbili zina dhima gani kwa mzungumzaji?

3.    Uingiliaji
Kuna tajriba fulani katika maisha ambazo huwafanya watu waweze kujieleza vizuri kwa lugha moja kuliko nyingine.  Hii haimaanishi kuwa hawaielewi lugha hiyo.  Tatizo ni kwamba wao hujikuta kuwa hawalipati neno mwafaka ambalo wanaweza kulitumia wanapozungumzia mada fulani.  Weinreich (1953) anadai kuwa uingiliaji ni ile hali ambayo ukiukaji wa kaida katika lugha hutokea katika mazungumzo ya wana uwili-lugha kutokana na wao kujua zaidi ya lugha moja.  Uingiliaji unaweza kutokea katika viwango vyote.  Kwa mfano, unaweza kutokea katika kiwango cha fonolojia ambapo matamshi ya mtu yanakuwa kama yale yanayopatikana katika lugha nyingine.  Katika kiwango cha semantiki, mtu huweza kushindwa kuchagua neno linalofaa.  Ni rahisi kuona kuwa hata katika kiwango cha kisintaksia, uingiliaji huu hutokea hasa katika mpangilio wa maneno.  Swali muhimu la kujiuliza hapa ni hili: Ni kwa kiasi gani mzungumzaji anazitenga lugha hizi mbili au anaziunganisha?

4. Ubadilishaji
Katika hali hii tunaangalia kiasi ambacho mzungumzaji hubadili mazungumzo kutoka kwa lugha moja hadi nyingine.

Uwili Lugha Sambamba na Uwili Lugha Kimfuatano

Dhana hizi mbili zinatumiwa kueleza tofauti katika mpangilio wa kiutambuzi wa mwana uwili lugha.  Tofauti hizi zinatokana na ile miktadha ambayo mtu aliweza kuwa mwana uwili lugha.  Katika uwili lugha sambamba, mtu anajifunza lugha mbili wakati mmoja na katika muktadha ule ule mmoja ambamo lugha hizo zinatumiwa pamoja.  Kwa hivyo anatumia lugha mbili kwa kuzibadili.  Kwa mfano, mtoto aliyejifunza Kiswahili na Kiingereza kutoka kwa wazazi wake nyumbani atajua maneno ‘kitabu’ na ‘book’, na atakuwa na maana moja kwa majina hayo tofauti.  Maneno hayo mawili yataunganishwa au kusimamiwa na dhana moja akilini mwake.
        Kitabu        =        book

    /kitabu/                /bƱk/

Hii ina maana kwamba dhana moja itakuwa na vitaja viwili.  Katika hali hii, lugha hizi mbili hutegemeana.  Basi utagundua kuwa uwili lugha sambamba huwa na seti moja ya maana iliyounganishwa kwa mifumo miwili ya maana.

Katika uwili lugha wa kimfuatano, mtu hujifunza kila lugha katika mazingira tofauti, na hata maneno ya lugha zile mbili hutenganishwa, kila neno likiwa na maana yake.  Katika hali hii kila lugha inajisimamia yenyewe.  Kwa mfano, mtu anaweza kujifunza lugha moja nyumbani na baadaye akajifunza lugha ya pili shuleni au kazini.  Kila lugha ambayo amejifunza itatumika kulingana na uhitaji wa mazingira yaliyopo (kazini au shuleni).  Kwa hivyo kila lugha inahusishwa na miktadha tofauti na mifumo yake ya fikra inakuzwa kwa njia tofauti.  Hii ina maana kwamba akijifunza neno la Kiswhaili ‘kitabu’ halafu ajifunze neno la Kiingereza ‘book’, maneno haya yatakuwa kila moja na maana mahsusi, hayataunganishwa akilini mwake kama dhana moja.  Itakuwa hivi:
        Kitabu                book

        /kitabu/            /bƱk/
Uwili lugha wa kimfuatano huwa na seti mbili za maana zilizounganishwa kwa mifumo miwili tofauti ya kiisimu.
Swali:
a.                   Je, wewe ni mwana uwili-lugha?
b.                   Eleza jinsi ulivyopata kuwa mwana uwili-lugha.

Athari za Uwili Lugha

Kuna athari nyingi za uwili lugha.  Baadhi ya athari hizo ni hizi:
i.                        Lugha moja itakopa maneno kutoka kwa nyingine. Kwa mfano, Kiswahili kilikopa sana kutoka kwa Kiarabu.
ii.                        Kuna uwezekano wa lugha moja kufa au kupotea kabisa.
iii.                        Muundo na hata msamiati wa lugha hizo utabadilika baada ya muda mrefu hata tukapata lugha mchanganyiko (Pijini au Krioli).
iv.                        Wazungumzaji wa lugha moja wataihama lugha yao na kuzungumza tu ile ya pili.  Kwa mfano, Wasuba walipoingiliana na Wajaluo walijikuta, baada ya muda mrefu, wakiwa wameiacha lugha yao na wanazungumza Kijaluo.
v.                        Kunaweza kutokea sarufi mbovu katika lugha zote au moja.
vi.                        Mzungumzaji atakuwa anabadili msimbo.
Kama namna tu ya kutoa mfano, tutajadili athari mbili, yaani kubadili msimbo na pijini/krioli, kwa upana zaidi.

Kubadili Msimbo

Tumeona kuwa mwana-uwili lugha anao uwezo wa kubadilisha mazungumzo kutoka lugha moja hadi nyingine.  Hii ni mbinu ambayo haiwezi kutekelezwa na mwana lugha moja.  Mbinu hii ndiyo tunaita kubadili msimbo au ubadilishaji msimbo.

Swali:
  Kubadili msimbo ni kufanya nini?

Ubadilishaji msimbo ni dhana inayotokea katika hali ya uwili-lugha, ambapo wana uwili-lugha huongea na wana uwili-lugha wenzao, na hivyo basi kutumia malighafi ya  lugha zote katika mawasiliano yao.

Kwa mtu ambaye hazungumzi lugha mbili, ubadilishaji msimbo waweza kuonekana kama jambo linalokanganya.  Hata inakuwa vigumu kufikiria kuwa mbinu hii inafuata sheria zozote au inampa mwana uwili-lugha nafasi zaidi ya kujieleza.

Ni kweli kwamba baadhi ya watu huchukulia ubadilishaji msimbo kuwa ni ishara ya kuoza kwa ule uwezo wa kiisimu.  Wanaona kuwa kubadili msimbo ni matokeo ya kutojua lugha moja vilivyo. Lakini maoni haya sio kweli kwa sababu hali hii ni halisi palipo na uwili-lugha au wingi lugha.

Swali:


Je, unafikiria kuna sababu za kubadilisha msimbo?

Kubadilisha msimbo husababishwa na mambo kadha.  Watu hubadilisha msimbo hasa wanapokosa kupata neno mwafaka au maelezo mwafuaka katika lugha wanayoitumia, au kwa sababu hawawezi kulikumbuka neno hilo au kwa sababu lugha hiyo inaonekana kuwa haielezi vizuri dhana wanazozungumzia.  Hivyo basi, mzungumzaji hubadili na kwenda kwa lugha ya pili ili kufidia upungufu huu.  
Vile vile mada fulani huweza kujadiliwa vizuri katika lugha moja kuliko lugha nyingine. Kubadili msimbo kwa aina hii huwa na dhima ya urejeshi.

Lugha pia hubadilishwa kama ishara ya kuonyesha umoja na yule mtu anayezungumziwa.  Hii inamaanisha kwamba mtu anatumia kubadilisha kwa lugha kama kuendeleza ule umoja au uhusiano.

Kwa mfano, mtu anaweza kubadili msimbo kutoka kwa lugha rasmi au lugha ya taifa hadi lugha ya kwanza.  Katika mazungumzo kama haya mzungumzaji huwa na nia ya kumhusisha mtu mwingine zaidi katika mazungumzo.

Vile vile, inaweza kuwa ni nia ya kumtenga mtu asiyeifahamu lugha fulani kutokana na mazungumzo yanayoendelea.  Hata hivyo, jambo hili lisichukuliwe kila mara kuwa ni ishara ya mwelekeo hasi kwa mtu asiyeelewa lugha nyingine.  Kubadili msimbo kwa aina hii huwa na dhima elekezi.

Ubadilishaji msimbo unaweza kutumika kusisitiza kauli fulani na kisha kuibuka mshindi katika mjadala fulani.  Katika hali hiyo hiyo, kubadili msimbo kunaweza kutumiwa kuonyesha hisia za mzungumzaji kwa msikilizaji hasa hisia za kirafiki au kuchukizwa, kejeli au mzaha.

Watu wanaotumia lugha moja huwasilisha hisia hizi kwa kubadili kiwango cha urasmi katika kauli zao lakini wana uwili-lugha, hutekeleza jambo hili kwa kubadili msimbo. Kwa mfano, ikiwa wana uwili-lugha wawili huzungumziana wakitumia lugha X, uteuzi wa lugha Y utaleta athari ya kipekee.  Mfano mwingine ni wakati mama anayetumia lugha ya mama au lugha ya taifa anapobadilisha lugha yake na kutumia Kiingereza kwa mtoto wake ili kuonyesha msisitizo au kuudhika kwa yale anayoyasema.  Kubadili msimbo kwa aina hii huwa na dhima elezi.

Tazama mfano huu (Juma aliye na umri wa miaka mitano anacheza nje).
Mama:  Juma njoo, chakula ki tayari.
Juma:    (anaendelea kucheza nje)
Mama:  Ju  - ma!  Njoo!
Juma:  (hasemi chochote)
Mama:  Juma Hasan, Come here!
Juma:    O.K. Naja, mama.
Zoezi:

Fafanua sababu mbalimbali zinazomfanya mzungumzaji kubadili msimbo.

Namna ya Kubadili Msimbo

Kuna njia nyingi za kubadili msimbo.  Ukiwasikiliza watu wakiongea utaona kuwa kuna namna fulani ya miundo ambayo hujitokeza katika mazungumzo yao.  Hebu basi tuone ni vipi watu hubadili msimbo.

1.    Kubadili vishikizo
Kishikizo ni msemo unaonukuliwa mara nyingi na watu.  Tunaposikiliza wana uwili lugha wakizungumza, tunaona kuwa huwa wanaingiza kishikizo cha lugha moja katika kauli au taarifa iliyo katika lugha nyingine.Kila lugha hutumia sauti fulani kuonyesha mishangao.  Hivyo basi sauti hizi za mishangao, uwe wa furaha au huzuni huweza kutumiwa pamoja na lugha nyingine.  Kwa mfano:
1)    Wau, unaoneka maridadi leo!
2)    You see, kama nilivyokuwa nikisema…….
3)    Salale, is it you?

Maneno yote yaliyopigiwa mstari ni maneno yanayoonyesha mshangao na yametumiwa kwa lugha tofauti na yale ya sentensi nzima.  Vishikizo hivi huingizwa mahali popote katika sentensi bila kuvunja sheria za kisintaksia za lugha nyingine.

Vishikizo vingine vinavyotumiwa sana ni you know, I mean, yeah, aisee, ngai.

2.    Kubadili msimbo baina ya sentensi
Huku ni kule kubadili msimbo katika mipaka ya kishazi au sentensi ambapo  kishazi au sentensi hiyo huwa katika lugha moja na sentensi nyingine katika lugha ya pili.

Kubadili msimbo kwa aina hii huhitaji ufasaha wa hali ya juu katika lugha mbili zinazohusika.  Hii inamaanisha kuwa mzungumzaji lazima afahamu vizuri sheria za kisarufi za lugha zote mbili.  Kwa mfano.
“I’ll start a sentence in English.  Kisha niikamilishe kwa Kiswahili”.
“I have come to inform you that, Mwalimu mkuu anataka kusema nawe”.
“Najua nimekosa, but what do you want?”

3.    Kubadili msimbo ndani ya Sentensi
Katika aina hii ya msimbo, msimbo hubadilishwa ndani ya kishazi au sentensi. Aina hii  ndiyo hujulikana kama kuchanganya msimbo.  Ni aina tata zaidi ya kubadili msimbo.  Kwa mfano, mtu anaweza kutamka sentensi kama hii, “Ninaenda mjini kufanya shopping”.  Katika sentensi hii tunaona kuwa kauli haikukamilika kabla ya mzungumzaji kuongeza neno la Kiingereza shopping.
Mfano mwingine ni huu: “Ninaenda gichagi kumtembelea mama”.  Pia aina hii huwa na maana ya kuchanganya msimbo katika mipaka ya neno.  Kwa mfano:
    Alimpush mpaka akapata kazi nzuri.
    Alienda tao.
Zoezi:

Huku ukitumia jamii yako kama mfano, andika sentensi tano kuonyesha namna  wana-uwili lugha hubadili msimbo kutoka kwa lugha moja hadi nyingine.

Pijini

Kuna njia nyingine kando na kubadilisha msimbo au kukopa maneno ambayo kwayo lugha inaweza kujipata imechanganyikana na nyingine.  Katika hali hii lugha mpya (moja au zaidi) huibuka kutokana na zile zilizopo.  Harakati inayojitokeza wazi ni ile inayojulikana kama upijini ambapo tunapata aina za lugha zinazojulikana kama pijini.

Pijini ni aina ya lugha inayojitokeza panapotokea mtagusano au mwingiliano wa watu wanaozungumza lugha tofauti.  Ni lugha ambayo hubuniwa na kutumiwa kwa mawasiliano baina ya watu ambao lugha zao ni tofauti na watu hawa hawana lugha moja nyingine wanayoielewa wote ili waitumie katika mawasiliano yao.  Kulingana na wanaisimu Yule (1996:234) na Hudson (1993:61) inakisiwa kwamba neno pijini linatokana na matamshi mabaya ya Kichina ya neno la Kiingereza business.

Kuibuka kwa Pijini

Wanajamii katika hali hii hujifunza lugha hiyo kutoka kwa wenzao kama njia iliyokubalika ya kuwasiliana na watu kutoka jamii nyingine.  Sababu moja kuu ya kutaka kuwasiliana na watu wengine huwa ni katika biashara.  Na lugha hiyo huwa haitumiwi na wanajamii wenyewe kwa wenyewe ila tu na wageni.

Kunazo pijini mbalimbali ambazo zimesambaa kote ulimwenguni zikiwemo sehemu za Uropa ambapo wahamiaji katika nchi kama vile Ujerumani, wameunda pijini kwa kuzingatia misingi ya lugha ya taifa ya nchi hiyo. Mfano wa pijini iliyoibuka katika hali hii ni Tok Pisini.  Hii ni pijini iliyo na misingi ya Kiingereza inayozungumzwa New Guinea na katika visiwa jirani.  Hii iliibuka ili kuendeleza mawasiliano kati ya watawala wa Kizungu na wenyeji ambao hawa wenyewe wana lugha ambazo ni tofauti na hivyo basi hawaelewani wenyewe kwa wenyewe.  Kipijini hiki hakikufaa tu wale wazungu bali kiliwafaa na wenyeji pia.

Tukumbuke kuwa sio pijini zote zimeibuka kama lugha za kibiashara kama ilivyo lugha ya Tok Pisin.  Hali nyingine ambayo imesababisha kuzuka kwa pijini ni pale ambapo watu wanaozungumza lugha tofauti wanawekwa pamoja na ni lazima wawasiliane miongoni mwao na hata wawasiliane na wale wenye nguvu.  Hali hii ilitokea katika bara la Afrika ambapo Waafrika walichukuliwa kuwa watumwa na kupelekwa katika “ulimwengu mpya”.  Kila mara mabwana waliwatenga watu waliozungumza lugha moja ili kuepuka swala la uasi miongoni mwa Waafrika.  Njia moja ambayo watumwa wangewasiliana na wenzao au mabwana zao ilikuwa kupitia kipijini ambacho walijifunza kutoka kwa mabwana zao na hata wao wenyewe kukibuni.  Hata hivyo, utaona kuwa kipijini hiki kilikuwa na misingi yake katika lugha za mabwana.
Swali:

Unaweza kufikiria juu ya hali zingine ambazo pijini inaweza kuibuka?

Sifa za Pijini

1.    Pijini huwa hazina wazunguzaji asilia.  Hii inamaanisha kuwa hakuna watu wanaoweza kudai kuwa hii ni lugha yao ya mzazi.  Tumeona sababu za kuzuka kwa lugha hii na hivyo basi lugha hii haiwatambulishi watu kijamii.

2.  Msamiati

Pijini huchukua msamiati kutoka kwa lugha zote mbili ili kuwezesha mawasiliano ya kimsingi.  Lugha ambayo huchangia msamiati mwingi ni ile lugha yenye watumiaji wengi au lugha yenye nguvu.  Kwa mfano, ikiwa kuna wahamiaji wanaozungumza Kizulu (lugha moja ya Afrika Kusini) na wameenda kuishi Nyeri na hawana lugha nyingine ya kuwasiliana na wenyeji, basi watu hawa hawatafaidika ikiwa msamiati wao utakuwa na maneno mengi ya Kizulu.  Hii ni kwa sababu wakaazi wa Nyeri sio watakaojifunza Kizulu ndio watakaojifunza Kikuyu. Hivyo basi Wazulu hawa watalazimika kutumia msamiati wa lugha ya walio wengi yaani Wakikuyu.

Kwa upande mwingine tunaona kuwa katika hali ya ukoloni ambapo wawakilishi wa nchi ya ukoloni wanahitajika kuwasiliana na wenyeji kuhusiana na maswala ya biashara au utawala, na ikiwa mambo haya yatahitaji wenyeji kuwasiliana na wawakilishi hawa kwa manufaa yao, basi ile pijini ambayo itaibuka itakuwa na msamiati unaoegemea kwenye lugha ya wawakilishi hawa wa kikoloni.  Hii ndiyo sababu tunapata pijini nyingi zilizo na msingi katika lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kidachi.

Hata ingawa msamiati utakuwa ni wa lugha yenye nguvu, zile lugha nyingine pia hutoa mchango.  Hivyo basi kuifanya pijini kuwa rahisi kujifunza kuliko ilivyo katika kujifunza lugha yenye nguvu katika hali yake ya kawaida.

3.  Othografia
Lugha hizi hazina othografia wala fasihi.  Hazijaandikwa kwa sababu zina matumizi mengi yanayohitilafiana.

4. Uradidi

Sifa nyingine (ya kimuundo) inayojitokeza katika pijini ni uradidi.  Huku ni kule kurudia maneno katika sentensi ili kusisitiza maana yake.  Kwa mfano, maneno kama big big child  (A big child).  Big big yamerudiwa ili kuonyesha unene wa mtoto anayezungumziwa.  Hii ni njia ya kufidia upungufu wa msamiati.
Kumbuka:

Ni vizuri tukumbuke kuwa, ikiwa pijini inayo misingi yake katika lugha fulani, tuseme X, hii haimaanishi kuwa pijini hiyo ni mfano wa lugha X ambayo imetumika vibaya.  Hatuwezi kufananisha matumizi ya lugha ya mtu anayejifundisha lugha X na pijini iliyo na misingi ya lugha hiyo X.

Utumiaji wa Ishara

Watumiaji wa pijini mara nyingi hutumia miondoko au ishara za mikono ili kujaliza mawasiliano katika lugha hiyo.  Baada  ya muda lugha hii hujenga historia yake.  Hivyo basi, hizi ni lugha ambazo haziwezi kupuuzwa kwa sababu kulingana na wataalamu wa isimu-jamii, inakisiwa kuwa takribani watu milioni kumi na mbili bado wanatumia lugha za pijini.
6.  Mkururo wa vitenzi hupatikana sana katika pijini.  Kwa mfano, hapa kuna sentensi kutoka kwa Pijini ya Cameroon:

    ‘dat chif i woman i go stat bigin tich i, tכk sei na so dem di mekam’

Tafsiri sisisi ya sentensi hii ni kama ifuatavyo:
‘that chief he woman he go start begin teach he talk say be so they habitually make it’
Kwa Kiingereza sanifu, haya ndiyo yanayoelezwa katika sentensi hiyo ya kwanza:

‘tha tthe chief’s wife set out to teach her, saying that is how it is usually done’

7.      Pijini aghalabu huwa na fonolojia sahili.
Sauti za konsonanti na vokali zinazopatikana katika pijini huwa ni chache na zisizo na utata wa kimatamshi na kimpangilio zikilinganishwa na zile zilizo katika lugha sanifu.
8.    Aidha, pijini huwa na sarufi rahisi.  Ule mfumo tata wa kimofolojia wa lugha asilia huepukwa.  Sentensi zinakuwa rahisi.  Aghalabu hakuna upatano wa kisarufi kati ya kiima na kiarifu.

Mifano ya Pijini

1.       Kipijini cha Cameroon.
2.       Kipijini cha Asmara.
3.       Kipijini cha Kisetla – (Kenya)

Zoezi:

Zungumza Kiswahili na Mkenya mwenye asili ya Kihindi.  Andika sentensi kama kumi kutoka kwa mazungumzo yenu.  Zichambue uone kama zina sifa zo zote za pijini.

Krioli

Tulipozungumzia lugha za pijini, tuliona kuwa sifa moja ya lugha hizi ni kwamba huwa hazina wazungumzaji asilia, yaani hakuna watu wanaoweza kudai kuwa lugha hiyo ni lugha ya mama.

Ni muhimu kusema hapa kuwa lugha za pijini zinapoibuka huwa hazifi mara moja.  Hii inamaanisha kuwa watu huendelea kuzitumia.  Inapotokea hivyo, pijini hukua hadi kufikia kiwango cha kuwa na wazungumzaji asilia.  Hali hii hutokea pale ambapo wazazi walio na watoto huwalea watoto hao pamoja wakitumia pijini.  Hii inamaanisha kuwa lugha hii si ya kibiashara tena, bali sasa inatumika kama lugha ya kwanza ya watoto hawa.  Inapofika kiwango hiki, ndipo sasa tunaanza kusema kuwa lugha hizi  ni krioli.

Swali:

Je, unafikiria krioli ni lugha gani?

Krioli hutokana na pijini kukua na kufikia kiwango cha lugha ya kwanza kwa watoto ambao wanazaliwa na wazazi wanaozungumza pijini.  Tofauti na pijini, krioli huwa na wazungumzaji wengi.  Inakisiwa kuwa takribani watu milioni kati ya kumi na kumi na saba huzungumza krioli ulimwenguni.  Kwa mfano, krioli iliyo na misingi ya Kifaransa inazungumzwa na idadi kubwa ya watu kule Haiti na krioli zilizo na misingi ya Kiingereza zinatumika Jamaica na Sierra Leone.

Lugha nyingi za krioli zinazozungumzwa na vizalia wa watumwa wa Afrika hutumika kama chombo cha kupashia habari kuhusiana na asili yao na vile vile kama ishara ya utambulisho wao.

Pijini inapokua na kufikia, krioli inachukuliwa kama lugha nyingenezo isipokuwa katika asili au chanzo chake ndicho huwa tofauti.  Hii ni kwa sababu krioli huwa zimepanua matumizi yake kiasi kwamba sajili mbalimbali huweza kutumia lugha hii.  Kutokana na hali hii lugha hii hupanua msamiati wake.  Hii ina maana kuwa inaweza kutumika katika shughuli rasmi kama vile shuleni, bungeni na kadhalika.  Vile vile muundo wake wa sarufi huimarishwa na kuwa changamano.

Tunaweza kusema kuwa krioli ni lugha ya kwanza kwa watu fulani ambao walikulia katika mazingira ya kipijini peke yake.  Hivyo basi katika ule ujifunzaji wake, watu wanajifunza pijini kama ni lugha ya kwanza wala sio lugha ya pili.

Swali:

Je, unafikiri Sheng ni pijini au krioli?  Fafanua.

Muhtasari:

Katika somo hili, tumezungumzia dhana za kimsingi katika lugha.  Tumeeleza tofauti iliyopo baina ya umilisi na utendaji; ‘langue’ na ‘parole’; lafudhi na lahaja; lugha sanifu, jumuia lugha,  uwili lugha, wingi lugha, pijini na krioli.  Vile vile tumeeleza athari ya hali hizi katika lugha.

Maelezo ya dhana:

Lugha-wenyeji    -    Lugha ya asili inayozungumzwa na wenyeji wa   
                                      nchi fulani.

Mtagusano         -     hali ya lugha mbili au zaidi kuathiriana kutokana
                                       na kukutana kwa namna fulani.

Sarufi zalishi    -    nadharia inayozingatia mfululizo wa   
                                      sheria zinazoeleza miundo ya sentensi na
                                      namna ya kuzalisha sentensi zaidi.

Ubadilishaji msimbo  -    Kutumia aina mbili tofauti za lugha kwenye
                                      makala moja wakati wa mawasiliano.



Marejeleo:
Angogo, R. (1980), “Linguistic and Attitudinal factors in the  Maintenance of Luyia
Group Identity”, Ph.D Thesis,  University of Texas,  Austin.

Bakari, M. (1982),  “The Morphophonology of Kenya Swahili Dialects”, Ph.D Thesis,
University of Nairobi.

Bloomfield, L. (1933) Language.  New York,  Hoilt Rinehart and Winston.

Bornstein, D. (1977), An Introduction to Transformational Grammar, Cambridge,                
                   Cambridge University Press.

Chiragdin, S. na Mnyampala M. (1977), Historia ya Kiswahili, Nairobi,  Oxford
University Press.

Fromkin, V. na Rodman, B. (1988), An Introduction to Language, Fort Worth,  Holt
Rinehart and Winston Inc.

Gumperz, J.J. (1962), ‘Social Network and Language Shift’ in J.J. Gumperz (ed)
Discourse Strategies, Cambridge,  Cambridge University Press.

Halliday, H. (1978), Language as Social Semiotic:  The Social Interpretation of
Language and Meaning,  London. Edward Arnold.

Harding E. na Riley, P. (1995), The Bilingual Family:  A Handbook for Parents,
                     Cambridge, Cambridge University Press.

Haugen, E. (1953), The Norwegian Language in America:  A Study of Bilingual
Behaviour,  Bloomington, Indiana University Press.

Hockett, C. (1958),  A Course in Modern Linguistics, New York, Macmillan.

Hymes, D. (1972), ‘Models of the Interaction of Language and Social Life’ in J.J.
Gumperz and D. Hymes (Eds) Directions in Sociolinguistics:  The Ethnography of Communication, New York and Oxford,  Basil Blackwell.

Labov, W. (1972),  Sociolinguistic Patterns,  Philadephia, University of Pennsylvania
                   Press.

Lyons, J. L. (ed) (1970), New Horizons in Linguistics, Harmondsworth,   
                   England, Penguin Books,

Mackey, W.F. (1962), “The Description of Bilingualism” Canadian Journal of
Linguistics, 7:518.

Massamba, D.P.B. na wengine (1999), Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu, TUKI,
Dar es Salaam.

Maundu, P.M. (1980),  Sound Change and the Reconstruction of Kikamba
Consonantal Sounds in Natural Generative Framework,  Masters Dissertation,  University of Nairobi.

Mbaabu, I. (1991) Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili,  Nairobi, Longman.

Mgullu, R.S. (1999) Mtalaa wa Isimu.  Nairobi,  Longhorn Publishers.

Musau, P. (1990) Kiswahili in the Twentieth Century, Nairobi, University of
                   Nairobi.

Mutahi, K. (1977) “Sound Change and the Classification of the Dialects of Southern
Mount Kenya”,  Ph.D Thesis,  University of Nairobi.

Muthwii, M. (ed) (2000),  Language Policy and Practices in Education in Kenya
and Uganda,  Nairobi, Phoenix Publishers.

Trudgill, P. (1983):  On Dialect, Oxford, Blackwell.

Wardhaugh, R. (1994),  Investigating Language:  Central Problems in Linguistics,  
Oxford, Blackwell.

Weinriech, U.  (1953),  Languages in Contact,  Mouton, The Hague.

Yule, G. (1996),  The Study of Language,   Cambridge,  Cambridge University
Press.
SOMO LA KUMI NA MOJA
UMUHIMU WA ISIMU KATIKA JAMII
Utangulizi
Katika kozi hii tumetoa kitangulizi na maelezo ya dhana ambazo utakumbana nazo katika masomo yako ya isimu baadaye.  Hata hivyo, labda unajiuliza je, isimu ina umuhimu gani katika maisha ya binadamu?  Katika somo hili tutaangalia maeneo yote ambayo isimu huifaidi jamii.  Tutaona jinsi ujuzi wa isimu huweza kunufaisha jamii.
Lengo:

Kufikia mwisho wa somo hili utaweza kueleza umuhimu wa isimu katika jamii.

Ni kweli kwamba watu wengi hawalihusishi somo la isimu na umuhimu wowote katika jamii  isipokuwa kuona kuwa ni somo linalomfaa tu mwanaisimu.Ukweli ni kwamba katika mawanda yote ya maisha ya binadamu, somo la isimu ni muhimu.  Isimu kama tulivyosema katika somo la tatu, ni uchunguzi wa lugha kisayansi.  Na lugha kama tulivyoona ni chombo muhimu sana cha mawasiliano miongoni mwa binadamu.
Swali:

Je, ni kwa njia gani isimu huwa muhimu?

1.    Ufunzaji wa Lugha

Wataalamu wengi wamekubaliana kuwa matumizi makubwa sana sasa hivi ya somo la isimu ni ufunzaji wa lugha.  Katika somo la nne, tumezungumza juu ya viwango vya isimu. Mwalimu yeyote anayefundisha lugha yo yote anapaswa kuelewa umbile la ndani la lugha anayofundisha na jinsi lugha hiyo inavyofanya kazi katika jamii ya wazungumzaji wake.

Ujuzi wa kiisimu, kwa mfano, utamsaidia mwalimu kumrekebisha mwanafunzi aliye na matatizo katika utamkaji wa maneno.  Utamkaji sahihi wa maneno ni muhimu sana kwa mtu anayejifunza lugha ya pili.  Mwalimu aliye na ujuzi wa kiisimu atafahamu kwa nini mwanafunzi anafanya kosa na itakuwa rahisi kwake kumsaidia.  Kwa mfano, ikiwa mwanafunzi hawezi kutamka sauti ‘th’ basi mwalimu atamwambia aweke ncha ya ulimi katikati ya meno anapoitamka.

Kupitia kwa somo la isimu-jamii (Tazama somo la tano) mwalimu pia anaweza kutambua nafasi ambayo lugha mbalimbali zinazotumika katika jamii husika hupewa.  Vile vile, kwa kutumia ujuzi wake wa kiisimu ataelewa mielekeo ya watu kuhusu lugha zinazozungumzwa katika maeneo yake na jinsi ya kukabiliana na mielekeo hiyo (Muthwii 2000).

2.    Tiba ya kimaongezi
Watu wengi huanza kujisaili kuhusu lugha  pale tu matatizo yanapotokea hasa wanaposhindwa kuzungumza tena baada ya ajali au mikasa mingine.  Watu hawa waliopata ajali wanaweza kuzungumza mambo yasiyoeleweka au hata kushindwa kudhibiti mazungumzo yao, au wakapoteza uwezo wa kuzungumza kabisa.  Watu kama hawa wanaweza kusaidiwa mradi tu kipengele cha lugha kilichotatizika kifahamike.  Vivyo hivyo, watoto wanaochelewa kuzungumza au wale walio na shida za kimaongezi wanaweza kusaidiwa.

Kipengele kinachohusika na kueleza namna matamshi yanavyotolewa ni kile cha fonetiki matamshi (Tazama maelezo katika somo la 4. (fonetiki).  Ili anayefunza lugha afanikiwe katika mafunzo ya ziada yafaayo kwa watu wenye shida ambao viungo vyao vya maongezi vina kasoro, vigugumizi au watu ambao hawakuzoea tangu awali kutamka sauti fulani, basi lazima atambue kipengele cha isimu kitakachomsaidia.   Mtaalamu huweza kutatua baadhi ya matatizo ya kimaongezi kwa kutumia maabara ya kiisimu ambamo atakuwa na vyombo vitakavyomsaidia mwenye kasoro kupata tiba.  Vifaa kama vioo vya kuangalia namna kinywa kinavyokaa na utembeaji wa viungo vilivyomo kinywani mtu anapotoa sauti fulani vitafaa.

Pia katika kufundisha viziwi, ufahamu wa fonetiki matamshi hasa viungo vya kinywa vinavyohusika katika utamkaji na mkao wavyo, utasaidia katika utamkaji sahihi.  Viziwi huangalia kwa makini sana mabadiliko ya midomo ya mzungumzaji anapotoa sauti mbalimbali.  Mabubu nao hufaidika kwani nadharia ya sintaksia husaidia kuhakiki na kutoa suluhisho kwa wale wanaotumia lugha-ishara.

3.    Tafsiri
Ufahamu wa isimu umeshatumika katika uwanja wa tafsiri ili kuchunguza na kubuni njia mwafaka za tafsiri.  Ujuzi wa kiisimu unahitajika katika kuipa tarakilishi au kompyuta utaratibu wa lugha unaofaa.  Mwanaismu anaipa kompyuta mashina ya maneno katika lugha asilia na lugha pokezi na kuonyesha jinsi lugha hizi zinavyoingiliana.  Ujuzi kama huu utarahisisha kazi katika mikutano ya kimataifa ambapo tafsiri zitafanywa kwa urahisi  na kwa haraka.

4.    Upangaji wa lugha
Ujuzi wa isimu ni muhimu katika aina nyingi za upangaji wa lugha kwa sababu:
a.                   Utungaji wa othografia ya lugha huhitaji ujuzi wa  kiisimu.  Othografia ni zile herufi zinazotumiwa katika lugha kuwasilisha sauti zilizo katika lugha hiyo.
b.                   Usanifishaji wa lugha ni kazi inayohitaji ujuzi wa kiisimu.

5.    Kuelewa tabia
Kuna haja ya kuchunguza lugha kwa sababu ndiyo inayotuwezesha kuelewa tabia za binadamu akiwa peke yake au anapoingiliana na wenzake.  Lugha na fikra vinahusiana sana hivi kwamba tunapoichunguza lugha tunaelewa zaidi jinsi akili ya binadamu inavyofanya kazi.

6.    Mhandisi wa  mawasiliano
Mhandisi wa mawasiliano anayeshughulika na mitambo hunufaika sana kutokana na ufahamu wa elementi za lugha-ishara ambazo anatumia kufanikisha kazi yake ya mawasiliano.  Kipengele cha isimu kinachotumika hapa ni kile cha fonetiki akustika (Tazama somo la nne).

Wahandisi hukadiria kiwango cha mawasiliano kinachopitia katika masafa mbalimbali.  Wao hutumia viwango mbalimbali vya mawasiliano ya lugha kama vile kupeleka ujumbe kwa kutumia waya au mawimbi ya redio, kipepesi (fax) barua-pepe na kadhalika.
Swali:

Ungemshawishi vipi mtu wa kawaida kuwa somo la isimu lina umuhimu kwa jamii?
   
Zoezi:

Hebu fikiria kuwa wewe ni mwalimu katika maeneo ambayo wanafunzi wako wanashindwa kutamka sauti za Kiswahili sanifu vizuri.  Ni kwa namna gani utatumia ujuzi wako wa kiisimu ili kuwasaidia?

Muhtasari:


Katika somo letu la mwisho, tumejaribu kuonyesha umuhimu wa isimu sio tu kwa kundi moja la watu yaani wanaisimu bali namna watu mbalimbali wanavyoweza kufaidika kutokana na somo hili.

Marejeleo:


Muthwii, M. (2000),  Language Policy and Practices in Education in Kenya      
                      and Uganda, Nairobi,  Phoenix Publishers.






















Maoni 8 :

  1. Well defined content...Asante Sana wahadhiri wetu wa lugha kuu la kiswahili

    JibuFuta
  2. NIMEFAIDIKA SANA KWA MSAADA MKUBWA MLIOTOWA. asanteni mbarikiwe.

    JibuFuta
  3. Asante lakini ungeweka tudownload

    JibuFuta
    Majibu
    1. Mtu anawezaje download hiyo kitu iko sawa kabisa

      Futa
  4. Nimeshukuru sana kwa kazi nzuri

    JibuFuta
  5. Jinsi ya kudownload VIP nimeipenda

    JibuFuta
  6. Asanteni sana kwa msahada wenu Mungu awabariki sana

    JibuFuta
  7. Asanteni sana Kwa mafunzo yenu muhimu ...nashukuru

    JibuFuta